HIZI NI SABABU ZA KUTUMIA MAWAKALA WA USAFIRI


Kuja kwa mtandao wa intaneti kumepelekea huduma nyingi kuhamia mtandaoni na hivyo kupunguza idadi ya watu kutembelea ofisi. Kupitia tovuti za makampuni wateja wamepewa fursa kubwa ya kuperuzi huduma mbalimbali na kupata taarifa za kutosha ndani ya muda mfupi. 

Sekta mojawapo iliyoyapokea mabadiliko hayo kwa kasi kubwa ni ya utalii na usafiri. Kama unatembelea mitandao mara kwa mara nadhani utakuwa umegundua kuwa kuna kampuni nyingi zinatoa huduma hizo kama vile Jumia Travel na Expedia.

Lakini haimaanishi kuwa kuja kwa intaneti kutaondoa kuhitajika kwa mawakala. Kwa asilimia fulani idadi ya wateja kwenda au kuwasiliana na mawakala imepungua. Lakini Jumia Travel ingependa kusisitiza kuwa mawakala wana nafasi kubwa kwa wateja hususani katika masuala yafuatayo:     

Kupata ushauri wa kitaalamu. Zoezi la kupanga mchakato mzima wa kusafiri huwa linachosha sana kama hauna utaalamu mkubwa. Mara nyingi mawakala wa usafiri wanakuwa na uzoefu mkubwa katika sekta hiyo. Na hii ni kutokana na kufanya kazi kwa muda mrefu, kujuana na watoa huduma pamoja na mchakato mzima mpaka safari inakamilika. Mbali na hapo haikugharimu pesa kupata huduma zao kwani mara nyingi wao hulipwa kwa kamisheni. 

Kuokoa fedha. Mawakala wanaweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha za mteja kwani wanaweza kumpatia huduma ambazo kwa njia ya kawaida hawezi kuzipata. Na hii ni kutokana na mahusiano mazuri na ya muda mrefu kwenye biashara waliyonayo na watoa huduma. Pia kuna bei na ofa zingine huwafikia mawakala kwanza kabla ya wateja. Kwa hiyo ukiwatumia wao utafaidika nazo tofauti na ukienda kwa watoa huduma hao moja kwa moja kama mteja.  

Kuokoa muda. Zoezi zima la kupanga kusafiri iwe ndani au nje ya nchi linachosha kutokana na mlolongo mrefu ndani yake. Lakini unaweza kuutua mzigo wote huo kwa mawakala wa usafiri. Kwa sababu wao wanakuwa wamekwishafanya utafiti wa kutosha na kujua wateja wanapendelea vitu gani na ni wapi kwa kuvipata. Kwa hiyo badala ya kupoteza muda mtandaoni jaribu kuwasiliana na wakala aliye karibu nawe akusaidie huku wewe ukistarehe kwa kuweka miguu juu ukisubiria simu kujulishwa kuwa kila kitu kipo tayari. 

Ni njia salama zaidi kwa mteja. Mtu anaweza kujiuliza ni salama kivipi wakati huduma wanazotoa wao ni sawa na za makampuni husika? Jibu ni rahisi, kuna wakati matatizo hujitokeza wakati wa kusafiri, kwa mfano, kuchelewa ndege au safari kufutwa kabisa, au kutopatiwa chumba cha hoteli ulichokihitaji. Zikitokea changamoto kama hizo na wewe ulitumia wakala basi hautakiwi kuwa na wasiwasi au kugombana na mtu. Cha kufanya ni kuwasiliana na wakala wako na yeye atasuluhisha kila kitu.   

 Wanajua kipi ni bora kwa wateja wao. Kutokana na kuwepo kwenye sekta ya uwakala kwa muda mrefu, kwa mfano, miaka 10, 20 au 30, ni dhahiri kwamba watakuwa wanajua maswali ambayo wateja huuliza na majibu wanayoyatarajia. Hivyo inakuwa ni rahisi kwao kuwapatia wateja wao kilicho bora zaidi kutokana na uzoefu walionao. Na kwa kuongezea mawakala hupokea ofa mbalimbali kutoka kwa mahoteli na kampuni za usafiri kwanza kabla ya wateja. Pia wao huwa na ofa zao ili kuwavutia zaidi wateja kutumia huduma zao, kama vile kipindi cha sikukuu na mapumziko mbalimbali. 

Unapatiwa machaguo sahihi kulingana na mahitaji yako. Faida mojawapo ya kuwatumia mawakala ni kwamba wao hawatoi au kunadi huduma za kampuni moja tu pekee. Kikubwa wao wanachokizingatia ni kutoa huduma nyingi kadri wawezavyo na washirika wao wa kibiashara. Hivyo basi ni rahisi kwao kusikiliza wateja wanataka nini na kuwatimizia kulingana na huduma walizonazo. Lakini ukienda moja kwa moja hotelini au shirika la ndege ni wazi kwamba utapata huduma zao tu pekee na si vinginevyo.

Kwa ufupi ukiwa kama msafiri ni vema kutambua ni aina gani ya safari unayotaka kufanya kabla ya kutumia wakala. Kama ni safari ya kawaida na haihitaji mambo mengi unaweza kujipati huduma mwenyewe kwa kuingia mtandaoni. Wapo mawakala wengi ambao wanatoa huduma mtandaoni na pia wana ofisi, kama vile Jumia Travel wanavyoendesha shughuli zao nchini Tanzania na kwingineko ndani na nje ya Afrika.    

0 comments: