Katika kikao chake cha hivi karibuni mjini
Manama huko Bahrain, Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi
lilitangaza uamuzi wa kuanza ushirikiano wa kijeshi na mipango ya
kistratijia kati ya nchi wanachama.
Ushirikiano huo na mipango ya kijeshi baina ya nchi za Kiarabu
za Ghuba ya Uajemi si jambo jipya lakini swali linalojitokeza hapa ni
kwamba, ni kwa nini kikao cha Manama kimepewa mazingatio maalumu katika
vyombo vya habri ya kikanda na vya Uingereza?
kwa kiasi fulani taarifa iliyotolewa mwishoni mwa kikao cha Manama
inatoa jibu la swali hilo. Taarifa hiyo imeituhumu Iran kuwa inaingilia
masuala ya nchi za Ghuba ya Uajemi na kumefanyika jitihada za makusudi
za kudumisha propaganda chafu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na
kuiarifisha kuwa ni kituo kikuu cha vitisho vinavyolikabili eneo hilo.
Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kwa miaka kadhaa sasa
limekuwa likikariri madai yasiyo na msingi wowote dhidi ya Iran katika
taarifa za mikutano na vikao vyake. Mwenendo huo umedumishwa katika
kikao cha sasa cha baraza hilo kwa tofauti kwamba, mara hii uungaji
mkono wa serikali ya London kwa kile Waziri Mkuu wa Uingereza,Theresa
May alichokiita kuwa ni "hatua za hujuma za Tehran katika Ghuba ya
Uajemi" umejumuishwa pia katika taarifa ya Manama.
Ni wazi kuwa lengo la uungaji mkono huo wa Uingereza ni kutayarisha
mazingira ya kurejesha majeshi ya nchi hiyo katika eneo la Ghuba ya
Uajemi. Inapasa kueleweka hapa kuwa, Uingereza imekuwepo katika eneo la
Ghuba ya Uajemi kama nchi ya kikoloni kwa muda mrefu unaokaribia karne
mbili na kimsingi sehemu kubwa ya hitilafu za mipaka na madai yasiyo na
msingi kuhusu umiliki wa ardhi yanayotolewa na watawala wa kifalme wa
nchi za Kiarabu za eneo hilo ni mirathi ya kipindi cha ukoloni wa
Uingereza. Mbali na hayo, malengo ya Saudi Arabia katika mpango huo
mzima yanatofautiana kidogo na yale ya Uingereza na inaonekana kuwa
Riyadh inafuatilia malengo yake maalumu. Malengo hayo zaidi yanatokana
na ushindani wenye uharibifu kwa ajili ya kuwa na satua na udhibiti
katika nchi nyingine za eneo hilo. Ni kutokana na msimamo huo ndiyo
maana Saudi Arabia daima imekuwa ikiitazama Iran kwa jicho la mshindani.
Huu ni uhakika ambao hata Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza amekiri
ukweli wake baada ya kukosoa utendaji wa Saudia katika eneo la Ghuba ya
Uajemi katika msimamo unaoonekana kukinzana kwa kiasi fulani na ule wa
Waziri Mkuu wa nchi hiyo Theresa May. Gazeti la The Guardian la
Uingereza limeonesha mkanda wa video ambao ndani yake Waziri wa Mambo ya
Nje wa nchi hiyo Boris Johnson amekosoa vikali siasa za Saudi Arabia
katika eneo la Mashariki ya Kati japokuwa ukosoaji huo umeandamana na
uungaji mkono wa serikali ya London kwa utawala wa kifalme wa Riyadh.
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May akiwa na wakuu wa PGCC mjini Manama Bahrain
Theresa May ni mwanamke wa kwanza na Waziri Mkuu wa kwanza wa
Uingereza kushiriki katika kikao cha Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya
Uajemi na katika kikao hicho ametoa pendekezo la ushirikiano zaidi kwa
ajili ya kuimarisha usalama wa kuwekeza katika masuala ya ulinzi na
mafunzo ya kijeshi. Katika pendekezo hili pia kunaonekana aina fulani ya
kubadilika siasa za Saudia Arabia na kujielekeza zaidi kwa nchi za
Ulaya badala ya Marekani. Gazeti la El Pais la Uhispania limeandika
kuwa: Saudi Arabia inataka kuimarisha zaidi uhusiano wake na nchi
nyingine zisizo Marekani. hata hivyo ni wazi kuwa, maana nyingine ya
kubadilika kwa mwelekeo huo wa Saudia ni mgongano ulipo baina ya maslahi
ya Uingereza na Marekani hususan baada ya London kujiondoa katika Umoja
wa Ulaya.
Bahrain ambayo ilikuwa mwenyeji wa kikao hicho tangu mwaka 2011
imekuwa ikikandamiza harakati ya amani ya wananchi ya kutaka mageuzi na
kudai haki zao za kisheria ikisaidiwa na Saudi Arabia. Yumkini kwamba
moja kati ya sababu za kubadili mwelekeo wa Saudi Arabia na waitifaki
wake kama Imarati na Bahrain ni kutaka kufidia kushindwa kwao katika
masuala mbalimbali ya Mashariki ya Kati.
Bi Theresa May Waziri Mkuu wa Uingereza akizungumza mjini Manama na Mtawala wa Dubai, Sheikh Mohamed Bin Rashid
Kwa miaka mingi maafisa wa serikali ya Saudia walikuwa wakimimina
mafuta katika masoko ya kimataifa kwa shabaha eti ya kuifanya Iran
ifilisike. Hata sasa Riyadh inaonekana kurudi nyuma katika medani zote.
kwani sasa Yemen imekuwa Vietnam kwa Saudi Arabia. Kusimama kidete kwa
watu wa Yemen dhidi ya uvamizi wa Saudi Arabia na washirika wake
kumeshusha hadhi na heshima ya Saudia kijeshi na kidiplomaia. Kwa msingi
huo ili kufunika na kukimbia fedheha hiyo, Saudia na washirika wake
wanakimbilia mwavuli wa kuitaja Iran kuwa ni tishio katika jumuiya za
kimataifa.
0 comments: