DURU MPYA YA MAZUNGUMZO YA SYRIA NA TAATHIRA YA HATUA ZA KIJESHI ZA MAREKANI

Duru ya nne ya mazungumzo ya mjini Astana, Kazakhstan ilianza Jumatano ya jana. Duru hiyo ya mazungumzo ya Syria imefanyika huku yakishuhudiwa mabadiliko madogo kwa upande wa washiriki.
Jumbe za makundi ya wapinzani wa Syria zinazoshiriki mazungumzo hayo, takribani ni zile zile zilizoshiriki mazungumzo yaliyopita. Ujumbe unaoiwakilisha serikali ya Damascus, unaongozwa na Bashar Jaafari, mwakilishi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa, huku timu ya Umoja wa Mataifa ikiwakilishwa na Staffan de Mistura, mjumbe wa Katibu Mkuu wa umoja huo nchini Syria. Katika muundo wa jumbe za Iran, Russia na Uturuki ambazo ni watazamaji wa mazungumzo hayo, nazo hazijashuhudia mabadiliko yoyote. Mabadiliko muhimu yaliyoshuhudiwa yalikuwa ya mwakilishi wa Marekani 'Stuart Jones' Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo katika masuala ya Mashariki ya Kati, ambaye amechukua nafasi ya balozi wa nchi hiyo huko Kazakhstan katika kikao hicho.
Pande tatu za Iran, Russia na Uturuki zinazosimamia mazungumzo hayo
Duru hiyo ya mazungumzo ikilinganishwa na duru ya tatu ya mazungumzo ya Astana nayo pia ingali inakabiliwa na vikwazo vingi. Matatizo muhimu katika mazungumzo ya Astana Nne yanatokana na hatua za kijeshi za mashambulizi ya Marekani ya tarehe saba Aprili dhidi ya kambi ya jeshi la anga ya Syria katika mji wa Shayrat, mkoani Homs na kadhalika mashambulizi tofauti ya Israel katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo. Hatua hizo za kijeshi ndizo zimepelekea hata kukosekana matumaini kuhusiana na mazungumzo ya Syria. Hii ni katika hali ambayo katika duru ya mwisho ya mazungumzo ya mjini Astana na Geneva ambazo zilifanyika mwezi Machi mwaka huu, kulikuwepo na matarajio mengi kuhusiana na njia za utatuzi wa kisiasa kuhusiana na mgogoro wa Syria, kiasi kwamba kwa mara ya kwanza katika duru ya mwisho ya mazungumzo ya Geneva, timu za wapinzani na ile ya upande wa serikali ya Damascus, zilifanya mazungumzo ya ana kwa ana baina yao.
Staffan de Mistura, mwakilisi wa UN nchini Syria
Kizuizi kingine katika mazungumzo ya Astana Nne, ni miamala ya kujikariri ya wapinzani wa serikali ya Syria. Hii ni kusema kuwa, katika kikao hicho wapinzani wa serikali kama ilivyokuwa katika kikao cha duru ya tatu, wamefanya ukwamishaji mwingi wa mambo. Hii ni katika hali ambayo kwa mujibu wa baadhi ya habari wapinzani wa Syria jana waliahirisha kushiriki mazungumzo hayo na badala yake wameamua kujiunga na meza ya mazungumzo hayo leo, huku baadhi ya duru zikisema kuwa, awali wapinzani hao walishiriki kwenye meza ya mazungumzo na kuondoka  kwenye mazungumzo hayo baadaye. Inaelezwa kuwa, tangu mapema wapinzani hao walitangaza kuwa wasingeshiriki mazungumzo hadi pale mashambulizi ya anga ya jeshi la serikali dhidi maeneo wanayoyadhibiti huko Syria yatakapositishwa.
Pande za wapinzani katika mazungumzo
Inaonekana kuwa, ukwamishaji huo unasababishwa na kutoweka matumaini yao juu ya kufikiwa malengo ya kuidhoofisha serikali ya Damascus katika mashambulizi ya Marekani ya tarehe saba Aprili dhidi ya kambi ya jeshi la anga ya Syria katika mji wa Shayrat, mkoani Homs na pia hujuma kama hizo za Israel katika maeneo tofauti ya nchi hiyo. Tunaweza kusema kuwa, mazungumzo ya Astana Nne yamefeli hata kabla ya kuanza kwake, kutokana na miamala hasi ya serikali ya sasa ya Marekani katika kipindi cha miezi miwili ya hivi karibuni. Pamoja na hayo lazima tukubali kwamba mazungumzo ndio njia muhimu kwa ajili ya utatuzi wa mgogoro wa Syria.
Mashambulizi yaliyofeli ya Marekani ya April huko Syria
Kama ambavyo kuendelea mazungumzo hayo, kunaweza kupunguza taathira ya mashambulizi ya kijeshi ya Marekani ya mwezi Aprili dhidi ya Syria na kufufua matarajio kwa ajili ya kufikiwa makubaliano kuhusiana na mgogoro wa nchi hiyo ya Kiarabu.

0 comments: