Na Jumia Travel Tanzania
Inawezekana utakuwa umesikia watu au
kusoma kwenye mitandao ya kijamii kuhusu sherehe za Halloween lakini
ukawa hauelewi. Mbali na hapo inawezekana pia umekutana na matangazo
kadhaa yakikutana kushiriki kwenye sherehe za sikukuu hiyo sehemu kadhaa
za starehe hususani vilabu vya usiku hapa nchini.
Kutokana na utandawazi uliosababisha
dunia kuwa kijiji tumejikuta kwa namna moja ama nyingine tukishiriki
matukio mbalimbali kwa wakati mmoja. Baadhi ya matukio hayo huwa
hatuelewi maana yake kwa undani zaidi. Kwa mfano, Halloween kwa namna
inavyosherehekewa ni kama ina uhusiano na sherehe za kishetani.
Ikiwa sehemu mbalimbali duniani
zimeshaanza maandalizi ya sherehe za Halloween ambazo hufanyika kila
ifikapo Oktoba 31 ya kila mwaka, Jumia Travel ingependa kukufahamisha
juu ya maana halisi ya sherehe hii.
Japokuwa umaarufu wa sherehe ya
Halloween umetokana na nchi ya Marekani lakini ukweli ni kwamba
wanahistoria wanaamini sherehe hii ilianzia nchini Ireland na kusambaa
nchi za jirani za Scotland, Uingereza, Ufaransa na baadaye sehemu
zingine duniani.
Na kudhihirisha kwamba Marekani
inasherehekea sherehe hii kikamilifu, inaaminika kwamba ni sherehe ya
pili kwa ukubwa wa kibiashara ndani ya mwaka. Katika kipindi hiki
takwimu zinaonyesha kwamba wamarekani hutumia zaidi ya dola bilioni 5
kuadhimisha sherehe hii. Na kwa kuongezea robo ya mauzo yote ya
peremende au pipi ya mwaka hufanyika ndani ya kipindi hiki nchini humo.
Halloween ina maana gani na kwanini husherehekewa kila ifikapo Oktoba 31 ya mwaka?
Maana halisi ya neno Halloween ni siku
ya mkesha wa siku ya watakatifu wote ambayo huadhimishwa kila ifikapo
Novemba mosi. Halloween pia ni ufupisho wa neno ‘Allhalloween, All
Hallows’ Evening na All Saint’s Eve’ ambapo husherehekewa kila ifikapo
Oktoba 31 ya kila mwaka.
Asili ya Halloween ilitokana na sherehe
ya ‘Samhain’ iliyokuwa ikiadhimishwa na watu wa kale wa Ireland au
‘Waseltiki’ kama wanavyojulikana.
Samhain ni sherehe ya wapagani wa
kiseltiki ikimaanisha ‘Mwisho wa Majira ya Joto’ ambayo huadhimishwa
mwisho wa msimu wa mavuno.
Hiki kilikuwa ni kipindi ambacho
walikuwa wakiwasha moto kuuzunguka na kisha kuvalia mavazi yanafanana na
ya mashetani ili kuepekana na mizimu inayosemekana huwa inarandaranda
usiku huo.
Katika karne ya nane, Papa Gregory III
alisema kwamba Novemba mosi itakuwa ni siku ya kuwakumbuka watakatifu na
wafia dini wote. Na hapo ndipo ‘Siku ya Watakatifu Wote’ ilipoanzia na
jioni yake ilikuwa ikijulikana kama ‘All Hallows’ Eve’ na baadaye kuwa
Halloween.
Halloween imepata umaarufu mkubwa kadiri
muda unavyokwenda na kuwa kipindi cha kufanya biashara kwa wingi ambapo
watoto na watu wazima husherehekea kwa kuvalia mavazi ya kuogofya kama
mizimu au mashetani na kwenda kuhudhuria sherehe zinazoandaliwa.
Kwanini watu huvalia mavazi ya kuogofya usiku wa Halloween?
Utamaduni ambao umekuwepo kwa miaka
mingi katika kusherehekea Halloween ni pamoja na kuvalia mavazi ya
kutisha kama mizimu au mashetani.
Washerehekeaji hufanya hivyo kutokana na
asili ya sherehe hii ambapo inaamini kwamba katika mkesha wa siku ya
Oktoba 31 kuamkia Novemba mosi mashetani, wachawi na mizimu huwa
inarandaranda mitaani kusherehekea kuanza kwa msimu wao - kipindi cha
majira ya baridi. Inasemekana kwamba huranda mitaani na kuwachezea watu,
kuwatisha, kuwadhuru na kuwafanyia hila mbalimbali kadiri wanavyopenda.
Njia pekee kwa watu waliokuwa wanaogopa
kutishwa na mizimu hiyo ni kuwapatia vitu ambavyo walikuwa
wanavipendelea, mara nyingi huwa ni vyakula vitamu na zawadi nzuri kama
vile peremende kwa kuviacha milangoni.
Au, njia nyingine iliyokuwa ikitumika,
kwa watu ambao walikuwa wanaogopa, ni kwa kuvalia mavazi kama yao na
kisha kurandaranda mitaani, lengo ni kwa mizimu hiyo kutowatambua na
kuwafananisha binadamu hao na wenzao.
Je unajiuliza kama usherehekee sikukuu
ya Halloween? Kumekuwa na dhana tofauti juu ya sherehe hii ambayo kwa
namna moja ama nyingine zimekuwa zikihusishwa na ushetani na ushirikina.
Hii inategemea namna wewe mwenyewe utakavyosherehekea na kwa malengo
gani na kama itaathiri vipi imani yako. Kwa makala haya, Jumia Travel
inaamini kwamba utakuwa umefahamu machache kuhusiana na sherehe hii
ambayo inazidi kushika kasi kadiri miaka inavyokwenda.
0 comments: