Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ulikuja hapa duniani Aprili 13, 1922 kupitia kwa Mpendwa Marehemu Bibi Mgaya wa Buritho kama zawadi kwa nchi ya Tanzania.
Mwalimu tunamshukuru Mungu kwa kutupa wewe ambaye umeitendea mambo makubwa Tanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla.
Mwalimu wakati nakumbuka kuzaliwa kwako nimepata fursa ya kuangalia kazi ulizozifanya mara baada ya kuacha madaraka ya Urais na kujikita katika kazi kuu tano; Mosi pamoja na kubaki na kofia moja ya Uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ya kuimarisha Chama na alianza maandalizi ya kukabidhi Uenyekiti huo kwa Rais aliyepokea madaraka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alikuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi.
Pili, mwaka 1986 baadhi ya Viongozi wa nchi za Kusini mwa Dunia, walikuomba kuanzisha Tume ya Uchambuzi wa maendeleo ya nchi za Kusini tangu miaka 30 iliyopita na kuweza kuona hatua za maendeleo na changamoto zilizopo katika mataifa hayo na mapendekezo ya nini kifanyike ili kuboresha ustawi wa wananchi.
Mwalimu Nyerere alikubali jukumu hilo, ndipo alianza kutembelea nchi 19 katika Bara la Asia na Marekani ya Kusini kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa majukumu hayo mapya. Safari ya kutafuta maoni hayo ilikuwa ni pamoja na kupata uthibitisho wa kuwaelewesha wananchi na nchi hizo kuhusu majukumu ya Tume na aina ya maoni yanayokusanywa.
Kazi hiyo aliifanya kwa miaka mitatu na kutoa ripoti kuwa nchi za Kusini zifanye maendeleo yao yenyewe yalenge maslahi ya wananchi walio wengi kwa kielelezo kuwa ili nchi za Afrika ziweze kupiga hatua za maendeleo ni vyema ziwe na mshikamano kama zinahitaji kushindana na nchi za Kaskazini.
“Nchi za Kusini zishirikiane kibiashara, kwa kuwa nchi za Kusini zina mazoea ya kufanya biashara na nchi za Kaskazini lakini hakuna utaratibu mzuri wa nchi za Kusini kufanya biashara wenyewe kwa wenyewe, au hata katika uwekezaji rasilimali” alisema Mwalimu Nyerere.
Aidha, Mwalimu Nyerere alisema Wataalam wengi wako Kusini lakini nchi za Kusini zinatafuta wataalam kutoka Kaskazini, hivyo ni wajibu wa nchi za Kusini kujenga na kuimarisha ushirikiano wa pamoja baina yao.
Tatu, Mwalimu alianzisha kituo cha muda cha Nchi za Kusini pale Geneva ambapo Mwalimu na Viongozi wengine walifanya kazi kwa muda wa miaka miwili, jukumu lao likawa kuelezea shughuli za maamuzi na mapendekezo ya Tume.
Nne, kuanzisha Ofisi ya kudumu ya Nchi za Kusini pale Geneva kwa ajili ya Mataifa hayo kutoa hoja kupitia vuguvugu la nchi za kundi la 77 ambazo hazikuwa na chombo cha kuwasaidia kupaza sauti zao.
Mwalimu akapokea jukumu hilo na kuanzisha Ofisi ya kudumu ambayo ilikuwa chombo cha Serikali badala ya chombo cha kiraia na kuhusisha nchi 49 ambazo ziliweka sahihi, pamoja na nchi kubwa ulimwenguni ikiwemo India, Brazil na Afrika ya kusini.
Tano, alikuja na wazo la kuanzisha Taasisi ya Mwalimu Nyerere, hatua iliyotokana na harakati za kazi yake ya kuunganisha nchi za kusini, ambapo alitaka taasisi hiyo kufanya kazi zake katika ukanda wote wa nchi za Bara la Afrika.
Miongoni mwa kazi hizo ni pamoja na kuangalia maendeleo ya watu, kupitia dhana ya umoja na ushirikiano miongoni mwao.
Nakumbuka hotuba ya Mwalimu Nyerere aliitoa mwezi Februari mwaka 1960, akiwa Rais wa chama cha Tanganyika African National Union (TANU) , alikaribishwa nchini Marekani katika Kongamano la Afrika katika Chuo cha Wellesley Massachusetts kuongelea kuhusu “Nafasi ya Afrika Duniani” .
Katika hotuba hiyo, Mwalimu alizungumzia hatua mbalimbali za ukombozi wa Bara la Afrika, mchango wa Waafrika katika Mataifa ya Ulaya na Marekani. Mwalimu alilisemea Bara la Afrika Kama Bara la matumaini kwa ubaguzi wa rangi.
Mwalimu alisisistiza kwa kusema “Muda utafika ambapo Marekani na Ulaya Magharibi watajisikia vibaya jinsi walivyoitumia Afrika” huku akitolea mifano ya mateso na manyanyaso waliyoyapata Waafrika ikiwemo vita vya Mau Mau nchini Kenya, vifo vya watu wa kabila la Waherero nchini Namibia, vita vya Majimaji nchini Tanzania.
Hotuba hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Mwalimu Nyerere kuchapishwa kimataifa, hakika imeonyesha kwa dhati, Mwalimu hata kabla ya Uhuru alitambua nafasi ya umoja katika kupigania uhuru wa Bara la Afrika.
Aidha, ndoto hii ya umoja alisafiri nayo katika kujenga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Nafasi ya Uenyekiti Jumuiya wa Nchi zilizo mstari wa mbele katika Ukombozi Kusini mwa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na nyingine nyingi.
Taasisi ya Mwalimu Nyerere dhumuni lake kuu ni kuendeleza Amani, Umoja na Utulivu wa Maendeleo ya pamoja Barani Afrika. Mwalimu alikuwa muanzilishi na Mweneyekiti wa kwanza wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere.
Septemba 14, 1996 alikaribishwa Kilimanjaro hoteli kuhutubia na kuzindua Taasisi ya Mwalimu Nyerere. Umuhimu wa Umoja, umuhimu wa ukubwa wa soko, Amani baina ya nchi ndani na nje ya nchi na Maendeleo katika Afrika.
Alipata fursa ya kukutana na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwaeleza juu ya Taasisi hiyo na madhumuni yake. Katika kipindi hiki Mwalimu alikuwa msuluhishi wa mgogora wa Burundi.
Mwalimu leo ungetimiza miaka 95 tangu kuzaliwa, kimwili hatupo pamoja nawe, lakini fikra zako, mitazamo yako, utendaji wako bado ni dira na muelekeo wa Taifa letu Daima tutazifuata. Hakika siku ya leo ni siku muhimu sana kwa nchi yetu. Mungu ibariki Tanzania Mungu ibariki Afrika.
0 comments: