ZOEZI LA FTX USHIRIKIANO IMARA 2024 LAFUNGULIWA RASMI NCHINI RWANDA.

 Na. Mwandishi Jeshi la Polisi-Rwanda.


Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, Meja Generali Fadhili Omary Nondo kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CDF) Jacob Nkunda ameshiriki katika hafla ya ufunguzi wa zoezi la ushirikiano Imara FTX, 2024 lililofanyika Juni 13, 2024 katika Chuo cha Jeshi nchini Rwanda ambapo amesema kuwa zoezi hilo limelenga katika kufanya kazi kwa pamoja, kujenga uaminifu, kubadilishana uzoefu pamoja na kujenga ushirikiano wa pamoja katika kupambana na uhalifu unaovuka mipaka.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Juu na Mafunzo ya nje ya nchi wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Samwel Mshana ambaye pia ni Mkuu wa Msafara wa washiriki kutoka Jeshi la Polisi wanaoshiriki katika zoezi hilo, kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Camillus Wambura, amesema kuwa mazoezi haya yana tija kubwa sana katika masuala ya ulinzi na usalama wa nchi kwa sababu yanahusisha kushirikiana kwa majeshi yote kwa kujenga uelewa wa pamoja katika kukabiliana na uhalifu.



Naye mmoja wa washiriki wa zoezi kutoka ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha Maafa, Dkt. Salum Manyatta amesema kuwa, mazoezi haya yana matokeo mazuri katika kuweka utayari wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kukabiliana na ugaidi, uharamia baharini, kukabiliana na majanga pamoja na ulinzi wa amani.


Zoezi hilo la kumi na tatu (13) tangu kuanzishwa kwa mazoezi haya mwaka 2011 limefunguliwa na Waziri wa Ulinzi wa Rwanda Mhe. Juvenal Marizamunda, June 13, 2024 katika Chuo cha Jeshi la Rwanda.


Zoezi hili limelenga katika kuzijengea uwezo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kukabiliana na changamoto za kiusalama na uhalifu unaovuka mipaka pamoja na kudumisha Ushirikiano Imara baina ya vyombo vya ulinzi na usalama katika operesheni za ulinzi wa amani.


0 comments: