ASKARI POLISI BARABARA YA MANYOVU MWANDIGA WALALAMIKIWA KWA KUKITHIRI KWA RUSHWA MKOANI KIGOMA

Na Magreth Magosso,Kigoma
 
BAADHI ya Askari Polisi Mkoa wa Kigoma wamelalamikiwa kulazimisha rushwa kwa vyombo vya usafiri na wananchi nyakati za masoko ya wakulima hali, inayowapa usumbufu katika shughuli zao za uzalishaji mali kwa kuwa wanakabiliwa na kodi mbalimbali zilizoanishwa na Serikali husika.
 
Akitoa hoja hiyo jana mbele ya wajumbe wa kikao cha baraza la madiwani wa Wilaya ya Kigoma vijijini, Diwani wa Kata ya Mkongoro Morani Mgina alieleza kuwa, kero hiyo imeshamiri katika barabara ya Mwandiga hadi Manyovu ambapo, kuna masoko makubwa ya wakulima wa bidhaa mbalimbali za mashambani.
 
“wananchi hawana amani, kama hoja ni kudhibiti wahamiaji haramu kwa nini iwe siku ya soko tu,wanakamata magari aina ya michomoko ambayo inabeba mizigo na kulazimisha kitu kidogo hata kama gari haina kosa na akibisha wanamchomekea tatizo jamani raia wanachoka kunyanyaswa” alilalamika Diwani Mgina.
 
Naye Diwani wa Kata ya Mkigo Erick Niganya alifafanua kuwa,pamoja na wananchi kulaani tabia ya rushwa kwa askari husika lakini madiwani wa kata zilizopo katika barabara hiyo wameshuhudia matukio kadhaa ya rushwa za nje nje kwa wafanyabishara hasa vyombo vya usafiri hawana amani siku za masoko mtambukwa .
 
Diwani wa kata ya Mngonya Mganza Mtale alianisha kuwa, kuna askari wanatoza ushuru ambao kimsingi ushuru unatozwa na wakala wa maeneo mtambukwa hali inayowapa sintofahamu ya hatma ya ushuru wanaotoza kwenye maeneo yasiyowahusu na kumtaka mwakilishi wa OCD kwenye kikao hicho abainishe mipaka yao ya utendaji kazi.
 
Akiongezea hilo Diwani wa kata ya Kalinzi Swage Swage alisema vielelezo vipo na wathirika wa kuombwa rushwa wapo tayari kuzungumza huku akitolea mfano tukio la dereva wa boda kulazimishwa kulipa kiasi cha sh.30,000 ilihali alimwonyesha askari viambatanisho vyote mtambukwa wa pikipiki hiyo,lakini aliondoka baada ya kutoa kiasi hicho.
 
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo (Nyarubanda)Enock Chobariko alimtaka mwakilishi wa OCD katika kikao hicho asikwepe ukweli wa rushwa kwa baadhi ya askari mkoani humo hasa barabara ya mwandiga hadi mamyovu kwa kuwa wanashuhudia kila mara na wapunguze mageti ya kusachi mizigo ,ambapo kwa njia hiyo kuna geti zaidi ya tano katika barabara moja tu.
 
Baadhi ya madereva wanaosafirisha abiria na mizigo katika barabara hiyo kwa nyakati tofauti majina kwa usalama wa kazi zao walisema kuna mazingira wanalazimika kuwapa kitu kidogo askari hao ili wafanye shughuli zao lakini ni kero kubwa isiyokwisha kwao,hata kama utakuwa na viambatanisho mtambukwa wa chombo chako na ukibisha usishangae kubambiwa janga.
 
Akijibia hilo mwakilishi wa OCD SP Israel Makongo alisema hawafurahii kusikia hilo na kukiri kuna baadhi wana kula rushwa hivyo kuwaomba watoe tarifa kwa wahusika ili sheria ichukue mkondo wake, kwa kuwa hakuna kiongozi ayependa tasisi yake ilalamikiwe kwa ubaya.
 
Alisema hakuna tasisi ya serikali inayotuma watumishi kuomba rushwa na kunyanyasa wananchi na hakuna hata raia mmoja aliyepeleka kero hiyo katika ofisi yao na kusisitiza kuwa kilichopo ni mgongano wa maslai wa utozaji ushuru baina ya wenyeviti wa vijiji,watendaji na baadhi ya madiwani.
 
Alianisha kuwa, kata za kigoma kaskazini zinapakana na vijiji vya nchi ya Burundi ambavyo vipo mipakani ndio sababu ya kuweka geti za ukaguzi na madiwani wasitoe kero ya rushwa kwa ujumla kwa kuwa kuna baadhi ya raia wanatumia siku za masoko hayo kuingia nchini kinyemela na awali kabla ya kuongezwa geti kwa siku raia 60 wa Burundi huingia kigoma kwa madai ya kusalimia ndugu zao.

0 comments: