IRAN YALAANI HUJUMA YA KIGAIDI DHIDI YA MABASI HUKO ALEPPO, SYRIA

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali mashambulizi ya mabomu dhidi ya mabasi yaliyokuwa yanawahamisha watu kutoka vijiji ambavyo aghalabu ya wakazi wake ni Waislamu wa madhehebu ya Shia huko katika mkoa wa Idlib, kaskazini magharibi mwa Syria.
Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameyataja mashambulizi hayo kama kitendo cha jinai, woga, fedheha na kisicho na utu dhidi ya watoto wadogo na wanawake wasio na ulinzi.
Sambamba na kutoa salamu za rambirambi kwa wahanga wa jinai hizo, serikali na taifa la Syria kwa ujumla, Qassemi amesema anashangazwa na madola yanayoyaunga mkono magenge ya kigaidi nchini Syria namna yanavyojifanya kuomboleza na kuhuzunishwa na ukatili huo wa jana akisisitiza kuwa huo ni unafiki  wa wazi.
Bahram Qassemi
Taarifa iliyotolewa na shirika rasmi la habari la Syria SANA imesema watu 40 waliuawa kwenye mashambulio hayo ya jana Jumamosi. Hata hivyo baadhi ya duru za habari zinasema waliokufa ni zaidi ya 43. Mabasi kadhaa yaliwaka moto huku mengine yakiharibiwa vibaya kutokana na athari za mlipuko huo uliotokea katika kituo cha upekuzi. 
Mabasi hayo yalikuwa yanawahamisha wakazi wa vijiji vya Kefraya na al-Foua vilivyoko katika wilaya ya al-Rashideen, viungano mwa mji wa Aleppo, yapata kilomita 355 kaskazini mwa mji mkuu Damascus.

0 comments: