IRAN YAFANYIA MAJARIBIO MAKOMBORA YA NEZE’AT-10 KWENYE LUTEKA YA 'BAITUL MUqADDAS 28'

Jeshi la Nchi Kavu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limefanyia majaribio makombora mawili yaliyopewa jina la Neze'at-10 katika mazoezi ya kijeshi yanayoendelea katikati mwa nchi.
Luteka hiyo iliyopewa jina la Baitul Muqaddas 28 imeanza leo na inatazamiwa kumalizika kesho Jumatatu viungani mwa mji wa Kashan, mkoani Isfahan. Mazoezi hayo ya kijeshi yanafanyika katika hatua tatu, mkondo wa kwanza na wa pili unafanyika leo katika maeneo ya jangwani, huku hatua ya mwisho ikitazamiwa kufanyika kesho katika eneo la operesheni la Nasrabad, katika mkoa huo huo wa Isfahan.
Kombora la Neze'at-10 au N-10 linaweza kupiga umbali wa kilomita 140. Kombora hilo la balistiki ambalo limeimarishwa na wataalamu wa Jeshi la Nchi Kavu la Iran linaweza kupigwa kwa kutumia simu ya rununu, tofauti na makombora mengine ya balistiki.
Kadhalika makombora ya masafa mafupi ya N-6 na maroketi ya Fajr 5 yatafanyiwa majaribio katika maneva hayo ya Baitul Muqaddas 28.
Akizungumza kabla ya kuanza luteka hiyo, Brigedia Jenerali Ahmad Reza Pourdastan, Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwepo tayari kivita jeshi la nchi hii ni sababu kuu inayowazuia maadui kuitishia Iran. Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Pourdastan, jeshi la nchi kavu la Iran liko tayari kikamilifu kulinda mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu.

0 comments: