MAMILIONI YA RAIA WA NIGERIA WANAKABILIWA NA BAA LA NJAA

Mamilioni ya raia wa Nigeria wanakabiliwa na baa la njaa hasa katika maeneo ambayo yana ukosefu wa amani kutokana na mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram.
Ripoti zinaonyesha kuwa, karibu raia milioni tano wa maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria wanakabiliwa na baa la njaa na wanaishi kwa kutegemea misaada ya chakula. Mashirika ya kieneo na kimataifa ya utoaji misaada ya kibinadamu yanasema kuwa, yamekuwa yakikabiliwa na changamoto nyingi katika ufikishaji misaada kwa walengwa likiwemo suala la ukosefu wa usalama na kuibiwa misaada hiyo kabla ya kuwafikia watu wenye shida nao kubwa. 
Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Toby Lanzer hivi karibuni alitangaza kuwa, watu wanaokadiriwa milioni saba katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria wanakabiliwa na hatari kubwa ya njaa na kwamba wanadhamini mlo mmoja kwa siku kwa tabu kubwa.
Rais wa kaskazini mashariki mwa Nigeria wakipokea misaada ya chakula
Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, kuna wasiwasi kwamba kundi la kigaidi la Boko Haram litawazuia raia kulima mazao ya chakula baada ya kukosa kulima kwa misimu mitatu mfululizo na kwamba suala hilo litazidisha hali mbaya katika maeneo ya kaskazini mwa Nigeria na kandokando ya Ziwa Chad. 
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa, watu wawili kati ya kila watatu miongoni mwa wakazi milioni 10.7 wa kaskazini mwa Nigeria wanahitajia misaada ya kibinadamu.

0 comments: