‘MAPRO’ WAPISHANA MITAA YA KARIAKOO

 

Na Mwandishi wetu, Michuzi TV

Hatimaye!!! Dirisha dogo la usajili msimu wa 2022-2023 limefungwa rasmi, usiku wa Januari 15, 2023 majira ya saa 6:01, huku Klabu mbalimbali zikionyesha umwamba katika usajili wa dirisha hilo ambalo lilifunguliwa Desemba 15, 2022.


Usajili wa dirisha dogo unafanyika majira kama haya kati ya Desemba na Januari ili Klabu mbalimbali zifanye maboresho ya vikosi vyao na kujiweka sawa katika mashindano mbalimbali ambayo Klabu hizo zinashiriki katika msimu husika wa mashindano.


Naam! fursa ya usajili katika dirisha hilo imewafurahisha wengi hususani Klabu kongwe za nchini Tanzania yaani Simba na Yanga, ambao wote wamehusika kufanya usajili wa Wachezaji mbalimbali katika vikosi vyao, sanjari na timu nyingine za Klabu kama Azam FC, Singida Big Stars na wengine.


Yanga SC, licha ya kuwa na Kikosi kipana katika msimu uliopita wa mashindano wa 2021-2022 na kupata mafanikio makubwa ya kutwaa mataji yote matatu nchini, mataji ya Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (NBC PL) na Kombe la Shirikisho (ASFC). Haikuwatosha! Wananchi wamehusika kufanya usajili katika dirisha hili dogo ili kuboresha zaidi Kikosi chao.


Msimu huu wa 2022-2023, Yanga SC wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na alama 50 katika michezo yao 19 huku wakishuka dimbani kwanye mzunguko wa 20 dhidi ya Ihefu SC. Wananchi wamefanikiwa kuwanyakua Wachezaji wapya, Mshambuliaji Kennedy Musonda kutoka Power Dynamos FC ya Zambia na Mlinzi wa kati kutoka Stade Maliën ya Mali, Mamadou Doumbia.


Yanga SC wametajwa pia kukamilisha usajili wa Golikipa wa Singida Big Stars, Metacha Boniface Mnata (Buffalo) kwa mkopo wa miezi sita, Metacha ametajwa kurejea tena kwa Wananchi ili kuziba pengo la Golikipa Abuutwalib Mshery ambaye imeelezwa amepata majeruhi akiwa na Kikosi hicho.


Tayari Wananchi wametoa mkono wa kwaheri kwa Wachezaji wa kigeni, Yacouba Sogne na Heritier Makambo ambao wote wamepisha maingizo mapya  katika mitaa ya Twiga na Jangwani kwenye Kambi yao kule Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam.


Simba SC wakiwa nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na alama 44 kwenye michezo 19 sanjari na kufanya mazuri kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL) wameendelea kufanya maboresho katika Kikosi chao baada ya kuingiza baadhi ya maingizo mapya ili kuboresha zaidi Kikosi hicho.


Mnyama ameboresha Benchi la Ufundi kwa kusajili Kocha mpya kutoka Vipers SC ya Uganda, Mbrazil Roberto Oliveira (Robertinho) ambaye amekuja kuongeza nguvu kwenye Kikosi hicho kilichokuwa chini ya Kocha mzawa, Juma Mgunda, ambaye alikuwa anasaidiwa na Suleiman Matola sanjari na Mussa Hassan Mgosi kwa wakati fulani.


Simba SC wamesajili pia Kiungo Mkabaji wa Kimataifa wa Burkina Faso, Hamed Ismael Sawadogo na Mshambuliaji wa Kimataifa wa DR Congo, Jean Beleke ambaye aliwahi kucheza Klabu ya TP Mazembe ya nchini humo. Hata hivyo, Simba SC huenda wakawa tayari wamechana na Wachezaji raia wa Nigeria, Nelson Okwa na Victor Akpan

0 comments: