MUHTASARI WA HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2017/18

                 UTANGULIZI
 
1.                 Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ndani ya Bunge lako Tukufu, ambayo imechambua Bajeti ya Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba sasa kutoa hoja kwamba Bunge lako likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Kazi za Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka 2016/17 na Vipaumbele vya Wizara kwa mwaka 2017/18. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya mapato na Matumizi ya Kawaida na Mpango wa Maendeleo wa Wizara kwa mwaka 2017/18.
2.                 Mheshimiwa Spika, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama hapa, napenda kuchukua fursa hii kwa heshima na unyenyekevu mkubwa kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake imara kwa nchi yetu na maelekezo yake ambayo yamekuwa dira sahihi katika utendaji wangu na katika kuimarisha huduma za Afya na ustawi wa jamii nchini. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuweka chachu katika kudhibiti matumizi ya madawa ya kulevya nchini ikiwa ni jitihada zake za kulinda afya za Watanzania hasa vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa letu. Kwa hali hiyo, Wizara yangu itaendelea kuelimisha na kuhimiza umma wa Watanzania kuhusu madhara yatokanayo na matumizi ya dawa ya kulevya.

3.                 Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miongozo na ushauri wake wa dhati hasa katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto na masuala ya kuwawezesha wanawake kiuchumi. Wizara yangu itaendelea kutumia taswira, ushawishi na uzoefu wake ili kujenga jamii ya watanzania inayowajali, kuwaheshimu na kuwaendeleza wanawake na wasichana.

4.                 Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake ambao umesaidia kuongeza ufanisi katika utendaji na kuimarisha huduma zinazotolewa na Wizara yangu. Aidha, naomba nimpongeze kwa hotuba yake aliyoiwasilisha kwenye Bunge hili ambayo imetoa dira ya jinsi Serikali itakavyotekeleza majukumu yake katika mwaka 2017/18.

5.                 Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe binafsi, kwa kuendelea kutekeleza majukumu yako kwa weledi katika kuliongoza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, nampongeza Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson (Mb.) na Wenyeviti wa Bunge kwa kusimamia vyema mijadala ndani ya Bunge.

6.                 Mheshimiwa Spika, napenda nimshukuru Mheshimiwa George Boniface Simbachawene (Mb) Waziri wa Nchi, OR- TAMISEMI kwa ushirikiano wake uliowezesha kusimamia na kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini hasa afya ya msingi. Pia, nawashukuru Mawaziri wa Wizara nyingine zote ambazo ushirikiano wao na Wizara yangu umechangia katika utoaji wa huduma za afya na maendeleo ya jamii.

7.                 Mheshimiwa Spika, kipekee napenda kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba (Mb), na Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb) kwa ushauri na maelekezo waliyoyatoa wakati wa maandalizi ya Bajeti hii. Aidha nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano mzuri wanaonipatia ikiwemo kutoa ushauri na maoni mbalimbali yenye lengo la kuboresha huduma za afya na ustawi wa jamii nchini. Ninawashukuru sana!
8.                 Mheshimiwa Spika, niwapongeze Waheshimiwa wote walioteuliwa kuwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi cha 2016/17. Ninawaahidi kuwapa ushirikiano ili tuendelee kuwatumikia wananchi kwa pamoja.

9.                 Mheshimiwa Spika, naomba kutoa pole kwako, Bunge lako Tukufu, kwa familia na wananchi wa Jimbo la Dimani kwa kifo cha Mheshimiwa Hafidh Ally Tahir na Dkt. Elly Marko Macha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum, CHADEMA. Aidha, natoa pole kwa watanzania wote, ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza ndugu na jamaa zao kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na magonjwa, ajali na majanga. Pia, natoa pole kwa wagonjwa na majeruhi wa ajali waliopo hospitalini na majumbani pamoja na wahanga wa vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia. Namuomba Mwenyezi Mungu awaponye haraka ili waweze kuendelea na ujenzi wa Taifa.

10.            Mheshimiwa Spika, Baada ya kusema hayo, ninapenda sasa kutoa maelezo kuhusu utekelezaji wa shughuli za Wizara kwa mwaka 2016/17, Vipaumbele vya Wizara kwa mwaka 2017/18 pamoja na maombi ya fedha ambazo zitaiwezesha Wizara yangu kutekeleza majukumu yake.
















II: MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI NAMPANGO WA MAENDELEO KWA MWAKA WA FEDHA 2016/17

11.            Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake, Wizara imeendelea kuzingatia Sera, Mipango na Mikakati mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ikiwa ni pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (2030), Dira ya Taifa ya Maendeleo (2025), Mpango wa II wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 - 2020/21), Sera ya Afya (2007), Mpango Mkakati wa IV wa Sekta ya Afya (2016 -2020) na Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM 2007 - 2017). Aidha tumezingatia Sera ya Taifa ya Wazee (2003), Sera ya Maendeleo ya Jamii (1996), Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008), Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000), Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (2001). Vilevile, Wizara imeendelea kutekeleza malengo yaliyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020.

Mapato na Matumizi ya Fedha - Fungu 52 (Afya)

12.            Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia mwezi Machi 2017, Wizara kupitia Fungu 52 imekusanya jumla ya Shilingi bilioni 118.7 sawa na asilimia 75 ya makadirio ya Shilingi bilioni 157.7 yaliyoidhinishwa kwa mwaka 2016/17. Usimamizi thabiti pamoja na matumizi ya mifumo ya Kielektroniki vimechangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa ufanisi huu.

13.            Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia mwezi Machi, 2017, jumla ya Shilingi bilioni 339.1 zilipokelewa ikiwa ni asilimia 43 ya fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara.(Shilingi bilioni 796.1). Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 205.3 sawa naasilimia 74 ni fedha za Matumizi ya Kawaida ikiwemo Mishahara na Shilingi 133.8 sawa na asilimia 26 ni fedha za Miradi ya Maendeleo. Aidha, tumepokea vifaa, vifaa tiba na dawa vyenye thamani ya Shilingi 256,238,088,964.00 kutoka Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa bajeti ya miradi ya maendeleo.

Fungu 53 - Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
14.            Mheshimiwa Spika, kupitia Fungu 53 Wizara ilitarajia kukusanya jumla ya Shilingi bilioni2.3. Vyanzo vya mapato ikiwa ni ada za wanafunzi katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na ada za Mashirika Yasio ya Kiserikali. Hadi kufikia mwezi Machi, 2017, makusanyo yalifikia Shilingi 930,281,152 sawa naasilimia 39.0.

15.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17, jumla ya Shilingi 49,857,955,920 ziliidhinishwa kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya Wizara kupitia Fungu hili. Hadi kufikia mwezi Machi, fedha za Matumizi Mengineyo Shilingi 4,950,097,864 zilipokelewa sawa na asilimia 28.4 ya bajeti iliyoidhinishwa na Shilingi 7,866,426,933 za Mishahara zilipokelewa sawa na asilimia 42.1 ya bajeti iliyoidhinishwa. Vilevile, katika bajeti ya miradi ya Maendeleo, Shilingi 497,718,250 zilipokelewa ambapo Shilingi 204,217,000.

16.            Mheshimiwa Spika, ifuatayo ni taarifa kuhusu majukumu yaliyotekelezwa na Wizara katika kipindi cha Julai 2016 hadi Machi 2017;





UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA SEKTA YA AFYA

HUDUMA ZA KINGA
Udhibiti wa Magonjwa ya Kuambukiza na Yasiyoyakuambukiza
17.            Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutoa huduma za kinga nchini ambazo zinajumuisha udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yasiyo ya kuambukiza, magonjwa yaliyokuwa hayapewa kipaumbele, huduma za uzazi na mtoto,lishe pamoja na utoaji wa elimu ya afya kwa umma. Katika kipindi cha 2016/17 Wizara kazi zilizotekelezwa ni pamoja na;

Huduma za Chanjo
18.            Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutoa huduma za Chanjo kulingana na Sera na Miongozo. Aidha, Wizara kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo, imehakikisha kuwepo kwa chanjo za kutosha kwa ajili ya huduma za chanjo kwa watoto na makundi mengine kwa kununua na kusambaza chanjo katika Mikoa na Halmashauri zote nchini ambapo jumla ya Shilingi bilioni 18 zimetumika. Utoaji wa huduma za uhakika wa chanjo imewezesha nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri katika utoaji wa huduma za chanjo kwa mwaka 2016, ambapo tuliweza kuvuka lengo kwa kufikia kiwango cha chanjo cha asilimia 97.

19.            Mheshimiwa Spika, Wizara imenunua magari 9 kwa ajili ya kuboresha huduma za usambazaji wa chanjo. Pia wizara ilinunua na kusambaza majokofu 317 ya kutunzia chanjo kwenye vituo vya huduma za afya nchini.

Usafi wa Mazingira
20.            Mheshimiwa Spika, Wizara iliendelea kuratibu awamu ya pili ya Kampeni ya Kitaifa ya Usafi wa Mazingira (2016-2021) ambapo katika mwaka 2016/17, jumla ya kaya 391,937 zimejenga vyoo bora, kati ya hizi, kaya 320,894 zina sehemu maalum ya kunawa mikono mara baada ya kutoka chooni. Katika kuongeza chachu ya ushindani katika kutekeleza Kampeni ya Kitaifa ya Usafi wa Mazingira, Wizara iliendesha mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira na kutoa zawadi mbalimbali kwa Halmashauri zilizofanya vyema. Katika mashindano hayo, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe iliibuka mshindi wa jumla kitaifa na kukabidhiwa zawadi ya gari jipya aina ya Toyota Hardtop 4WD. Aidha, Wizara ilinunua na kugawa jumla ya pikipiki kwa Halmashauri 100 nchini hususani za vijijini.

Udhibiti wa Magonywa yaliyokuwa hayapewa kipaumbele
21.            Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mpango wa Taifa ya Kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa hayapewa kipaumble imeendea kugawa dawa za kingatiba za matende, mabusha, usubi, trakoma, kichocho na minyoo ktk Halmashauri 71 zenye maambukizi ambapo watu million 14.3 walifikiwa. Aidha upasuaji wa matende na mabusha bila malipo umefanywa kwa wagonjwa 805 katika Halmashauri za Temeke na Ilala na 100 katika Mkoa wa Mwanza.

Udhibiti wa Malaria
22.            Mheshimiwa Spika, katika kuendelea na mapambano dhidi ya Malaria, Wizara imesambaza dawa za kutibu malaria na vipimo vya kupima malaria (mRDT) kwenye mikoa 26 ya Tanzania Bara. Katika kipindi cha Julai 2016 hadi Machi 2017, jumla ya dozi za  dawa mseto (ALU) milioni 12.5 na Vitepe vya mRDT  milioni 15.5 vimenunuliwa na kusambazwa katika vituo vya huduma za afya nchini pamoja na kuhamasisha  matumizi ya kipimo cha mRDT. Vile vile unyunyiziaji wa dawa ukoka umefanyika katika mikoa 4 ya Kanda ya Ziwa ambayo ina maambukizi makubwa zaidi ya malaria ambayo ni (Kagera, Mwanza, Mara na Geita). Pia kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu imetekelezwa katika Halmashauri ya Kilombero - Morogoro na Halmashauri zote za Mkoa wa DSM. Jumla ya vyandarua milioni 2.6 vilinunuliwa na kusambazwa katika Halmashauri hizo.
Udhibiti wa Kifua Kikuu na Ukoma
23.                        Mheshimiwa Spika, huduma za kifua kikuu na Ukoma zimeendelea kuimarika nchini ambapo mafanikio makubwa yameendelea kupatikana. Kwa hivi sasa kiwango cha wagonjwa wanaotibiwa na kuponani asilimia 90 kati ya waliogunduliwa kuugua kifua kikuu.Wizara imeendelea kuboresha huduma za vipimo kwa kuimarisha maabara 4 za Kandaya Mbeya (Hospitali ya Rufaa Mbeya), Mwanza (Bugando Medical Centre), Dodoma (Hospitali ya Rufaa ya Mkoa) na Kilimanjaro (Hospitali ya Kibong’oto) ambazo zimeweza kufunguliwa na kuanza kutoa huduma za uchunguzi wa vimelea vya kifua kikuu.Hapo awali huduma hii ilikuwa inapatikana katika maabara moja tu iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

24.                        Mheshimiwa Spika, huduma za uchunguzi na matibabu yakifua kikuu sugu zimeimarishwa na kusogezwa karibu na wananchi kutoka Hospitali moja ya Kibongoto hadi Vituo 18  Aidha, shughuli mbalimbali za uelimishaji na uhamasishaji jamii kuhusu Kifua Kikuu zilitekelezwa ikiwemo kuendesha Kampeni kupitia vyombo vya habari (TV, Radio) yenye lengo la kuibua wagonjwa wapya wa kifua kikuu kwa kuwa ni asilimia 39 tu kati ya wagonjwa 162,000 waliopo nchini ndio walio katika matibabu.Tunamshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza mapambano dhidi ya kifua kikuu nchini. Nisisitize kuwa Kifua Kikuu Kinatibika na Huduma za Kupima na Matibabu hutolewa bila Malipo.

Udhibiti wa UKIMWI
25.            Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kudhibiti UKIMWI kwa kutoa ushauri nasaha na kupima virusi vya UKIMWI (VVU) pamoja na kutoa dawa za watu wenye maambukizi ya Virusi vya VVU/UKIMWI (WAVIU). Kuanzia mwezi Januari hadi Desemba, 2016 jumla ya wateja wapya milioni 7.4 walipata ushauri nasaha na kupima VVU.

26.            Mheshimiwa Spika, kuanzia mwezi Oktoba 2016, Wizara ilianza kutoa dawa za ARV kwa watu wenye maambukizi ya Virusi vya VVU/UKIMWI (WAVIU) bila kujali kiwango cha CD4 ambapo hadi Machi 2017 jumla ya WAVIU wanaotumia ART/ARV ni 849,594 ambayo ni sawa na asilimia 60 ya watu million 1.4 wanaokadiriwa kuwa na maambukizi ya VVU nchini. Kati ya hao watoto 55,670 wako kwenye matibabu ya ARV. Pia, Wizara imefunga mashine mpya 14 za kupima uwingi wa virusi vya UKIMWI (viral load) katika damu katika hospitali za rufaa za mikoa ya Mtwara, Dodoma, Tabora, Iringa, Morogoro, Arusha, Ruvuma, Kagera na Rukwa na Hospitali za Rufaa za Kanda - Bugando, Mbeya, KCMC, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Maabara ya Taifa ya Viwango na Ubora.

27.            Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutekeleza afua ya tohara kwa wanaume kama mojawapo ya afua ya kupambana na maambukizi ya VVU. Kuanzia mwezi Januari hadi Desemba, 2016 jumla ya wanaume 374,411 kati ya lengo la wanaume 492,844 wenye umri wa kati ya miaka 10 hadi 49 wamepata huduma ya Tohara kutoka mikoa 14 ya kipaumbele.

Udhibiti wa Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza
28.            Mheshimiwa Spika; kutokana na ongezeko kubwa la Magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile Kisukari, Shinikizo la Damu na Magonjwa ya Moyo, Wizara imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa kupambana na magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza wa 2016 – 2020 ambao ulizinduliwa Dodoma mwezi Novemba 2016. Hatua hiyo ilifuatiwa nakuanzishwa kwa Kampeni ya Kitaifa inayolenga katika kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi na kupima afya mara kwa mara na kuzingatia ulaji wa vyakula unaofaa. Kampeni hiyo ilizinduliwa na Mhe. Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan mwezi Desemba 2016 jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine Mhe. Makamu wa Rais aliagiza kuwa kila Jumamosi ya Pili ya Mwezi iwe ni Siku ya Hamasa ya Kufanya Mazoezi. Afya Yako Mtaji Wako

29.            Aidha Wizara iliendelea na jitahada mbalimbali zenye lengo la kuelimisha jamii juu ya madhara ya Tumbaku. Kuanzia Januari 2017, Kanuni za Kudhibiti Tumbaku zinataka maandishi ya onyo “uvutaji wa Sigara una madhara” yawe yenye ukubwa wa asilimia 30 ili yaweze kuonekana mazuri

Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto
30.               Mheshimiwa Spika, Upatikanaji wa huduma inayofikiwa na wanawake wote, kabla ya ujauzito, wakati wa ujauzito, na wakati wa kujifungua hadi wiki sita baada ya kujifungua ni muhimili muhimu  wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi. Hata hivyo, tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi bado ni changamoto. Tafiti zilizofanyika hapa nchini mwaka 2015 zinaonyesha kwamba idadi ya vifo ni 556 kwa kila vizazi hai 100,000. Katika kuimarisha huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto nchini, Wizara imeandaa Mpango Mkakati wa miaka 5 wa mwaka 2016 hadi 2020 unaolenga kuboresha afya ya uzazi, watoto na vijana pamoja na mambo mengine kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kufikia 292 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2020. Katika kutekeleza mkakati huo, Wizara imezingatia maeneo makuu matatu: ambayo ni:huduma ya uzazi wa mpango,huduma wakati wa ujauzito na huduma wakati wa kujifungua.

31.            Mheshimiwa Spika, kuhusu huduma za uzazi wa mpango, Wizara imekuwa ikitekeleza afua mbalimbali ili kuhakikisha kwamba huduma hii inapatikana kwa wote wanaoihitaji. Katika kipindi cha Julai 2016 hadi Machi 2017, jumla ya wateja 357,244 walifikiwa kupitia huduma za mkoba na 2,509,280 walifikiwa kupitia vituo vya kutolea huduma za afya. Wizara imenunua na kusambaza dawa za uzazi wa mpango.Utekelezaji wa afua hizo umewezesha kiwango cha kutumia uzazi wa mpango kupanda kutoka asilimia 27 mwaka 2010 hadi asilimia 32 mwaka 2015/16 (TDHS, 2015). Lengo ni kufikia asilimia 45 mwaka 2020.



32.            Mheshimiwa Spika, imebainika kuwa matatizo mengi wakati wa ujauzito yanaweza kuzuilika, kugundulika na kutibiwa kama wanawake wajawazito watahudhuria kliniki ya wajawazito na kupimwa na wahudumu wenye ujuzi. Katika kipindi cha 2016/17, Wizara iliendelea kuhakikisha huduma kwa wanawake wajawazitozinapatikana sambamba na kuelimisha wajawazito kuhudhuria kliniki.Kulingana na tafiti zilizofanyika mwaka 2015/16 asilimia 98 ya wajawazito wote walihudhuria kliniki angalau mara moja na asilimia 51 walihudhuria angalau mara 4 ambacho ni kiwango cha chini cha mahudhurio kinachopendekezwa. Lengo ni kufikisha asilimia 70 ya wanawake wajawazito kuhudhuria kliniki angalau mara 4 katika kipindi cha ujauzito ifikapo mwaka 2020. Nitumie fursa hii kuwahimiza akinamama wajawazito kuhudhuria kliniki angalau mara nne katika kipindi cha ujauzito wao ili kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi vinavyoepukika.

33.            Mheshimiwa Spika, upatikanaji wahuduma wakati wa kujifungua ikiwemo huduma ya dharura wakati wa kujifungua hadi wiki sita baada ya kujifungua, ni muhimu sana ili kuepuka vifo vitokanavyo na uzazi. Huduma kwa matatizo haya hupatikana tu kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya na mtoa huduma mwenye ujuzi. Katika mwaka 2016/17, Wizara kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuhamasisha na kuhimiza wanawake wajawazito kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma.Idadi ya akinamama wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma imeongezeka kutoka asilimia 51 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 64 mwaka 2015/16. Napenda kutoa wito kwa wanawake wajawazito wote nchini wajifungulie kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya ili kupunguza vifo na changamoto za uzazi kwa mama na mtoto.

34.            Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na OR - TAMISEMI, imekamilisha ukarabati wa vituo vya afya 8 katika Mikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu na Mara ili kusogeza huduma karibu na wananchi za uzazi za dharura ikiwemo upasuaji wa kutoa mtoto tumboni (CEmONC). Hadi sasa, Kati ya Vituo vya Afya 473 vinavyomilikiwa na Serikali ni vituo vya Afya 117sawa na asilimia 21 ndio vinatoa huduma za uzazi za dharura ikiwemo upasuaji wa kutoa mtoto tumboni.Lengo la serikali ni kuhakikisha angalau asilimia50 ya vituo vya afya nchini vinatoa huduma kamili za uzazi wa dharura ifikapo mwaka 2020.

35.            Mheshimiwa Spika, Huduma za Rufaa kwa Wajawazito zimeendelea kuboreshwa ambapo Wizara imegawa magari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) 67 katika Halmashauri za Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa na Kigoma na mikoa mingine hapa nchini. Aidha, Wizara imegawa magari 8 kwa ajili ya kuratibu shughuli za afya ya mama na mtoto katika Kanda ya Ziwa, Kati, Magharibi, OR - TAMISEMI Dodoma, na magari 2 katika kitengo cha Afya ya mama na Mtoto Wizarani. Hatua hiyo itatoa msukumo na kuimarisha juhudi za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi katika mikoa hiyo ambayo takwimu zimeonesha kuwa wana vifo vingi zaidi.


36.            Mheshimiwa Spika, Wizara imechukua hatua kwa ajili ya kuongeza uwajibikaji kwa ngazi zote ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa kutaka kila kifo cha mama na mtoto kinachotokana na matatizo ya uzazi kijadiliwe ndani ya saa 24 katika kituo/hospitali husika kwa lengo la kubaini chimbuko la kifo hicho na kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuboreshwa zaidi kwa huduma zinazotolewa katika kituo husika. Sambamba na hilo Wizara kuanzia mwezi Oktoba 2016 imeanzisha utaratibu wakutaka kila halmashauri na mikoa nchini kutoa taarifa ya vifo vitokanavyo na uzazi kila mwezi.

37.            Mheshimiwa Spika, katika Hotuba yangu tumeeleza hatua tulizochukua ili kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 ikiwemo watoto wa chini ya mwezi mmoja vipungue kutoka 21 hadi 16 katika kila vizazi hai 1,000; vifo vya watoto wa chini ya umri wa mwaka mmoja kutoka 45 hadi 25 katika kila vizazi hai 1,000 na vifo vya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano kutoka 54 hadi 40 katika kila vizazi hai 1,000

Huduma za Lishe
38.            Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kushirikiana na asasi mbalimbali za Serikali na zisizo za kiserikali kuhamasisha masuala ya Lishe sambamba na kuhakikisha virutubishi muhimu kwa ukuaji wa mwili na akili vinaendelea kupatikana kote nchini. Kwa sasa urutubishaji unaoendelea ni ule wa uongezaji wa virutubishi muhimu kwenye unga wa mahindi na usindikaji wa mafuta ya alizeti kwa kuongeza vitamini A. Aidha kupitia mpango wa urutubishaji chakula kwa kutumia virutubishi nyongeza kwenye chakula cha kawaida kwa watoto wenye umri wa miezi 6 hadi 59 katika ngazi ya jamii (Home food Fortification) umefanyika ktk mikoa mbalimbali nchini.

HUDUMA ZA TIBA
Huduma za Damu Salama
39.            Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama imeendelea kutekeleza jukumu la ukusanyaji na usambazaji wa Damu Salama nchini, ambapo katika kipindi cha Julai 2016 hadi Machi, 2017 jumla ya chupa za damu 145,300 zilikusanywa, sawa na asilimia 63 ya lengo la kukusanya chupa 230,000 kwa mwaka. Chupa zote za damu zilizokusanywa ziliweza kupimwa ambapo na asilimia 90 ya chupa za damu zilizokusanywa zilionekana kutokuwa na maambukizi ya aina yoyote na hatimaye kusambazwa hospitalini kwa ajili ya kupewa wagonjwa wahitaji.

Aidha, Wizara kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI imeanzisha utaratibu wa kuwa na vituo vya benki za damu kwenye ngazi ya mikoa ili visaidiane na benki za damu za kanda katika kuboresha upatikanaji wa damu salama hususani kwa akina mama wajawazito. Hadi sasa Benki za damu za Mikoa 7 zimeanzishwa katika mikoa ya Dar es salaam, Lindi, Morogoro, Dodoma, Iringa, Kigoma na Shinyanga. Uanzishwaji wa benki hizo katika mikoa ya Mara na Kagera upo katika hatua za mwisho. Lengo ni kuhakikisha kila Mkoa una Benki ya Damu ikiwa ni jitihada za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Huduma za Maabara za Uchunguzi wa Magonjwa

40.            Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuboresha huduma za maabara za uchunguzi wa magonjwa ya binadamu ikiwemo Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii (kama nilivyoeleza katika aya ya 56 ya Hotuba yangu.

Upatikanaji wa Dawa, Vifaa, Vifaa Tiba na Vitendanishi

41.            Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika kuboresha upatikanaji wa dawa kwa kununua, kutunza na kusambaza dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Katika mwaka 2016/17, Wizara ilitenga Shilingi bilioni 251.5 kwa ajili ya kununua na kusambaza dawa, vifaa, vifaa tiba,na vitendanishi ikilinganishwa na kiasi cha Shilingibilioni 31kilichotengwamwaka 2015/16. Hadi kufikia Machi 2017, jumla ya Shilingi bilioni 112.1 ikilinganishwa na shilingi bilioni 24 zilizotolewa mwaka 2015/16.Hadi kufikia mwezi Machi 2017 mikoa/halmashauri/hospitali zimepokea zaidi ya asilimia 95.

42.            Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia Machi, 2017, asilimia 81 ya dawa muhimu zaidi (essential medicine) zinapatikana katika Bohari ya Dawa. Ongezeko hili la upatikanaji wa dawa kutoka asilimia 36 kipindi cha mwezi Juni 2016 na kufikia asilimia 81 mwezi Machi, 2017 limetokana na uamuzi wa Serikali wa kuongeza bajeti ya dawa na kuhakikisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya dawa,vifaa, vifaa tiba, na vitendanishi. Aidha, Wizara kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imeanza kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo ununuzi wa dawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji kwa lengo la kupunguza gharama za dawa na kuongeza uwezo wa MSD kununua dawa nyingi zaidi.Lengo la Wizara ni kuhakikisha hali ya upatikanaji wa dawa inafikia asilimia 90 ifikapo mwishoni mwa mwaka wa fedha 2016/17.


43.            Mheshimiwa Spika, Wizara pia imetekeleza ahadi ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuhakikisha kila kituo cha kutolea huduma za afya cha umma kinakuwa na vifaa vya kutosha. Katika mwaka 2016/17, Wizara imenunua na kuanza kusambaza kwa kila Halmashauri vitanda vya kawaida 20, vitanda vya kujifungulia 5, magodoro 25 na mashuka 50.Uzinduzi wa zoezi hili umefanyika mwezi Aprili 2017 katika halmashauri ya Kongwa Dodoma. Jumla ya vitanda vya kawaida (Hospital beds) 3,680, vitanda vya kujifungulia (delivery beds) 920, magodoro 4,600 na mashuka 9,200 vimenunuliwa ambapo thamani yake ni Shilingi bilioni 2.9.


Uimarishaji wa Huduma za Matibabu ya kibingwa

44.            Mheshimiwa Spika, moja ya jukumu la kipaumbele kwa Wizara ilikuwa ni kuendelea kuboresha na kuimarisha huduma za kibingwa zitolewazo nchini. Maboresho hayo, yanalenga katika kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa ya Matibabu nje ya nchi ili kupunguza gharama kubwa ambazo serikali inaingia katika kupeleka wagonjwa nje ya nchi. Hadi kufikia Machi 2017, idadi ya Wagonjwa waliopewa rufaa ya Matibabu nje ya nchi ilipungua kwaasilimia 35 kutoka wagonjwa 553 mwaka 2015/16 hadi Wagonjwa 357 mwaka 2016/17.Mafanikio haya ni kutokana na maboresho yaliyofanyika katika Hospitali zilizo chini ya Wizara zinazotoa huduma za Kibingwa ambazo ni Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), MOI na Ocean Road.

Hospitali ya Taifa Muhimbili
45.            Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Taifa Muhimbili imeendelea kuchukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha utoaji wahuduma za kibingwa. Hatua hizo ni pamoja na kufanya ukarabati wa Wodi 5 za wagonjwa mahututi (ICU).Ukarabati huo utaongeza vitanda vya ICU kutoka 21 na kufikia 75. Aidha, Hospitali imeanza kukarabati jengo kuu la upasuaji wa kina mama wajawazito na jengo la upasuaji wa watoto; ukarabati huo utaongeza vyumba vya upasuaji 6 na na kufikia jumla ya vyumba 19. Upanuzi wa jengo la kusafisha figo unafanyika ambao utaongeza vitanda 27 na kufikia jumla ya vitanda 42.

Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI)

46.            Mheshimiwa Spika, Taasisi ya MOI imeendelea na juhudi za kupanua wigo wa huduma huduma ya upasuaji wa mifupa ikiwemoe migongo ya watoto iliyopinda.

47.            Mheshimiwa Spika, Taasisi ya MOI kwa kushirikiana na GSM Foundation imetoa huduma ya upasuaji wa vichwa vikubwa na mgongo wazi kwa watotokupitia kambi Tiba katika mikoa 18 ya Tanzania Bara na hospitali ya Mnazi Mmoja - Zanzibar. Katika kipindi cha Julai 2016 hadi Machi 2017, jumla ya watoto 2,200 walifanyiwa uchunguzi na watoto 250 walifanyiwa upasuaji kwa mafanikio na kutoa mafunzo kwa Madaktari wa upasuaji katika hospitali za rufaa za mikoa/kanda nchini.

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete(JKCI)
48.            Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha Julai 2016 hadi 2017, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKC) imeendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo ikiwemo kufanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa 236, idadi hii ni sawa na wastani wa wagonjwa 30 kwa mwezi ukilinganisha na wastani wa wagonjwa 15 kwa mwezi  katika mwaka wa fedha 2015/16. Aidha jumla ya wagonjwa 608 walipatiwa matibabu maalum kupitia tundu dogo kwa kutumia mtambo wa kisasa - catheterization laboratory (stents, percutaneous intervention, device closure, pacemarker). Idadi hii ni ongezeko la asilimia 190 ukilinganisha na wagonjwa 290 waliohudumiwa katika mwaka wa fedha 2015/16. Vile vile iliendesha kambi 3 za upasuaji kwa kushirikiana na mataifa rafiki (Israel, Germany na Australia). Hatua hiyo imesaidia kujenga uwezowa madaktari wazawa kwa kupata utaalam wa kupasua wagonjwa kutumia tundu dogo.

Taasisi ya Saratani OceanRoad
49.            Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Saratani Ocean Road  imehudumia wagonjwa wa Saratani nawagonjwa wasio wa saratani kama nilivyoeleza kwenye aya ya 75 hadi 79 ya Hotuba yangu. Masuala makubwa ni pamoja na kukamilika kwa ukarabati wa jengo la kutolea tiba ya dawa (chemotherapy) pamoja na kununua vifaa na vitanda ambapo idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa imeongezeka kutoka wastani wa wagonjwa 40 hadi kufikia wagonjwa 100 kwa wakati mmoja.

50.            Aidha, Taasisi imeweza kupunguza muda wa kusubiri kuanza tiba za mionzi (radiotherapy) kutoka miezi 3 hadi wiki 6; kwa kuhakikisha wagonjwa wanapata tiba mara mbili kwa wiki na kufanya matengenezo ya mashine kwa haraka. Lengo la Wizarani kupunguza muda huo uwe chini yawiki 2 pindi mashine mpya za LINAC zitakaposimikwa.

51.            Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa dawa za saratani umeboreshwa kutoka asilimia 4 mwaka 2015/16 hadi kufikia asilimia 60 mwezi Machi, 2017; na kwa baadhi ya saratani kama ya mlango wa kizazi, saratani ya koo na tezi dume dawa za dripu (chemotherapy) zinapatikana kwa asilimia 100.

52.            Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Saratani OceanRoad ilikamilisha ujenzi wa jengo la ‘bunker’ ambapo mashine za mionzi za LINAC pamoja na CT Simulator zitasimikwa.

Hospitali Maalumu ya Kibong’oto
53.            Mheshimiwa Spika, Hospitali iliendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wa kifua kikuu na UKIMWI, Kifua Kikuu Sugu na Kifua Kikuu cha kawaida (aya ya hotuba yangu). Aidha hospitali imepata mashine ya kupima usugu wa vimelea vya Kifua Kikuu kwa dawa daraja la pili na kupunguza muda wa uchunguzi wa Kifua Kikuu Sugu Zaidi (Extensive drug Resistant TB) chini ya siku 90. Pia hospitali imeweza kufupisha muda wa kuanza Tiba kutoka siku 14 mpaka siku 3 tangu mgonjwa kugundulika kuwa na kifua Kikuu Sugu hivyo kupunguza maambukizi kwa jamii.

Hospitali ya Mirembe

54.            Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Mirembe ilihudumia wagonjwa wa akili na magonjwa ya kawaida wakiwemo wagonjwa wa akili wahalifu.

Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya)

55.            Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Kanda- Mbeya imeendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje na wagonjwa waliolazwa. Aidha, Hospitali imeendelea kuimarisha huduma za kibingwa, ambapo hadi kufikia Machi 2017, jumla ya wagonjwa 37 walifanyiwa upasuaji kwa kutumia tundu dogo.

56.            Mheshimiwa Spika, Hospitali pia imeendelea kuboresha na kupanua wigo wa huduma zinazotolewa kwa kukarabati jengo la daraja la kwanza na kukamilisha ujenzi wa jengo la watoto. Kukamilika kwa miradi hiyo miwili kutaongeza uwezo kwa hospitali kutoka vitanda 477 vya sasa mpaka vitanda 605.

57.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17, Hospitali imeanzisha Idara ya matibabu ya pua, koo na masikio (ENT) na hivyo kuwaondolea wananchi wa Kanda hiyo usumbufu wa kusafiri kufuata huduma hizo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Hadi kufikia mwezi Machi 2017 wagonjwa 883 wenye matatizo hayo wamehudumiwa. Aidha, Idara ya Mifupa imeimarishwa baada ya kupata vifaa vya sign nailssets hivyo kupunguza muda wa wagonjwa walio vunjika kukaa wodini ambapo kwa sasa mgonjwa hukaa wodini kwa muda wa chini ya siku tatu ikilinganishwa na siku 42 ilivyokuwa hapo awali. Vilevile, Huduma ya kusafisha figo (dialysis) imeimarishwa kwa kununua vitanda vipya 3 na hivyo kufikisha idadi ya vitanda 6.



Hospitali ya Rufaa Benjamin Mkapa - DODOMA

58.            Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa Benjamin Mkapaimefunga mitambo ya Uchunguzi wa magonjwa mbalimbali kama vile MRI, CT-Scan, Mammography, General Purpose X-ray, Fluoroscopy, Ultrasound na Dental Unit and Dental X-ray machine. Huduma zitaanza kutolewa baada ya Tume ya Taifa ya Mionzi kutoa leseni. Aidha, hospitali ipo katika hatua za mwisho za ukamilishwaji wa maabara ya kisasa (Cath-lab) kwa ajili ya matibabu ya moyo pamoja na Maabara yenye uwezo wa kuchunguza vinasaba.

Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa - Bugando

59.            Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Bugando imeendelea kutoa huduma mbalimbali zakibingwa zikiwemo huduma za kifua na moyo ambapo jumla ya wagonjwa 1,347 walihudumiwa na 26 walifanyiwa upasuaji mkubwa. Aidha, huduma za moyo kwa watoto zimeanza kutolewa kuanzia mwezi Januari 2017 na hadi sasa watoto 250 wamepata huduma hizo. Hospitali imetoa huduma kwa akinamama 174 wenye fistula. Vilevile, Hospitali imeendelea na ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma ikiwa ni pamojana kliniki za wagonjwa wa nje, jengo la Saratani, na kukamilisha ujenzi wa kliniki ya wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

60.            Mheshimiwa Spika, Hospitali imekamilisha ufungaji wa CT-Scan simulator ambayo hutumika kupanga matibabu ya mionzi ya saratani. Huduma zitaanza kutolewa baada ya Tume ya Mionzi ya Taifa (TAEC) kutoa leseni. Kukamilika kwa mradi huo na kuanza kutolewa kwa matibabu itakuwa ni faraja kubwa kwa wagonjwa wa saratani wa Kanda ya Ziwa.  Hospitali pia imeanzisha kituo cha kusafisha damu (Haemodialyis Unit) ambacho kinaweza kutoa huduma kwa wagonjwa 10 kwa wakati mmoja.



Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini - KCMC

61.            Mheshimiwa Spika, Hospitali ya KCMC kwa kushirikiana na Taasisi za Foundation for Cancer Care in Tanzania (FCCT) na Tanzania Cancer Care Foundation (TCCF) ambao ni marafiki wa Shirika la Msamaria Mwema Tanzania imekamilisha ujenzi wa kituo cha tiba za saratani awamu ya kwanza kati ya nne. Awamu hiyo ilijumuisha ujenzi wa jengo la kliniki kwa ajili ya wagonjwa wa saratani na jengo la tiba ya dawa (Chemotherapy) hivyo kusogeza matibabu ya saratani karibu na wananchiwa mikoa ya Tanga, Manyara, Singida, Arusha, na Kilimanjaro. Wagonjwa waliohudumiwa na kituo hicho ni 415. Aidha Hospitali imekamilisha ujenzi wa Wodi mpya kwa ajili ya wagonjwa walioungua moto na kemikali. Wodi hizo zina uwezo wa kulaza wagonjwa 24 kwa wakati mmoja.Vilevile, Kitengo cha ICU kwa ajili ya watoto kimefunguliwa tangu Oktoba 2016 ambapo hadi kufikia mwezi Machi 2017, jumla ya watoto 91 wamepata huduma.Hospitali pia imeanza kutoa huduma za kusafisha figo tangu Desemba 2016 baada ya kufunga mashine nne za kusafisha figo. Kati ya Januari na Machi 2017, jumla ya wagonjwa 32 wameshapata huduma hii.

Takwimu za mwaka 2016/17 zinaonyesha kuwa magonjwa yanayoongoza kwa rufaa nje ya nchi ni Saratani (36%), Moyo (17%), Masikio, pua na koo (15%), mishipa ya fahamu (8%), mifupa (4%) na mengineyo (5%).

UHAKIKI UBORA WA HUDUMA ZA AFYA
Uhakiki na Ukaguzi 
62.            Mheshimiwa Spika, Wizara imekamilisha zoezi la kufanya tathmini ya awali ya Vituo vya Kutolea Huduma za Afya ya msingi katika  vituo 1,665 vya Halmashauri zote za mikoa 6 iliyokuwa imesalia (Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Kilimanjaro na Arusha). Matokeo ya tathmini yameonesha kuwa asilimia 27 ya vituo hivyo, vilipata nyota sifuri, asilimia 52 vilipata nyota moja, asilimia 16.3 vilipata nyota mbili, asilimia 4.12 vilipata nyota tatu na nyota nne.

63.            Mipango ya Uimarishaji Ubora wa huduma za afya kwa kila Kituo iliandaliwa na utekelezaji unaendelea kwa kushirikiana na Timu za Uendeshaji Afya za Halmashauri.

64.            Mheshimiwa Spika, Wizara pia ilifanya tathmini ya marudio kwa vituo 52 katika mkoa wa Shinyanga. Matokeo ya tathmini ya hiyo, yameonesha kuwepo kwa mabadiliko makubwa katika utekelezaji wa mipango ya uboreshaji wa huduma, ambapo kati ya vituo 40 vilivyokuwa na nyota sifuri, ni vituo 3 tu (7.5%) ndivyo vimebaki katika hadhi ya nyota sifuri.

RASILIMALIWATU KATIKA SEKTA YA AFYA
65.            Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuimarisha miundombinu kwenye vyuo vya mafunzo ya afya kwa lengo la kuongeza udahili na upatikanaji wa rasilimali watu. Udahili huo umeendelea kuimarika kutoka wanafunzi 13,002 mwaka 2015/16 hadi wanafunzi 13,632 mwaka 2016/17. Aidha, Serikali imeendelea na jitihada za kuajiri watumishi wa afya ambapo katika mwaka 2016/17, kibali cha kuajiri madaktari 258 kimepatikana. Madaktari hawa tayari wameshapangwa katika Hospitali/Mikoa na Halmashauri mbalimbali nchini. Hatua hii itasaidia kupunguza pengo la watumishi hasa katika ngazi ya vituo, Hospitali za wilaya na mikoa.


UGHARAMIAJI WA HUDUMA ZA AFYA NCHINI

66.            Mheshimiwa Spika, Wizara ilikamilisha maandalizi ya Mkakati wa Ugharamiaji huduma za afya nchini. Lengo kuu la Mkakati huu ni kutafuta vyanzo mbalimbali vya uhakika vya kuongeza rasilimali fedha katika Sekta ya afya. Moja ya eneo la kugharamia huduma za afya ni kupitia wananchi kujiunga na Mifuko ya Bima ya afya. Kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) imefanikiwa kuongeza idadi ya wanachama wa bima kutoka wanachama702,598 mwaka 2015/16 na kufikia wanachama 792,987 mwezi Machi 2017.



67.            Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Bima ya Taifa ya Afya na kwa kushirikiana na Benki ya Ujerumani (KfW) inatekeleza Mpango wa NHIF/CHF kwa Wanawake Wajawazito na Watoto ujulikanao kama Tumainila Mama ambapo katika kipindi cha Julai 2016 hadi kufikia mwezi Machi 2017, wanawake wajawazito 147,615 walijisajiliwa na hivyo kufanya jumla ya wanufaika kufikia wanawake 572,576 katika mikoa ya Mbeya, Tanga, Lindi, Mtwara na Songwe.

68.                        Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI pamoja na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya inaendelea na  utekelezaji wa mpango wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF). Hadi kufikia Machi 2017 Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ulikuwa na jumla ya kaya 1,595,651 zilizojiunga ukilinganisha na kaya 1,452,855 zilizokuwa zimejiunga mwaka 2015/16. Wizara imetoa malipo ya tele kwa tele kwenye Halmashauri kulingana na kiwango cha makusanyo ya CHF. Katika kipindi cha Julai 2016 hadi Machi 2017 Shilingi bilioni 3.5 zilitolewa na kulipwa kwa Halmashauri mbalimbali nchini.

Uratibu wa Mfuko wa Pamoja wa Afya (Health Basket Fund)

69.            Mheshimiwa Spika, Wizara imekuwa na jukumu la kuratibu  Mfuko wa Pamoja wa Afya (Health Basket Fund) unachangiwa na Wadau (7) ambao ni Denmark, Uswisi (SDC), Ireland, Canada, Benki ya Dunia, UNICEF na Korea Kusini. Aidha, Wizara imeendelea na  juhudi za kuwaleta pamoja wadau wengine zaidi ili wachangie  katika Mfuko huo ili kuleta ufanisi na matokea makubwa katika utekelezaji wa miradi ya afya nchini.

70.            Mheshimiwa Spika, Hadi robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2016/17, kiasi cha Shilingi bilioni 88.8 kimepokelewa kupitia Mfuko wa Pamoja wa Afya. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 5.6 zilipokelewa na Wizara ya Afya (Fungu 52), Shilingi milioni 865.1 zilipokelewa na  OR-TAMISEMI, Shilingi bilioni 2.6 zilipokelewa na  Mikoa na kiasi cha Shilingi bilioni 79.7 zilipokelewa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Fedha hizi hutumika kadiri ya Mkataba wa Makubaliano kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo, ambapo asilimia 33 ya fedha zinazopelekwa katika Halmashauri zinatakiwa kutumika kama nyongeza ya fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa na asilimia 67 ni kwa ajili ya utekelezaji wa afua mbalimbali ambazo zinalenga kuboresha huduma za afya nchini.


UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (FUNGU 53)

MAENDELEO YA JAMII
71.            Mheshimiwa Spika, Sera ya Maendeleo ya Jamii ya 1996 inasisitiza ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka kuleta mabadiliko chanya katika jamii. Katika kutekeleza maelekezo hayo, Wizara katika kipindi cha 2016/17 iliendelea kuwezesha na kuratibu utekelezaji wa majukumu ya Maendeleo ya Jamii hususan katika kutoa hamasa kwa jamii kushiriki katika shughuli za maendeleo kupitia miongozo mbalimbali. Kazi zilizofanyika ni pamoja nakuandaa Mwongozo wa Ufuatiliaji na Tathmini ya shughuli za Maendeleo na Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kuhakikisha shughuli za maendeleo na ustawi wa jamii zinatekelezwa kwa ufanisi na kuwanufaisha wananchi ipasavyo katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na hivyo kuharakisha kufikiwa kwa malengo mbalimbali ya maendeleo.

72.            Mheshimiwa Spika, Wizara ina jukumu la kuandaa wataalam wa kada ya Maendeleo ya Jamii katika ngazi mbalimbali za elimu kupitia Vyuo 8 vya Mafunzo ya Taaluma ya Maendeleo ya Jamii naTaasisi ya Maendeleo Tengeru. Katika mwaka 2016/17, Wizara imeendelea kuzalisha wataalamu wa Maendeleo ya Jamii ambapo jumla ya wataalam 1,685 walihitimu na wanachuo 2,216 walidahiliwa katika ngazi za Astashahada, Stashahada, Shahada na Stashahada ya Uzamili. Wataalamu hawa ni muhimu katika kuwandaa wananchi kushiriki katika kupanga na kutekeleza programu za maendeleo hususan Kilimo, Elimu, Maji, Barabara, Afya, Mifugo na Hifadhi ya Mazingira.

MAENDELEO YA JINSIA
73.            Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutekeleza afua mbalimbali kwa lengo la kufikia usawa wa jinsia na kuwawezesha wanawake nchini. Utekelezaji huo ulizingatia mambo yafuatayo:

Uwezeshaji Wanawake kiuchumi
74.            Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea na jitihada za kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwapatia mikopo kupitia Benki ya Wanawake Tanzania na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ili waweze kushiriki na kunufaika na ukuaji wa pato la kaya na taifa sawa na wanaume.

75.            Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu Mfuko huu kwa lengo la kuwawezesha wanawake wajasiriamali wadogo. Katika mwaka 2016/17, jumla ya Shilingi milioni 156 zilikopeshwa kwa Halmashauri 5 za Kisarawe, Busokelo, Gairo, Iringa Manispaa, Masasi na Mtwara vijijini kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi 61 vyenye wanawake wajasiriamali 658.

76.            Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake unawafikia wanawake wengi, Wizara kwa kushirikiana na OR TAMISEMI imeendelea kuzihamasisha Halmashauri kuchangia asilimia tano (5%) ya mapato yao ya ndani katika Mfuko huo. Katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2016, jumla ya Halmashauri 147 zilichangia jumla ya Shilingi 7,826,722,946. Pamoja na kuongezeka kwa mwamko wa Halmashauri kuchangia katika Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Halmashauri 39 hazikuchangia. Napenda kutumia fursa hii kuzipongeza Halmashauri zote ambazo zimechangia katika Mfuko huu.  Aidha, natoa rai kwenu wabunge wenzangu kuhakikisha Halmashauri zetu zinachangia ipasavyo Mfuko huu.

77.            Mheshimiwa Spika, Benki ya Wanawake Tanzania, imetoa mikopo kwa wajasiriamali 6,956 yenye thamani ya Shilingi bilioni 10.4. Aidha, idadi ya wajasiriamali walionufaika na mikopo imeongezeka kutoka wajasiriamali 79,983 mwaka 2015/16 hadi kufikia wajasiriamali 86,939 mwaka 2016/17 ambapo asilimia 75 ya wanufaika ni wanawake.Vile vile Benki iliwezesha jumla ya wanawake 223 kumiliki ardhi katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na Benki imeongeza vituo vya kutolea mikopo na mafunzo kutoka vituo 184 mwaka 2015/16 hadi kufikia vituo 252 mwaka 2016/17.

78.            Mheshimiwa Spika, vile vile, Wizara kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI iliratibu uanzishwaji na uzinduzi wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi katika mikoa ya Kigoma na Singida. Uanzishwaji wa majukwaa haya unalenga kuendeleza jitahada za Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye alizindua Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Tanzania kwa ngazi ya taifa.

MAENDELEO YA MTOTO
79.            Mheshimiwa Spika, Maendeleo endelevu ya Taifa lolote, yanategemea uwekezaji katika makuzi, malezi, na maendeleo ya mtoto. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, idadi ya watoto ni asilimia 51.6 ya watanzania wote. Hali hii inaonesha umuhimu wa kulinda na kusimamia utekelezaji wa haki za msingi za mtoto ambazo ni; kuishi, kuendelezwa, kulindwa, kushiriki na kutobaguliwa.

Mimba na ndoa za utotoni
80.            Mheshimiwa Spika, mimba na ndoa za utotoni bado ni kikwazo katika kufikia maendeleo endelevu ya nchi yetu. Kwa mujibu wa Utafiti wa Taasisi ya Takwimu ya Taifa kiwango cha ndoa za utotoni nchini ni asilimia 37. Mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni ni Shinyanga (59%) Tabora (58%), Mara (34%), Dodoma (51%) na Lindi (48%).  Aidha Takwimu hizo pia zinaonesha kuwa asilimia 27 ya watoto wanaathirika na mimba za utotoni nchini, mikoa inayoongoza ni Katavi (36.8%), Tabora (36.5%), Simiyu (32.1%), Geita (31.6%) na Shinyanga (31.2%). Katika kukabiliana na ndoa na mimba za utotoni, Wizara kwa mwaka 2016/17 ilishirikiana na wadau kufanya utafiti katika mikoa 10 na halmashauri 20 na kubaini kuwa vyanzo vikubwa vya ndoa na mimba za utotoni ni umaskini na mila potofu. Utafiti huu umesaidia Serikali na wadau wengine kuendesha kampeni na programu za kupinga ndoa za utotoni ili kupunguza tatizo hili. Wizara kwa kushirikiana na wadau iliendesha Kampeni maalum ya kupinga ndoa za utotoni mkoani Shinyanga ambayo iliwafikia wananchi zaidi ya 800 na kuokoa Watoto wa kike 102 waliokuwa katika hatua za kuozeshwa.

Maendeleo ya Mtoto wa Kike
81.            Mheshimiwa Spika, Katika kuhakikisha kuwa mtoto wa kike anapata fursa ya kujiendeleza, Wizara imeendelea kuhamasisha uanzishwaji wa klabu za wasichana shuleni ambazo zinawapa fursa ya kujitambua, kujua haki zao na kutoa taarifa ya ukiukwaji wa haki zao. Jumla ya klabu 105 za watoto wa kike na kiume shuleni katika wilaya ya Tarime, Shinyanga vijini na Kahama zimeanzishwa.

HUDUMA ZA USTAWI WA JAMII
82.            Mheshimiwa Spika, huduma za ustawi wa jamii zinalenga kuyawezesha makundi maalum kupata huduma za msingi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo. Makundi haya ni pamoja na watoto walio katika mazingira hatarishi, watoto walio katika mkinzano na sheria, watu wenye ulemavu na wazee ikiwemo familia zenye migogoro kama nilivyoeleza kuanzia aya ya 148 hadi 157 ya Hotuba yangu.



HAKI NA USTAWI WA WAZEE
83.            Mheshimiwa Spika, wazee ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya taifa kutokana na uzoefu na ujuzi walionao katika nyanja mbalimbali. Kwa mwaka 2016/17,Wizara kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki na ustawi wa wazee kupitia vyombo vya habari na maadhimisho ya siku ya wazee. Elimu hii imesaidia kuongezeka kwa idadi ya wazee wanaopata huduma za afya na kupungua kwa vitendo vya ukatili. Kwa mujibu wa Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi mauaji ya wazee yamepungua kutoka 190 mwaka 2015 hadi 135 mwaka 2016.

84.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17, Wizara imeendelea kutoa huduma kwa wazee 456 wasiojiweza katika makazi 17 yanayoendeshwa na Serikali. Huduma hizi nipamoja na chakula, malazi na matibabu.


85.            Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuwashukuru wadau mbalimbali waliochangia katika kuhakikisha huduma bora kwa wazee nchini. Kipekee napenda kumshukuru Mke wa Rais, Mhe, Mama Janet Magufuli kwa kuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia wazee wanaotunzwa katika makazi ya wazee hapa nchini. Natoa wito kwa jamii kuiga mfano wa mama yetu huyu. Sote ni wazee watarajiwa tunahitaji kuwaenzi, kuwaheshimu na kuwatunza wazee wetu.

WATALAAM WA USTAWI WA JAMII
Mheshimiwa Spika, Kupitia Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Wizara imeendelea kuzalisha wataalam wa ustawi wa jamii kupitia mafunzo katika ngazi ya astashahada, stashahada, shahada, stashahada ya uzamili na Shahada ya uzamili ambapo katika mwaka 2016/17, jumla ya Wataalam 1,164 walihitimu.




UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2016/17 KWA TAASISI NYINGINEZILIZO CHINI YA WIZARA
TAASISI YA CHAKULA NA LISHE
86.            Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Chakula na Lishe imeendelea imeendelea na jitihada za kupambana na utapiamlo kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na wanawake walioko kwenye umri wa kuzaa. Aidha, Utafiti wa Maendeleo ya Afya Nchini wa mwaka 2016 umebaini kuwa tatizo la udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano limepungua kutoka asilimia 42 hadi 34, uzito pungufu umepungua kutoka asilimia 16 hadi 14.

BOHARI YA DAWA (MSD)

87.               Mheshimiwa Spika, Bohari ya Dawa inatekeleza majukumu yake ya msingi ya ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa Dawa, Vifaa, Vifaa Tiba, Vitendanishi na chanjo ili kuwezesha upatikanaji endelevu katika vituo vya kutolea huduma za afya zaidi ya vituo 5,414 nchini, kama ilivyoelezwa katika aya ya 166 hadi aya 168 ya hotuba yangu.

MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA (NHIF)

88.            Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umeendelea kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuongeza wigo wa wanufaika wa bima ya afya. Kazi zilizotekelezwa ni kama nilivyoeleza aya ya 169 na 170 ya hotuba yangu.


MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA (TFDA)

89.            Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Chakula na Dawa imeendelea na kazi ya udhibiti wa ubora na usalama wa chakula, dawa, vipodozi na vifaatiba.


WAKALA WA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

(GCLA)


90.            Mheshimiwa Spika, Wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali imeendelea kutoa huduma za kufanya uchunguzi wa sampuli mbalimbali zikiwemo za Vinasaba, sumu, Dawa za Kulevya, Vyakula, Dawa asilia, Kemikali, Maji, Vilainishi vya Mitambo na sampuli za mazingira. Mtambo wa kisasa wa Liquid Chromatography Mass Spectrometer umenunuliwa kwa kiasi cha Shilingi bilioni 1.6. Mtambo huo utatumika kufanya sampuli mbalimbali za sumu, kilimo, uvuvi, mifugo, maji, dawa za binadamu, gesi, mafuta. Aidha mtambo huu utatumika kuchunguza dawa za kulevya na kutoa mchango katika juhudi za Serikali kupambana na matumizi ya dawa za kulevya.


TAASISI YA UCHUNGUZI WA MAGONJWA YA BINADAMU (NIMRI)
91.            Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa ya Binadamu imeendelea kutekeleza majukumu ikiwa ni pamoja na kuratibu na kufanya tafiti mbalimbali zainazohusu maonjwa ya binadamu hapa nchini.




III: VIPAUMBELE VYA WIZARA NABAJETI YA MAPATO, MATUMIZI YA KAWAIDA NA MIRADI YA MAENDELEO KWA MWAKA WA FEDHA 2017/18

Fungu 52 (AFYA)
92.                     Mheshimiwa Spika Katika mwaka wa fedha 2017/18, Wizara kupitia fungu 52 itatekeleza vipaumbele vifuatavyo:-

                             i.    Kuimarisha Huduma za Kinga, Tiba, na kuongeza usawa katika kutoa huduma za afya;
                            ii.    Kuimarisha huduma za afya ya uzazi na mtotoili kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto;
                           iii.    Kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya umma vya kutolea huduma za afya;
                          iv.    Kuimarisha miundombinu kwenye vyuo vya mafunzo ya afya kwa lengo la kuongeza udahili na upatikanaji wa rasilimali watu;
                           v.    Kuimarisha matibabu ya kibingwa nchini kwa kuendeleza ujenzi, upanuzi, ukarabati wa miundombinu na kufunga mitambo ya kisasa ya kutolea huduma za afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Benjamin Mkapa - Dodoma, Taasisi ya Saratani Ocean Road, Hospitali Maalum za Mirembe na Kibong’oto; pia Hospitali za Rufaa za Kanda za Bugando, KCMC, Mbeya na Mtwara;
                          vi.    Kuimarisha huduma za lishe na upatikanaji wake katika jamii na vituo vya kutolea Huduma za Afya;
                         vii.    Uimarishaji wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuboresha huduma za afya;
                       viii.    Kuhamasisha wananchi kwa nia ya kuongeza idadi ya wanaojiunga na Mifuko ya Bima za Afya.

Fungu 53 (Maendeleo ya Jamii)
93.                     Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Fungu 53, Wizara imepanga kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia maeneo ya kipaumbele yafuatayo;

                     i.        Kuamsha ari ya wananchi kushiriki katika shughuli za kujiletea maendeleo;
                    ii.        Kuwezesha utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/18 – 2021/22;
                   iii.        Kuimarisha upatikanaji wa haki na maendeleo ya Mtoto;
                  iv.        Kukuza usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi;
                   v.        Kuimarisha huduma za ustawi wa Mtoto na Wazee;
                  vi.        Kuimarisha ushiriki wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika maendeleo ya jamii kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi; na
                 vii.        Kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Vyuo vya Maendeleo ya Jamii pamoja na Taasisi ya Ustawi wa Jamii

94.            Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo yaliyoainishwa katika vipaumbele vya mwaka 2017/18,kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na;

HUDUMA ZA KINGA
95.               Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha 2017/18, Wizara itaendelea kutekeleza afua mbalimbali za huduma za kinga.




Huduma za Chanjo

                             i.        Kuendelea kununua na kusambaza chanjo za watoto na wajawazito ili kuwakinga na magonjwa ambapo jumla ya Shilingi bilioni 33 kutoka vyanzo vya ndani zimetengwa.

          Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto

                             i.        Kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kununua na kusambaza dawa na vifaa vya uzazi wa mpango nchini ambapo Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 14;

                            ii.        Kuendelea kununua, kusambaza na kutoa bila malipo dawa kwa ajili ya uzazi salama katika vituo vya umma vya kutolea huduma ikiwemo oxytocin (dawa ya kuzuia kutokwa na damu baada ya kujifungua), magnesium sulphate (kwa ajili ya kifafa cha mimba), Fefol (kwa ajili ya kuongeza damu) ambapo jumla ya Shilingi bilioni 7 zimetengwa;

                           iii.        Kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za uzazi za dharura ikiwemo upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni kwa kuboresha vituo vya afya 150 ambapo jumla ya Shilingi bilioni 1.8 kutoka vyanzo vya ndani zimetengwa;

                          iv.        Kuendeleakuboresha upatikanaji wa damu salama kwa kuongeza vituo 5 vya benki za damu katika mikoa ya Katavi, Rukwa, Ruvuma, Njombe na Manyara, ambapo jumla ya Shilingi bilioni 2 zimetengwa;


HUDUMA ZA TIBA
Dawa, Vifaa, Vifaa Tiba na Vitendanishi.
96.               Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha 2017/18, Wizara itaendelea kuimarisha upatikanaji waDawa, Vifaa, Vifaa Tiba na Vitendanishi nchini kwa kununua na kusambaza katika vituo vya kutolea huduma za afya. Jumla ya Shilingi bilioni 236 zimetengwa. Nitumie fursa hii kuzitaka Halmashauri na Hospitali zote za umma kuanzisha Mfuko wa Dawa (Drug Revolving Fund) kabla ya mwisho wa mwezi June 2017 ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa fedha za dawa.

Huduma za Damu Salama
97.               Mheshimiwa Spika katika mwaka 2017/18, Wizara imetenga jumla ya Shilingi bilioni 3.5 ili kuendelea kukabiliana na tatizo la uhaba wa damu salama kwa kutekeleza yafuatayo:

                     i.        Kukusanya chupa 230,000 za damu salama ili kukidhi mahitaji ya damu salama nchini; na

                    ii.        Kuendesha kampeni ya ukusanyaji wa damu kutoka makundi mbalimbali katika jamii.

Uimarishaji wa Huduma ya kibingwa

98.               Mheshimiwa Spika, Wizara itaendeleakuimarisha upatikanaji na utoaji wa huduma za matibabu kibingwa nchini kupitia Hospitali ya Taifa Muhimbili, MOI, JKCI, Ocean Road na Hospitali zetu za Rufaa za Kanda (Mbeya, Bugando na KCMC) kama nilivyoonyesha kuanzia aya ya 191 hadi 201 ya Hotuba yangu.

99.               Kupitia Hospitali ya Taifa Muhimbiliambapo kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na Kuanzisha huduma za kubadilisha figo (Renal Transplant). Hatua hii inatarajiwa kupunguza gharama za kupandikiza figo nje ya nchi kutoka kiasi cha shilingi milioni 80 hadi shilingimilioni 20 kwa mgonjwa mmoja.

Aidha Hospitali ya Taifa Muhimbili itaanza kutoa huduma za upandikizaji wa vifaa vya kusaidia kusikia (Cochlear implants). (Gharama Kwa mgonjwa 1 nchini India Ni takribani shilingi milioni 80, huduma hii ikitolewa nchini itagharimu takribani shilingi milioni 30.

Pia Hospitali ya Taifa Muhimbili itajenga jengo Maalum kwa Wagonjwa wanaolipia (Private Wing) ambapo jumla ya shilingi bilioni 14.5 zimetengwa.

100.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Taasisi ya Saratani OceanRoad itaendelea kuimarisha huduma za kinga, uchunguzi, mafunzo na tiba ya saratani. Kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na Kununua vifaa vya kisasa vya uchunguzi na matibabu ikiwa ni pamoja na PET Scan ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 14.5 zimetengwa. Hatua hii inatarajiwa kupunguza rufaa za wagonjwa nje ya nchi kwazaidi ya asilimia 60 na hivyo kuokoa pesa za Serikali kiasi cha Shilingibilioni 5kwa mwaka zinazotumika kulipia matibabu ya wagonjwa ya saratani nje ya nchi. (Gharama Kwa mgonjwa 1 India Ni takribani shilingi milioni 100, huduma hii ikitolewa nchini itagharimu takribani shilingi milioni 12.

101.    Mheshimiwa Spika, Hospitali zetu za MOI, JKCI, Mirembe, Kibongoto, Benjamin Mkapa, Mbeya, Bugando, KCMC  zitaendelea kutoa huduma.Aidha tutaendelea na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini Mtwara ambapo kiasi cha shilingi bilioni 2 kimetengwa. JKCI tumeweza kupunguza gharama za upasuaji wa moyo kutoka milioni 20 hadi milioni 8.

102.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Wizara pia inakusudia kuboresha utoaji wa huduma za uuguzi na ukunga unaozingatia maadili, utu na heshima ya mteja (respective care).

103.          Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika mwaka 2017/18, kazi zitakazotekelezwa na fungu 53 ni pamoja na;

MAENDELEO YA JAMII
                     i.        Kuendelea kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini wa shughuli za maendeleo na ustawi wa jamii katika ngazi za Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mtaa;

                    ii.        Kuendelea kuwajengea uwezo Wataalam wa Maendeleo ya Jamii wa kusimamia sera na miongozo ya Wizara ili waweze kuishirikisha jamii katika kujiletea maendeleo;

MAENDELEO YA JINSIA

Kuwawezesha wanawake kiuchumi

                     i.        Kupitia Benki ya Wanawake Tanzania kutoa Mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 12 kwa wajasiriamali wanawake 9,650 katika mikoa ya Dares Salaam, Mbeya, Njombe, Iringa, Dodoma, Ruvuma, Pwani na Mwanza;

                    ii.        Kuhamasisha uanzishwaji wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi katika mikoa yote ya Tanzania Bara kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI;

                   iii.        Kuendelea kuhakikisha Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake unawafikia wanawake wengi.Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI katika mwaka 2017/18, itaendelea kuhamasisha Halmashauri kuchangia asilimia tano (5%) ya mapato yaoya ndani katika Mfuko;

MAENDELEO YA MTOTO
Ukatili dhidi ya watoto
104.          Mheshimiwa Spika, kupitia Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto, Wizara pamoja na mambo mengine itatekeleza yafuatayo:
                     i.        Kuimarisha utendaji wa kamati za ulinzi wa mtoto katika Mamlaka za Serikali ya Mitaa kuanzia ngazi ya Vijiji, Kata na Halmashauri za Wilaya;

                    ii.        Kuendelea kutoa mafunzo kuhusu malezi chanya na athari za ukatili dhidi ya watoto katika Halmashauri 12 za Mikoa ya Lindi na Mtwara;



HUDUMA ZA USTAWI WA JAMII
105.          Mheshimiwa Spika Wizara imeendelea kuweka mifumo ya matunzo,malezi na ulinzi wa watoto yenye misingi ya kijamii.Kwa mwaka 2017/18, pamoja na mambo mengine itafanya yafuatayo:
                     i.        Kuendelea kuzijengea uwezo Halmashauri na wadau wengine kuweka mifumo imara ya matunzo na ulinzi kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi;

                    ii.        Kuhamasisha na kuelimisha waajiri kuzingatia marekebisho ya Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini hususan kifungu cha 33(10) na kuzifanyia marekebisho kupitia Kanuni zake mpya kwa kutoa fursa kwa waajiriwa wanawake kupata haki ya kunyonyesha watoto wao;

                   iii.        Kuendelea kuwajengea uwezo watoa huduma kwa watoto wanaokinzana na sheria ili kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wakati;

HAKI NA USTAWI WA WAZEE

106.          Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuboresha huduma za ustawi wa jamii, makazi ya wazee na kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wazee kote nchini na kutokomeza mauaji ya wazee.

IV: SHUKRANI
107.          Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii ya kipekee kuzishukuru nchi za Denmark (DANIDA), Uswisi (SDC), na Ireland (Irish Aid), Canada (DFATD) na Mashirika ya Kimataifa yakiwemo Benki ya Dunia, UNICEF, na UNFPA kwa kutoa misaada katika Mfuko wa Pamoja wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za afya nchini. Aidha, naishukuru na kuipongeza Korea Kusini kupitia shirika lake la Maendeleo (KOICA) kwa kuamua kujiunga na nchi zinazochangia fedha katika Mfuko wa pamoja kwa ajili ya huduma za afya kuanzia mwaka 2016/17. Pia, napenda kuzishukuru nchi za Canada, China, Cuba, Hispania, India, Italia, Japan, Marekani, Misri, Sweden, Uingereza, Ujerumani na Ufaransa na ambazo zimeendelea kuisaidia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa njia mbalimbali.


108.          Mheshimiwa Spika, vilevile nayashukuru mashirika mengine ya Kimataifa kwa ushirikiano wao waliotoa kwa Wizara. Mashirika haya yanajumuisha Mfuko wa Dunia Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (GFATM), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Benki ya Nchi za Kiarabu kwa ajili ya Maendeleo ya Uchumi ya Nchi za Afrika (BADEA), Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU), Global Aliance on Vaccine (GAVI), Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kudhibiti UKIMWI (UNAIDS), Shirika la Umoja wa Kimataifa la Maendeleo (UNDP), UNFPA, UN-Women, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Benki ya Dunia (WB). Wengine ni Abbott Fund, BASIC NEED (UK), ACF – Canada, Baylor College of Medicine ya Marekani, Canadian Bar Association, CDC, CORDAID (Netherlands), CUAMM, DANIDA, DFID, Engender Health (USA), EED, Elizabeth Glaser Paediatric Aids Foundation (EGPAF), Family Health International (FHI360), FINIDA, GIZ, Good Samaritan Foundation (GSF), German TB and Leprosy Relief Association (GLRA), HelpAge International, ILO, Jane Adams School of Social Work ya Chuo Kikuu cha Illinois Marekani, John Snow Incorporation (JSI), JICA, KOICA, KfW,Global Partnership for Education (GPE), Madaktari Afrika na Madaktari Wasio na Mipaka (Medicins Sans Frontieres – MSF), MSERIOR, ORIO, P4H, SAREC, SDC, SIDA (Sweden), Shirika la Upasuaji la Spain, SIGN la Marekani, na Shirika la Human Resource Capacity Project, Touch Foundation, USAID na, Children Investment Foundation Fund (CIFF), World Lung Foundation.




109.          Mheshimiwa Spika, ninawashukuru pia Wadau wa Maendeleo ambao ni African Programme for Orchorcerciasis Control, Africare, Axios International, Aids Relief Consortium, AIHA, ASCP, ASM, APHL, Balm and Gillead Foundation, Bill and Melinda Gates Foundation, Clinton Health Access Initiative, CLSI, CMB, Christoffel Blinden Mission (CBM), Christian Relief Services (CRS), Citi Bank, Department of Defence ya Marekani, Community of Saint Egidio (DREAM), Duke University, ECSA, Futures Group, Glaxo Smith Kline (GSK), General Electric (GE – USA), Havard University na University of Maryland, Helen Keller International, Henry Jackson Foundation, IMA, ICAP, International Trachoma Initiative, Intrahealth, International Eye Foundation, I-TECH, Jhpiego, Johns Hopkins University, Labiofarm Industry, London School of Hygiene and Tropical Medicine, Management Science for Health (MSH), MEDA, Merck & Company, Malaria No More, Military Advancement for Medical Research, NOVARTIS, Pathfinder, PATH, President’s Emergency Plan for AIDS Relief (PEPFAR), Pharm Access International, PactWorld, Plan International, Pfizer, Qiagen, Research Triangle Institute (RTI), Regional Psychosocial Support Initiatives (REPSSI), Saint Thomas Hospital- London, Save the Children, SightSavers International, Supply Chain Management Systems (SCMS) na University of Columbia, URC, USA-Presidential Malaria Initiative (PMI), World Vision, FXB, Walter REED Army Institute of Research (WRAIR) na World Education Inc.

110.          Mheshimiwa Spika, ninawashukuru watu binafsi, vyama vya hiari na mashirika yasiyo ya kiserikali ya ndani ya nchi kwa kuwa mstari wa mbele katika kuchangia uimarishaji wa huduma za afya. Mashirika hayo ni pamoja na AGOTA, Aga Khan Foundation, APHFTA, AMREF, AGPAHI, APT, BAKWATA, Benjamin William Mkapa HIV/AIDS Foundation, CCBRT, CSSC, CCT, Counsenuth, ELCT, Ifakara Health Institute, Lions Club, MAT, AFRICARE, Msalaba Mwekundu, MEHATA, MEWATA, MUKIKUTE, FAWETA, TAMWA, TAWLA, TGNP, MDH, MeLSAT, PASADA, PAT, PSI, PRINMAT, Rotary Club International, SIKIKA, Shree Hindu Mandal, TANNA, TPHA, TPRI, Tanzania Surgical Assosciation (TSA), Tanzania Society of Anaethesiologist of Tanzania (SATA), Association of Gynaecologists and Obstetricians of Tanzania (AGOTA), Association of Paedricians of Tanzania (PAT),Tanzania Diabetic Association, TANESA, THPS, TUNAJALI, Tanzania Midwife Association, TDA, TAYOA, TISS, TEC, UMATI, USADEFU, White Ribbon Alliance, Mabaraza yote ya Kitaaluma, Mashirika, hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya na ustawi wa jamii nchini pamoja na vyama vyote vya kitaaluma vya sekta ya afya.

111.            Mheshimiwa Spika, navishukuru Vyuo Vikuu vya Dar es Salaam, Muhimbili, Sokoine, Ardhi, Mzumbe, Dodoma, Chuo Kikuu Huria, Kumbukumbu ya Hurbert Kairuki, IMTU, Tumaini, St. Agustino, CUHAS, Sebastian Kolowa, St. John, Aga Khan, Morogoro Muslim, Taasisi ya Teknolojia ya Nelson Mandela, Arusha pamoja na Vyuo vyote vilivyo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kuwa mstari wa mbele katika kuchangia uimarishaji wa huduma za afya na maendeleo ya jamii. Aidha, nawashukuru wadau wengine waliotoa huduma ya elimu kwa njia za redio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii katika masuala ya afya na maendeleo ya jamii.

112.                     Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki cha utendaji wangu wa kazi nikiwa Waziri, nimepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi na wafanyakazi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla (Mb.), Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ushirikiano anaonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, naomba kuwashukuru Dkt. Mpoki M. Ulisubisya Katibu Mkuu (Afya) na Bibi Sihaba Nkinga Katibu Mkuu (Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) kwa mchango wao katika kuwezesha utekelezaji wa majukumu yangu. Vilevile, nawashukuruProf. Muhammad Bakari Kambi, Mganga Mkuu wa Serikali, Makamishna, Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo vya Wizara. Nawashukuru pia, Wakurugenzi wa Hospitali zetu ambazo ni Hospitali ya Taifa Muhimbili, MOI, JKCI, Ocean Road, Mirembe, Kibongo’to na Hospitali za Rufaa za Kanda  ya Mbeya, Benjamini Mkapoa Dodoma, Bugando, na KCMC  na Taasisi zilizo chini ya Wizara. Nawashukuru Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Waganga Wafawidhi wa Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati, Wakuu wa Vyuo vya Mafunzo vilivyo chini ya Wizara na Mashirika ya Dini, ya Kujitolea na Binafsi. Nawashukuru wafanyakazi wote wa Wizara. Natoa shukrani kwa sekta zote ambazo tunashirikiana nazo katika kutoa huduma za afya, maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii pamoja na watumishi wote wa afya na wananchi kwa ushirikiano wao. Kwa watumishi wa afya na ustawi wa jamii nchini, nawaasa waendelee kuzingatia misingi ya huduma bora na kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya taifa letu.

113.                     Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii pia kuishukuru familia yangu, kwa uvumilivu wao na pia kwa kunitia moyo katika kutekeleza majukumu yangu ya Kitaifa. Kwa wananchi na hasa wanawake wa Mkoa wa Tanga nawashukuru kwa ushirikiano wanaoendelea kunipatia katika kuendeleza Mkoa wetu. Naahidi kuwa nitaendelea kuwaenzi na kuwatumikia kwa nguvu zangu zote ili kuleta mabadiliko ya haraka ya kimaendeleo katika Mkoa  wetu.



V: MAOMBI YA FEDHA KWA KAZI ZILIZOPANGWAKUTEKELEZWA KATIKA MWAKA WA FEDHA 2017/18
Fungu 52 - Afya
Mapato
114.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Wizara imekadiria kukusanya mapato ya Shilingi 225,038,495,525.00. Kati ya fedha hizo Shilingi 207,472,729,612.00 zitakusanywa katika mashirika nataasisi zilizo chini ya Wizara na Shilingi 17,565,765,913.00 ni kutoka makao makuu.

Matumizi ya Kawaida
115.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Wizara inakadiria kutumia kiasi cha Shilingi 291,895,940,000.00 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida. Kati ya fedha hizo, Shilingi 64,063,937,000.00 zitatumika kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi227,832,003,000.00 zitatumika kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi. Kati ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya Mishahara Shilingi49,036,786,000.00 ni kwa ajili ya watumishi wa Wizara, Makao Makuu na Shilingi 178,795,217,000.00 ni kwa ajili ya watumishi wa Taasisi, Mashirika na Wakala zilizo chini ya Wizara.

Miradi ya Maendeleo
116.          Mheshimiwa Spika, kwa upande wa shughuli za maendeleo, Wizara inakadiria kutumia Shilingi 785,805,952,000.00 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Kati ya hizo, fedha za ndani ni Shilingi 336,300,000,000.00 na fedha za nje ni Shilingi 449,505,952,278.00.

Jumla ya Makadirio ya Bajeti kwa 2017/18 kwa Fungu 52 niShilingi 1,077,701,892,000.00



Fungu 53 – Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
117.          Mheshimiwa Spika, Makadirio ya Makusanyo ya Maduhuli na Matumizi kwa Mwaka 2017/18 kwa Fungu – 53 ni kama ifuatavyo:
Makusanyo ya Maduhuli

Wizara inataraji kukusanya Maduhuli yenye jumla ya Shilingi 2,101,874,000.00 ambazo ni ada za wanafunzi kutoka Vyuo 8 vya Maendeleo ya Jamii, ada za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na mauzo ya vitabu vya zabuni.
Matumizi ya Kawaida na Miradi ya Maendeleo
Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa mwaka 2017/18, niShilingi 35,300,602,090.00 ambapo Mishahara ni Shilingi 19,142,252,240.00 na Shilingi 16,158,349,850.00 ni Matumizi Mengineyo.Aidha, Miradi ya Maendeleo inakadiriwa kutumia kiasi cha Shilingi 2,606,278,000. Kati ya fedha hizo, Shilingi 2,000,000,000.00ni fedha za ndani na Shilingi 606,278,000 ni fedha za nje.

Jumla ya Makadirio ya Bajeti kwa 2017/18 kwa Fungu 53 niShilingi 37,906,880,090

118.        Mheshimiwa Spika, Jumla kuu ya fedha zote zinazoombwa kwa Wizara ni Shilingi 1,115,608,772,090.00

119.          Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

0 comments: