VIJANA DAR ES SALAAM WAANZISHA KLABU ZA MABADILIKO KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA MASOKONI

Mwezeshaji wa Kisheria wa Shirika la Equality for Growth (EfG), Mariam Rashid (kulia), akitoa mafunzo ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa vijana wafanyabiashara katika Soko la Ilala Mchikichini jijini Dar es Salaam kabla ya kufungua klabu za mabadiliko za kupinga ukatili huo katika soko hilo mwishoni mwa wiki.
Mwezeshaji wa kisheri Juliana Charles akichukua jina na maelezo kwa mfanyabiashara wa soko hilo aliyekubali kuwa mwana mabadiliko wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mwezeshaji wa kisheria Charles Beatus (katikati), akiwa na vijana wa klabu ya wauza nguo za mitumba ya kike katika soko la Ilala Mchikichini wakibandika bango la mabadiliko.
Vijana wa mabadiliko wa Soko la Ilala Mchikichini wakiwa 
kataika picha ya pamoja.
Mwanasheria wa EfG, Muna Abdallah akichukua maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Klabu ya Mabadiliko ya wauza nguo za kike katika soko la Ilala Mchikichini, Adam Mohamed (kushoto)
wanamabadiliko wakionesha vipeperushi vya kampeni ya Tunaweza baada ya kufungua klabu hizo.
Mwezeshaji wa kisheria Zainabu Namajoji akichukua maelezo 
kwa wanamabadiliko.
Vijana wafanyabiashara katika Soko la Ilala Mchikichini jijini Dar es Salaam wakiwa katika picha ya pamoja na wawezeshaji wa kisheria wa Shirika la Equality for Growth (EfG), wenye fulana za njano, baada ya kufungua klabu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia katika soko hilo mwishoni mwa wiki.

Maelezo yakichukuliwa.

Na Dotto Mwaibale

VIJANA wafanyabiashara katika masoko ya Temeke Sterio na Ilala Mchikichini jijini Dar es Salaam wameanzisha klabu za mabadiliko zitakazo saidia kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia masokoni kupitia kampeni ya miezi miwili ya Tunaweza inayofanywa na Shirika la Equality for Growth (EfG).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari wafanyabiashara hao wamesema kwamba wameamua kuanzisha klabu hizo za mabadiliko na kushiriki kampeni hiyo baada ya kuhamasishwa na wasaidizi wa kisheria wa Shirika la Equality for Growth (EfG) kuhusu kutokomeza vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia katika maeneo yao ya biashara.

"Kampeni hii tumeikubali na ndio maana baada ya kuhamasishwa na EfG tumeamua kufungua klabu za wanamabadiliko kwani tumeona inatujengea mazingira mazuri ya kufanya biashara zetu katika eneo ambalo halina vitendo vya ukatili wa kijinsia" alisema Adam Mohamed ambaye ni Mwenyekiti wa klabu ya mabadiliko eno la wauza nguo za mitumba ya kike Soko la Ilala Mchikichini.

Alisema kwa muda mrefu katika soko hilo kulikuwa na kukithiri kwa vitendo hivyo lakini kupitia kampeni hizo imesaidia kuvipunguza na kuwa baada ya kupata mafunzo hayo kutoka EfG wamekuwa wakiifanya kampeni hiyo hata nje ya masoko ili jamii ijue umuhimu wa kuachana na vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia.

Mwenyekiti wa klabu ya wauza viatu na raba katika Soko la Ilala Mchikichini, Philip Chuwa alisema klabu zilizoanzishwa zitasaidia kukabiliana na vitendo hivyo kwa kuwa wanachama wake ni wafanyabiashara wenyewe hivyo itakuwa rahisi kumbaini mtuhumiwa na kumchukulia hatua.

Akizungumzia kampeni hiyo ya Tunaweza Mwanasheria na Mratibu kutoka Shirika la EfG, Mussa Mlawa alisema kampeni hiyo inaendeshwa na Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake Tanzania (WLAC) lakini katika masoko inafanywa na EfG.

Alisema lengo la kampeni hiyo ni kusukuma mabadiliko ya kupinga vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia masokoni na katika jamii.

Alisema kampeni hiyo kwa Dar es Salaam inafanyika katika masoko matano ya Ilala Boma, Mchikichini, Temeke Sterio, Buguruni na Ferry.
 

0 comments: