WIZARA YA AFYA YAMTAKA MKEMIA MKUU KUFUATILIA MATUMIZI YA SIGARA YA KIKO YA MAJI (SHISHA)

index 
Na Beatrice Lyimo Maelezo Dar Es Salaam.
………………………………….
WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imeiagiza Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kufuatilia matumizi ya sigara ya kiko ya maji (Shisha) katika kumbi za starehe  za hapa nchini kwa kuwa sigara hizo zinahusishwa na  matumizi ya madawa ya kulevya.
Akizungumza katika hafla ya utoaji tuzo kwa wanafunzi na walimu bora wa masomo ya kemia na biolojia kwa mwaka 2013-2014 iliyofanyika leo Ijumaa (Septemba 18, 2015), Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,  Dkt Donan Mmbando alisema hatua hiyo ni mkakati wa serikali wa kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya nchini.
Dkt Mmbando alisema  Wizara kupitia Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali inatoa mchango mkubwa wa uchunguzi wa kimaabara kuweza kutambua dawa za kulevya na pia kuwatambua waathirika wa dawa hizo.
“Serikali inatambua umuhimu na unyeti wa kazi zinazofanywa na wakala wa maabara na mkemia mkuu wa serikali katika kulinda afya na usalama wa watu na mazingira pamoja na kuleta uelewano katika jamii” alisema Dkt Mmbando.
Aidha alisema serikali itaendelea kuitegemea Taasisi hususani katika utaalamu kwa utatuzi wa masuala yanayohusiana na kulinda afya na usalama wa jamii, hivyo itahakikisha inaiwezesha taasisi hiyo katika mahitaji ya rasilimalli watu na fedha.
Aidha Dkt Mmbando aliwapongeza walimu na wanafunzi wote waliofanya vyema katika mitihani yao na kuwakumbusha juu ya madhara ya matumizi ya dawa za kulevya ambayo yanaweza kufuta ndoto ya kuwa nguvu kazi ya taifa.

0 comments: