Mratibu
Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa hapa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez
nae akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani.
Bw. Rodriguez pia alisoma ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
kuhusu maadhimisho hayo
Sehemu ya wageni waalikwa akiwemo Mama Shamim Khan ( wa kwanza kushoto) wakimsiliza Bw. Rodriguez (hayupo pichani)
Aliyekuwa
Kamanda wa Kwanza wa Brigedi Maalum ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na
Vikundi vya Uasi nchini DRC, Meja Jenerali James Mwakibolwa
akiwasilisha mada kuhusu "Wajibu wa Raia katika Kutunza Amani" wakati wa
maadhimisho hayo
Sehemu ya
wageni waalikwa na waandaaji wa maadhimisho hayo akiwemo Bi. Stela Vuzo
(kushoto), Afisa kutoka Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC)
wakimsikiliza Meja Jenerali Mwakibolwa (hayupo pichani)
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi
Liberata Mulamula ametoa wito kwa Watanzania hususan vijana kuwa mstari
wa mbele katika kulinda na kuhakikisha amani iliyopo nchini inadumu.
Balozi
Mulamula ametoa wito huo wakati akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku
ya Kimataifa ya Amani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Alliance Française,
Jijini Dar es Salaam.
Balozi
Mulamuala ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo alisema
kuwa kila Mtanzania anao wajibu wa kuchangia katika amani ya nchi huku
akiwataka vijana ambao ni wengi kuhakikisha wanailinda amani iliyopo kwa
ajili ya kujiletea maendeleo yao na vizazi vijavyo.
Aliongeza
kuwa fursa mbalimbali zikiwemo za uongozi na maisha bora hazipatikani
kwa kutumia nguvu wala vurugu na kuwataka vijana kujikita katika elimu,
kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kutimiza ndoto zao ikiwemo kuwa
viongozi wanaofaa hapo baadaye.
“Nahamasika
kwamba vijana ambao ni asilimia 60 ya wananchi wa Tanzania wanao wajibu
mkubwa katika kulinda amani ya nchi yetu na ninaamini kuwa kijana
anaweza kuwa kiongozi popote pale alipo na katika lolote analolifanya
hivyo nawaomba mjijenge kwenye elimu, bidii katika kazi na kuwa
waadilifu ili muwe viongozi bora baadaye”, alisema Balozi Mulamula.
Akizungumzia
Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2015, Balozi Mulamula
aliwahakikishia wananchi kuwa utakuwa wa amani na utulivu na kwamba
wananchi wote wanao mchango mkubwa wa kuhakikisha amani inakuwepo wakati
wote wa uchaguzi hadi hapo utakapokamilika. Vile vile alitoa rai kwa
wananchi kujitokeza kupiga kura ili kuchagua viongozi wanaowataka badala
ya kuingia mitaani na kusababisha uvunjifu wa amani.
“Tumieni
fursa iliyopo kuchagua viongozi bora. Kura yako ndio amani yako. Hivyo
nawaomba wote wenye sifa mjitokeze kupiga kura wakati ukifika”
alisisitiza Balozi Mulamula.
Awali
akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja
wa Mataifa hapa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez alisema kuwa maadhimisho
hayo ya 33 yanayobeba kauli mbiu isemayo “Ushirikiano kwa ajili ya
Amani; Utu kwa Wote” yamefanyika wakati muafaka huku Tanzania ikijiandaa
na uchaguzi mkuu na kuwataka vijana kuzingatia utawala wa sheria kwani
kupanga ni kuchagua na kwamba amani ndio kitu cha kwanza.
Aidha,
katika ujumbe wake kwenye maadhimisho hayo uliosomwa na Bw. Rodriguez,
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Ban Kimoon ametoa wito kwa nchi
zote duniani zinazokabiliwa na migogoro na uvunjifu wa amani kuweka
silaha chini na kurejea katika meza za mazungumzo. Aidha amezitaka nchi
zote duniani kuwekeza kwa vijana ambao ndio wajenzi wa amani.
Akiwasilisha
mada wakati wa maadhimisho hayo kuhusu “Wajibu wa Raia katika Kutunza
Amani” Kamanda wa Kwanza wa Brigedi Maalum ya Umoja wa Mataifa
iliyoanzishwa kupambana na Waasi huko DRC, Meja Jenerali, James
Mwakibolwa alisema kuwa Tanzania imekuwa kisiwa cha amani kutokana na
juhudi za viongozi katika kuhakikisha amani inadumishwa na vilevile
ushirikiano mkubwa wa wananchi kwa serikali yao.
Aidha,
aliongeza kuwa ili amani iliyopo idumu ni muhimu kuwa na viongozi
thabiti wanaotenda haki na pia elimu ya uraia itolewe kwa wananchi kwani
amani ikitoweka kila mtu ataathirika kwa namna moja au nyingine.
“Nimekuwa
kwenye maeneo ya vita na ukosefu wa amani na nimejifunza kuwa amani
ikitoweka si rahisi kuirejesha. Hivyo nawasihi Watanzania wenzangu
kudumisha amani kwa kutii sheria bila shuruti na kutoa ushirikiano kwa
vyombo vya usalama pale inapohitajika ili nchi iendelee kuwa na amani na
kukuza uchumi kwa maendeleo ya nchi” alisema Meja Jenerali Mwakibolwa.
Siku ya
Kimataifa ya Amani huadhimishwa duniani kote tarehe 21 Septemba kila
mwaka ambapo maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo:
“Ushirikiano kwa ajili ya Amani; Utu kwa Wote”.
0 comments: