NAIBU MWINGINE WA ABU BAKR AL-BAGHDADI, MKUU WA DAESH AUAWA KWA KOMBARA MOSUL

Jeshi la Iraq limetangaza habari ya kumuangamiza naibu mkuu wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika operesheni iliyofanyika magharibi mwa mji wa Mosul hii leo.
Luteni Jenerali Raed Shaker Jawdat, Kamanda wa Kikosi cha Polisi ya Federali ya Iraq amesema, kiongozi nambari mbili wa Daesh anayefahamika kama Abu Abdulrahman, naibu wa Ibrahim al-Samarrai maarufu kwa jina la Abu Bakar al-Baghdadi ameuawa leo Jumatano baada ya jeshi la Iraq kuvurumisha makombora katika ngome ya magaidi hao katika eneo la Zanjili, magharibi mwa mji wa Mosul.
Kanali ya telivisheni ya Shafaaq inayorusha matangazo yake kwa lugha ya Kiarabu imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, Abu Maria al-Roumi, kamanda mwingine wa genge hilo la kigaidi raia wa Russia ameuawa katika operesheni nyingine tofauti katika eneo la Ras al-Jadah, huku kamanda mwingine wa ngazi za juu wa Daesh kwa jina Abu Walid al-Tunisi akiuawa katika wilaya ya al-Farouq.
Abu Bakr al-Baghdadi, kiongozi wa Daesh (ISIS)
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Masuala ya Kikabila wa Daesh, anayefahamika kama Abu Abdullah al-Shabaki, ameuawa katika shambulizi la anga la Marekani katika mji wa Zanjili. 
Mapema mwezi huu, ndege za jeshi la Iraq zilishambulia ngome ya kijeshi ya kundi hilo la Daesh eneo la magharibi mwa al-Anbar na kusababisha kuuawa kiongozi mwingine nambari mbili baada ya Baghdadi kwa jina la Ayad Hamid Khalaf Al-Jumaili, maarufu kwa jina la Abu Yahya. Al-Jumaili alitambuliwa kwa cheo cha Waziri wa Vita wa kundi hilo la ukufurishaji la Daesh.
Jeshi la Iraq likishirikiana na vikosi vya kujitolea vya Hashd al-Sha’abi, limepata mafanikio mengi na kuangamiza makamanda waandamizi wa Daesh, tangu lilipoanzisha operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul Februari 19.  

0 comments: