WANANCHI KIJIJI CHA NANDA HALMASHAURI YA WILAYA YA NEWALA MKOANI MTWARA WAMSHUKURU DKT. SAMIA

 Na Mwandishi maalum -Newala


WANANCHI wa kijiji cha Nanda Halmashauri ya wilaya ya Newala mkoani Mtwara,wamemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,kwa kutoa fedha ili kukarabati mradi wa maji Makonde ambao ukikamilika utamaliza adha ya muda mrefu ya huduma ya maji safi na salama.

Wametoa pongezi hizo jana kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava,baada ya kukagua ujenzi wa tenki la kuhifadhi zaidi ya lita milioni 3 za maji linalojengwa kupitia mradi wa maji Makonde.

Mwanahamis Juma mkazi wa Nanda alisema,changamoto ya maji katika kijiji hicho na vijiji vingine katika Halmashauri ya wilaya Newala ni tatizo la muda mrefu na kwa sasa wanalazimika kutumia maji ya visima na mabonde kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.

Alisema,mradi huo utakapokamilika utawasaidia kupata huduma ya maji safi na salama kwenye maeneo yao na kuwaondolea usumbufu wa kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi yao.

Issa Athuman,ameipongeza serikali kupitia wizara ya maji,kwa kufanya ukarabati mradi huo uliojengwa tangu miaka ya hamsini bila kufanyiwa ukarabati mkubwa na ndiyo unaotegemea kutoa huduma ya maji kwa wananchi wa wilaya zaidi ya tatu katika mkoa wa Mtwara.

Mbunge wa Jimbo la Newala vijijini Maimuna Mtanda alisema,wananchi wa Jimbo la Newala vijijini kwa muda mrefu wana ukame mkubwa wa maji safi na salama,hivyo kuanza kwa ukarabati wa mradi huo mkubwa kutaleta nafuu kubwa kwao.

“Ndugu Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,katika jimbo letu baadhi ya watu wamefariki Dunia bila kuonja ladha ya maji ya bomba,kwa hiyo upanuzi wa mradi huu utaleta nafuu kubwa na kuwaondolea wananchi changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji”alisema Mtanda.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji Makonde Francis Bwire alieleza kuwa,upanuzi wa mradi huo unalenga kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita 2 hadi 6 kwa siku kwa kutumia chanzo cha Mitema ambapo mahitaji ya wananchi kwa siku ni lita milioni 4.

Alitaja kazi zinazofanyika katika mradi huo ni ulazaji bomba kuu kilometa 40 kutoka kwenye chanzo cha maji cha Mitema-Newala,kujenga tenki la kuhifadhi maji la lita milioni 3 katika kijiji cha Nanda na tenki la lita milioni 6 katika kijiji cha Nambunga,ujenzi wa zege la awali na kazi mbalimbali zilizopo katika mkataba wa ujenzi wa mradi.

Bwire,ameishukuru serikali kwa kuufanya mradi wa maji Makonde kuwa miongoni mwa miradi inayofanyiwa ukarabati mkubwa chini ya miradi ya miji 28 hapa nchini.

Alisema,kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuongeza hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa asilimia 100 na wananchi watapata nafasi kubwa ya kufanya shughuli za uzalishaji mali badala ya kutumia muda mwingi kwenda kutafuta maji.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava, amemuagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji Makonde,kumsimamia kwa karibu Mkandarasi ili aweze kukamilisha kazi kwa wakati na kwa ubora mkubwa.

Alisema,wananchi wa Nanda na vijiji vingine vilivyopo katika Jimbo la Newala wana shida kubwa ya maji safi na salama,kwa hiyo ni lazima Mkandarasi aongeze nguvu ili akamilishe kazi hiyo haraka na wananchi waondokane na changamoto ya huduma ya maji.
Mkazi wa kijiji cha Nanda wilaya ya Newala mkoani Mtwara Mtanda kushoto,akimpa zawadi ya kuku Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava.
Tenki lenye uwezo wa kuhiafdhi lita milioni 3 linalojengwa katika kijiji cha Nanda Halmashauri ya wilaya Newala mkoani Mtwara.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava,akizungumza na Wakazi wa kijiji cha Nanda Halmashauri ya wilaya Newala baada ya kukagua ukarabti wa mradi wa maji Makonde unaotekelezwa na Serikali kwa gharama ya zaidi ya Sh.bilioni 84.7,kulia kwake Mkuu wa wilaya Newala Alhaji Mwangi Rajabu Kundya.

0 comments: