WAPINZANI WAANDAMANA KUPINGA TUME YA UCHAGUZI KENYA, MMOJA AFARIKI

Wapinzani waandamana kupinga tume ya uchaguzi Kenya, mmoja afariki
Polisi nchini Kenya wamelazimika kutumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa muungano wa upinzani NASA walioandamana katika miji ya Nairobi na Kisumu kushinikiza mabadiliko katika Tume Huru ya Uchaguzi IEBC.
Taarifa zinasema mtu mmoja amefariki dunia kufuatia mshtuko wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya waandamanaji katika Kaunti ya Siaya magharibi mwa Kenya ambayo ni ngome ya kinara wa upinzani Raila Odinga.
Muungano wa upinzani nchini Kenya unasema unaongoza maandamano kushinikiza mabadiliko ndani ya tume hiyo kabla ya kufanyika uchaguzi wa marudio wa urais tarehe 26 mwezi huu wa Oktoba.
Kiongozi wa muungano huo Raila Odinga ametangaza kuwa, hawatakubali kufanyika uchaguzi huo iwapo Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo Ezra Chiloba na maafisa wengine wataendelea kuandaa uchaguzi mpya ambao utakuwa ni mchuano kati ya Odinga na Rais Uhuru Kenyatta.
Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta
Serikali ya Kenya imesema maandamano ya muungano wa upinzani yatadhibitiwa na vitengo vya kuimarisha usalama vya nchi hiyo. Rais Uhuru Kenyatta amesema kuwa ni haki ya wafuasi wa Nasa na viongozi wao kuandamana lakini ameonya kuwa serikali haitawaruhusu  wasababishe fujo na matatizo kwa wengine wasiohusika na maandamano.

0 comments: