TGNP YAENDESHA SEMINA KUJADILI VIPAUMBELE KATIKA BAJETI YA WIZARA YA AFYA YA MWAKA 2017/2018

 Ofisa Programu wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Alphonce Slima, akiongoza semina ya kujadili vipaumbele katika bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 iliyofanyika makao makuu ya TGNP Mabibo jijini Dar es Salaam jana.
 Mdau  Neofita Kunambi akizungumza wakati akichangia mada kwenye semina hiyo.
 Anna Sangai akichangia jambo kwenye semina hiyo.
 Sadick Juma mkazi wa Mbezi Beach, akielezea changamoto ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Muhimbili.
 Janeth Mawinza akielezea changamoto ya matibabu ya homa ya ini ambayo dawa zake hazipatikani nchini hadi zitoke India.
 Moses Benard akizungumzia wajawazito kujinunulia vifaa vya kujifungulia na suala la dawati la ukatili wa kijinsia kuwepo vituo vya polisi.
 Mdau Dalia Kalungwana akichangia jambo.
 Washiriki wakiwa kwenye semina hiyo.
 Semina ikiendelea.
 wananchi wakifuatilia kwa karibu semina hiyo.
Vijana wakifuatilia mada katika semina hiyo.

Na Dotto Mwaibale

WANANCHI wameiptia bajeti ya mwaka 2017/ 2018 ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto iliyotengwa na kuomba iongezwe kwa kuzingatia ukubwa wa wizara hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika semina ya siku moja iliyoandaliwa na Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) ya majadiliano ya kupitia bajeti hiyo ili kuona vipau mbele vyake waliombwa iongezwe ili iweze kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye wizara hiyo ambayo imelemewa kutokana na ukubwa wake.

Kwa mwaka wa fedha wa 2016/ 2017 wizara hiyo ilitengewa bajeti ya sh.bilioni 845 ikilinganishwa na mwaka wa fedha wa 2017/2018 ambayo tofauti yake sio kubwa.

Akizungumza katika semina hiyo, Neofita Kunambi alisema katika wizara hiyo kunachangamoto kubwa bila ya kuongezewa fedha katika bajeti yake hazitaweza kuisha.

"Bila ya kuongeza bajeti katika wizara hii wajawazito wataendelea kujinunulia vifaa vya kujifungulia tunaomba jambo liangaliwe kwa karibu" alisema Kunambi.

Anna Sangai alisema huduma za afya zinapaswa kuboreshwa kuanzia upatikanaji wa dawa na vifaa tiba na bila kuongezwa kwa bajeti katika wizara hiyo itakuwa ni ndoto.

Mkazi wa Mbezi Beach, Sadick Juma alisema upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, miundombinu na ukatili wa kijinsia ni changamoto kubwa katika wizara hiyo.

Alisema licha ya kuwepo duka la Bohari ya Dawa (MSD) katika Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Muhimbili (MNH), upatikanaji wa dawa umekuwa mgumu hivyo kuifanya Muhimbili kuwa na majengo mazuri bila ya kuwa na dawa.

"Ukitaka kuona changamoto hata ukiwa ni mwanachama wa mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF) ugua au uwe na mgonjwa ambaye ni mwanachama uende katika hospitali hiyo kwanza kupokelewa tu pale mapokezi ni balaa na ukifika muda wa kutakiwa kupata dawa utaambulia panado na kuambiwa dawa hazipo" alisema Juma.

Juma aliongeza kuwa huduma ya bure kwa watu wenye msamaha hiyo ni ndoto kwani wagonjwa hao hawasikilizwi kabisa jambo ambalo ni hatari.

Alisema serikali imekuwa ikijipodoa kuwa inaboresha huduma za afya lakini hali halisi haipo hivyo akitolea mfano kwa nchi nzima maduka ya dawa ya MSD yapo nane tu je upatikanaji wa dawa na vifaa tiba utafikia katika kiwango cha kukidhi mahitaji alihoji Juma.

Janeth Mawinza alisema bajeti hiyo iangalie zaidi jinsi ya kutibu magonjwa kama ya homa ya ini ambayo matibabu yake kwa hapa nchini hayapatikani mpaka dawa itoke nchini India.

Moses Benard alisema ikiwa mjamzito aliopo mjini anatakiwa kujinunulia vifaa vya kujifungulia hali ikoje kwa yule ambaye yupo kijijjini ambaye anachangamoto ya kutokuwa na fedha na kukimbiwa na mwenza wake hivyo akaomba Waziri wa wizara hiyo kutoa tamko rasmi la kuwataka wajawazito kutonunua vifaa hivyo wanapokwenda hospitali kujifungua.

Wadau wengine waliongelea jijini Dar es Salaam maeneo mengine kama Kipunguni wilayani Ilala kukosa kuwa na zahanati au hospitali hivyo kulazimika kwenda wilaya ya Kisarawe kupata matibabu jambo ambali linashangaza hivyo wakaomba bajeti ya wizara hiyo iongezwe ili kufanikisha upatikanaji wa zahanati au hospitali katika maeneo yao.

0 comments: