MAREKANI YAWAWEKEA VIKWAZO WANASAYANSI 271 WA SYRIA

Marekani imewawekea vikwazo wafanyakazi zaidi ya 270 wa shirika la serikali ya Syria linalotuhumiwa kwa uundaji wa silaha za sumu, wiki kadhaa baada ya mashambulizi ya gesi ya sumu katika jimbo la Idlib.

IS Chemiewaffen Reaktionen Aleppo Syrien (picture-alliance/AP Photo)

Katika mojawapo ya hatua madhubuti kuwahi kuchukuliwa na Marekani, wizara ya fedha ya nchi hiyo imetangaza vikwazo vipya dhidi ya wanasayansi na baadhi ya maafisa wa nchini Syria kutokana na kuhusika kwao katika kuunda silaha za sumu, ambazo zinadaiwa kutumika kuwauwa raia zaidi ya watu 80 katika jimbo hilo la Idlib mapema mwezi huu.
Waziri wa fedha wa Marekani, Steven Mnuchin, amesema vikwazo hivyo vipya vinakilenga kituo cha kisayansi kinachomuunga mkono Rais Bashar al-Assad na pia wafanyakazi 271 wa kituo hicho kinachoshughulikia mitaala na utafiti wa kisanyansi (SSRC).  Marekani inadai kwamba kituo hicho kilihusika na utengenezaji wa gesi ya sumu aina ya Sarin iliyotumika katika mashambulizi hayo.
Mnuchin ameeleza kwamba Marekani inatoa ujumbe madhubuti na pia haitavumilia matumizi ya silaha za sumu yatakayofanywa na yeyote yule. "Marekani inadhamiria kuuwajibisha utawala wa Assad kwa tabia yake isiyokubalika," alisema Munchin, aliyeongeza kuwa vikwazo hivyo ni pamoja na kuwazuia Wamarekani kufanya biashara na watu hao waliotajwa.
Vikwazo baada ya mashambulizi
USA Steven Mnuchin in New York (picture-alliance/Newscom)
Waziri wa Fedha wa Marekani, Steven Mnuchin, anasema vikwazo dhidi ya wanasayansi hao vinajumuisha kugomea kushirikiana nao kibiashara na kitaaluma.
Vikwazo hivyo vinakuja wiki chache baada ya jeshi la nchi hiyo kuushambulia uwanja wa ndege za kivita wa Syria mnamo tarehe 7 Aprili ili kuuadhibu utawala wa Assad na kutoa onyo dhidi ya kufanya mashambulizi zaidi kwa kutumia silaha za sumu. 
Uwanja huo ulishambuliwa kwa makombora 59 ya masafa ya kati aina ya "Tomahawk". Huko nyuma, tayari wizara ya fedha ya Marekani ilishawawekea vikwazo maafisa wengine 18 wa Syria mnamo Januari mwaka huu.
Mashambulizi hayo ya silaha za sumu pia yalijadiliwa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini Urusi, ambayo nbi mshirika mkubwa wa Assad, iliitumia kura yake ya turufu kulizuia azimio lililoitaka serikali ya Syria itoe ushirikiano ili kuwezesha uchunguzi, huku Rais Assad akikanusha madai hayo dhidi ya nchi yake na kusema kwamba huo ni uzushi wa nchi za Magharibi.
Mnuchin amesema wizara yake "itashirikiana na wizara ya mambo ya nje pamoja na washirika wa kimataifa ili kuendeleza juhudi za kuhakikisha kwamba shughuli za kifedha za wote waliowekewa vikwazo zinafungwa."

0 comments: