Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.
Rosemary Senyamule amekabidhiwa na Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Godwin
Gondwe madarasa 51, Vyoo 63 na nyumba 1 ya waalimu ikiwa ni sawa na
shule 7 zilizokamilika katika Wilaya ya Bahi.
Akipokea
shule na miundombinu yake Senyamule amepongeza uongozi wa Wilaya ya
Bahi kwa kukamilisha mradi huo tarehe 28 Juni 2023 ikiwa ni siku mbili
kabla ya tarehe iliyopangwa na Mkoa yaani tarehe 30 Juni 2023.
“Bahi
mnajipambanua sana katika suala la elimu, awali tu tulikuwa tunaziambia
Halmashauri zingine zije zijifunze kwenu kuhusu kufaulu, leo tutawatuma
kujifunza kuhusu mnavyojipanga kukamilisha miradi ya ujenzi kwa wakati
na viwango vya hali ya juu” Senyamule amesisitiza.
Amesema
Mkoa wa Dodoma umepokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya 16
zenye miundombinu ya kisasa ikiwa ni pamoja na michezo ya watoto na uzio
kwa ajili ya madarasa ya awali.
Akikabidhi
madarasa hayo Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Godwin Gondwe amesema Wilaya
yake imekamilisha ujenzi huo wa Shule na madarasa kwa muda ulioelekezwa
kwa ubora na viwango elekezi, huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pesa ya
kufanikisha ujenzi huo.
“Mheshimiwa
Mkuu wa Mkoa naomba upokee Shule hii na madarasa ambayo yamekamilika
kwa viwango vya ubora wa hali ya juu kwa niaba ya wana Bahi naomba
utufikishie shukrani zetu kwa Mhe Rais” Amefafanua Mhe. Gondwe
Kwa
upande wake Afisa Elimu Wilaya ya Bahi Mwl. Boniphace Wilson amesema
kukamilika kwa madarasa hayo ni suluhu ya msongamano wa wanafunzi katika
madarasa ya awali ambapo Wilaya hiyo ilipokea fedha kiasi cha Shilingi
Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya mbili zenye jumla ya
vyumba 28, madarasa manne ya awali, majengo mawili ya utawala na
vichomea taka.
Wilaya
ya Bahi imekuwa Wilaya ya kwanza katika Mkoa wa Dodoma kukamilisha
ujenzi wa miundombinu ya mradi wa Boost ikiwa ni pamoja na Ujenzi wa
shule mpya za msingi, vyumba vya madarasa, madarasa ya mfano ya elimu ya
awali, matundu ya vyoo na nyumba za walimu.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizundua Shule ya Msingi Bahi Mission baada ya kukamika. Wilaya ya Bahi ilipokea kiasi cha Shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya mbili zenye jumla ya vyumba 28, madarasa manne ya awali, majengo mawili ya utawala na vichomea taka.
0 comments: