SERA ZA MAREKANI KATIKA MASHARIKI YA KATI NI KUENEZA HOFU NA VITISHO DHIDI YA IRAN
Posted by khamisimussa77@gmail.com at 11:40 AM
James Mattis, Waziri wa Ulinzi wa Marekani
amesema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Riyadh Saudi Arabia
baada ya kukutana na mwenyeji wake kwamba, timu ya Rais Donald Trump
inaandaa mikakati ya kuidhibiti na kuikwamisha Iran kupitia njia ya
kuimarisha uratibu na Saudi Arabia na waitifaki wengine wa Marekani.
Jenerali Mattis amedai kwamba,
Iran imekuwa ikivuruga amani na uthabiti katika Mashariki ya Kati hivyo
kuna haja ya kuzuia satwa na ushawishi wa taifa hili ili ipatikane njia
ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Yemen kupitia mazungumzo kwa upataishi
wa Umoja wa Mataifa. Kwa hakika matamshi haya ya Waziri wa Ulinzi wa
Marekani si jambo jipya. Viongozi wa Marekani bila kujali ni wa chama
cha Democrats au cha Repulican wamekuwa wakitumia lugha hizo za vitisho
tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipopata ushindi na Mfumo wa
Jamhuri ya Kiislamu ulipokuja na kukata mikono ya Marekani hapa nchini.
Kwa muktadha huo, uadui wa madola
yanayotumia mabavu ulimwenguni hususan Marekani kwa taifa taifa la Iran
ni jambo lisilo na shaka hata kidogo. Hii inatokana na kuwa, uadui wao
uliendelea kushuhudiwa katika kipindi chote ambacho serikali mbalimbali
na zenye utashi tofauti zilipoingia madarakani nchini Marekani.
Pamoja na hayo, inaonekana kuwa, lengo la viongozi wa Marekani katika
kipindi hiki la kutumia lugha hizi za vitisho ni kutoa ishara ya kuweko
mabadiliko ya kimsingi katika sera za Marekani katika kukabiliana na
Iran. Hivi sasa siasa za Marekani dhidi ya Iran kwa namna fulani
zinaonekana kuipa Saudi Arabia baadhi ya majukumu. Kiasi kwamba, akitoa
natija jumla ya mazungumzo yake huko Riyadh, Waziri wa Ulinzi wa
Marekani amesema kuwa, Washington imefikia natija na Riyadh kuhusiana na
jambo hilo. Mattis amesema: Kwa hakika sisi tunapaswa kufanya kitu
na kuimarisha muqawama wa Saudia mbele ya miamala ya Iran. Kama ambavyo
tunafanya kazi tukiwa washirika, tunapaswa kuchukua hatua ambazo
zitakufanyeni nyinyi viongozi wa Saudia na jeshi lenu muwe na utendaji
mzuri zaidi.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani ameyatoa
matamshi na madai haya mjini Riyadh katika hali ambayo, kila mahala
ambako kuna matatizo katika Mashariki ya Kati na popote pale ambako
kunafukuta moto wa vita kuanzia Asia mpaka Ulaya na Afrika mpaka Amerika
ya Latini basi kunashuhudiwa mkono wa Marekani na waitifaki wake.
Aidha stratejia ya Marekani katika
Mashariki ya Kati inaeleweka wazi. Stratejia hiyo haina tofauti sana na
duru zilizopita za uongozi nchini Marekani kabla ya Rais wa sasa wa nchi
hiyo Donald Trump. Marekani ingali inawategemea watawala wa nchi za
Kiarabu wa eneo hili katika uuzaji silaha zake kwa kisingizio cha
kukabilia na vitisho ambavyo Marekani yenyewe imevipandikiza. Utawala wa
Aal Saud nao ukitumia mbinu ya kale umekuwa ukinunua silaha nyingi kwa
kutumia fedha za mafuta ikiwa na lengo la kununua muda zaidi kwa utawala
wake unaotetereka na kulegalega.
Katika uwanja huo, himaya ya Marekani
kwa uvamizi wa Saudia katika vita vya Yemen ni jambo muhimu, kwani
kivitendo siasa za chokochoko za Saudia katika vita hivyo na vile vile
katika kuyaunga mkono makundi ya kigaidi huko Syria na Iraq zimeshindwa
na kugonga mwamba. Njia pekee iliyobakia kwa Aal Saud ni kutoa upendeleo
kwa Marekani usio na masharti yoyote. Hata hivyo inawezekana kuyatazama
matamshi haya ya Mattis katika engo nyingine. Waziri huyo wa Ulinzi wa
Marekani anasema kuwa, Washington na washirika wake wanataka kuikwamisha
Iran.
Matamshi haya kwa namna fulani yanaweza
kuwa yana lengo la kupima radiamali ya Iran mkabala na lugha za vitisho
za Marekani. Kwani viongozi wa White House wanatambua vyema msimamo wa
Iran kuhusiana na jambo hilo.
Akihutubia Jumatano ya jana kwa mnasaba wa Siku ya Jeshi hapa nchini,
wakati alipokutana na kundi la makamanda wa jeshi, Ayatullah Ali
Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kuwa, moja
ya nukta imara za mfumo wa Kiislamu hapa nchini ni kuwa na moyo wa
kishujaa na kusimama kwake kidete mbele ya makeke na upayukaji wa madola
ya kibeberu. Aidha alisema kuwa, moja ya hila na ujanja unaotumiwa na
madola vamizi ni kuyatisha mataifa na tawala za nchi nyingine na kutumia
woga wa mataifa hayo kufanikisha malengo haramu ya madola hayo ya
kibeberu na ndio maana mara zote utayaona madola hayo ya kiistikbari
yakipenda kujigamba na kujionesha kuwa yana nguvu kubwa.
Kiongozi Muadhamu amesema bayana kwamba,
kama Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran lingeyaogopa madola ya
kibeberu na kulegeza kamba mbele yao, basi leo hii kusingekuwa na athari
yoyote ile ya Iran na Uirani. Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, adui
yeyote yule, awe Mmarekani au mkubwa kuliko Marekani hawezi kufanya
lolote mbele ya mfumo wa utawala unaotegemea vizuri nguvu za wananchi
wake na ambao umesimama kidete mbele ya adui.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: