ZIMBABWE NI YA ' PILI ' KATIKA MATAIFA YALIYOENDELEA AFRIKA - MUGABE

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amekanusha kuwa  nchi yake iko katika hali mbaya kiuchumi na kushikilia kuwa ni mojawapo ya  mataifa yalioendelea zaidi barani Afrika.
Robert Mugabe (picture-alliance/AP Photo)
Akizugumza katika  mkutano wa jukwaa la kiuchumi duniani-World Economic Forum kwa Afrika, unaoendelea  mjini Durban nchini Afrika kusini rais Mugabe  amesema mataifa ya magharibi  yamekuwa yakijaribu juu chini kuvuruga uchumi wa Zimbabwe.Katika mkutano huo wa Durban rais Mugabe amesema serikali yake imepiga hatua katika kuimarisha hali ya maisha ya Wazimbabwe na hivi sasa  asilimia 90 wanaweza kusoma na kuandika kinyume na ilivyokuwa awali.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 93  alisema  japo taifa lake linakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha na hivi sasa mifugo  wanatumika kufanya malipo mbalimbali ikiwemo karo ya shule, bado linashikilia nafasi nzuri kiuchumi ukiliganisha na mataifa mengine ya Afrika."Zimbabwe ni miongoni mwa mataifa yaliyoendelea zaidi barani Afrika na baada ya Afrika kusini sidhani kama kuna taifa lingine lilo na maendeleo makubwa kama  Zimbabwe, tuna vyuo vikuu 14. Nakubali  tuna matatizo yetu lakini sisi sio taifa maskini" alisema rais Mugabe.
Simbabwe Obst- und Gemüsemarkt in Jambanja (Getty Images/AFP) Soko la matunda na mboga Zimbabwe
Serikali ya Zimbabwe imekuwa ikishindwa hata  kuwalipa  mishahara wafanyikazi wa serikali na kwa mujibu wa ripoti ya  shirika la umoja wa  mataifa UNDP inashikilia nafasi ya 24 katika maendeleo barani Afrika.Wakosoaji wanasema rais Mugabe  ameharibu uchumi wa nchi ambayo ilitegemewa  zaidi kuongoza kiuchumi barani Afrika  na pia  kusababisha ukosefu wa ajira ambao kwasasa umefikia asimilia 80 ,kufuatia  sera  zake  kama kuchukua kwa nguvu mashamba ya kibiashara  yaliyokuwa yakimilikiwa na wazungu na pia uchapishaji fedha.
Licha ya maandamano ya mara kwa mara  kupinga uongozi wake,rais Mugabe aliuambia mkutano huo wa Durban kuwa bado anaungwa mkono wa raia wengi" Uchumi haiwezi kukua kwa haraka  kama watu wetu wanavyotarajia.Tunahitaji kuwekeza zaidi na uwekezaji huo unapaswa kuwa umeanzishwa zamani,lakini bado wengi wetu wamo katika kiwango cha chini."Nae waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schaeuble ambae ni miongoni mwa wajumbe wanaohudhuria mkutano huo ameitaka jumuiya ya kimataifa  kuimarisha ushirikiano  wake na bara la Afrika ,akiongeza kuwa  ushirikano mpya na nchi 20 zinazoongoza kiuchumi duniani yaani  G20 utafungua nafasi  nyingi za uwekezaji Afrika.
 Wolfgang Schauble World Economic Forum Afrika 2017 Durban (Reuters/R.Ward) Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schaeuble
Matamshi ya waziri huyo yamekuja  siku mbili baada ya mwenzake wa mambo ya nje Sigmar Gabriel  kuyataka mataifa ya Ulaya kuunganisha sera zao kuhusu Afrika, kutokana na kutozungumza kwa sauti moja.Mkutano huo unaokamilika hapo kesho unahudhuriwa na marais mbalimbali   akiwemo mwenyeji Jacob Zuma,Yoweri Museveni wa Uganda miongoni mwa wengine.

0 comments: