|
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe
(Mb.) akihutubia katika ufunguzi rasmi wa Semina ya Ushirikiano wa
Kibiashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway iliyofanyika kwenye
Hoteli ya Hyatt Regency ya Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri
wa Biashara na Viwanda wa Norway, Mhe. Monica Maeland, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata
Mulamula, Balozi wa Norway nchini, Mhe. Hanna-Marie Kaarstad na wadau
wengine katika sekta ya biashara na uwekezaji kutoka Norway na hapa
nchini. |
|
Waziri
wa Biashara na Viwanda wa Norway, Mhe. Maeland (kulia) akimsikiliza
Mhe. Membe (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa
semina hiyo. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula na katikati ni
Balozi wa Norway hapa nchini, Mhe. Kaarstad. |
|
Waziri Membe akiendelea kuzungumza |
|
Waziri
wa Biasha na Viwanda nchini Norway Mhe. Monica Maeland naye alipata
fursa ya kuzungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya Ushirikiano wa
kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Norway, Mhe. Maeland yupo
nchini kwa lengo la kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara wa Tanzania
nchini Norway. Pia wakati wa ziara hiyo Mhe. Maeland amezindua mtambo wa
mbolea wa Yara ulioko kwenye Bandari ya Dar es Salaam na pia
atatembelea Jumuiya ya Afrika Mashariki Jijini Arusha. |
|
Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Mindi Kasiga (kulia) na mmoja wa wadau
katika semina hiyo Bw. John Ulanga (kushoto) wakifuatilia Hotuba
mbalimbali zilizokuwa zikiendelea kutolewa na Mhe. Membe na Mhe. Maeland
(hawapo pichani). |
|
Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Tunsume Mwangolombe (katikati) naye
akifuatilia ufunguzi wa Semina hiyo. |
|
Sehemu ya wadau wakifuatilia ufunguzi wa Semina hiyo |
|
Semina ikiendelea |
|
Waziri
Membe (katikati) na Waziri Maeland kwa pamoja na wajumbe waliofuatana
nao wakiwa kwenye mazungumzo mara baada ya kumaliza ufunguzi wa semina. |
|
Waziri
Membe (kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) juu
ya faida ya semina hiyo ya wafanyabiashara wa Tanzania na Norway. |
|
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea.(Picha na Reginald Philip). |
Na Mwandishi wetu
Waziri wa Mmabo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe ameisifu Serikali ya
Norway kwa kuwa mshirika wa karibu wa maendeleo wa Tanzania hususan
katika sekta za biashara na uwekezaji.
Waziri Membe alitoa kauli hiyo
kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Abdallah Kigoda wakati
akifungua rasmi semina kuhusu kuimarisha ushirikiano wa Kibiashara na
Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt
Regency Jijini Dar es Salaam leo.
Katika ufunguzi huo ambao
ulihudhuriwa pia na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Norway, Mhe. Monica
Maeland ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi, Mhe. Membe alisema kuwa
Tanzania na Norway zimekuwa na ushirikiano wa kidiplomasia kwa miaka
mingi lakini sasa nchi hizi zimeamua kushirikiana zaidi katika masuala
ya uwekezaji na biashara ili kukuza uchumi kwa maendeleo ya nchi zote
mbili.
Aliongeza kuwa, kwa miaka mingi
Tanzania imefaidika na ushirikiano na Norway katika sekta mbalimbali
ambapo nchi hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa katika kuisaidia Tanzania
kupambana na umaskini na kukuza uchumi. Hata hivyo alisema umefika
wakati sasa nchi hizi mbili zinufaike kupitia biashara na uwekezaji
ambapo nchi zote zina fursa nyingi katika maeneo hayo ikiwemo gesi na
mafuta, kilimo na madini.
Mhe. Membe alisema kuwa
kufanyika kwa semina hii itakayowakutanisha wafanyabiashara na
wawekezaji itaongeza thamani katika uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati
ya nchi hizi mbili ambapo Tanzania ina mengi ya kujifunza kutoka Norway
ambayo ni miongoni mwa nchi zinazosafirisha zaidi gesi asilia na mafuta
duniani. Hivyo aliwaasa Watanznaia kutumia semina hiyo kujifunza ili
kuimarisha sekta ya nishati ya hapa nchini.
“Semina hii ni fursa kwa
Kampuni za Tanzania na Norway kujifunza na kubadilisha uzoefu na mawazo
ya namna bora ya kuboresha sekta za biashara na uwekezaji kwa manufaa ya
nchi zote mbili” alisema Waziri Membe.
Akizungumzia biashara
inayofanyika kati ya Tanzania na Norway, Mhe. Membe alisema kuwa
Tanzania inatakiwa kuongeza biashara yake nje ya nchi ili kuimarisha
uchumi wake. Alieleza kuwa kwa sasa biashara kati ya Tanzania na Norway
imeongezeka kutoka shilingi bilioni 1.6 mwaka 2010 hadi kufikia shilingi
bilioni 6.9 mwaka 2014 kwa bidhaa zilizozwa Norway kutokea Tanzania
ikiwemo kahawa, chai, viungo, maua, mbogamboga, mbao na madini.
Kwa upande wa bidhaa kutoka
Norway, Tanzania imenunua kwa ongezeko la kutoka bilioni 22.3 mwaka 2010
hadi kufikia shilingi bilioni 73 mwaka 2014. Bidhaa hizo ni pamoja na
dawa za binadamu na bidhaa za viwandani.
Kwa upande wake Waziri wa
Viwanda na Biashara wa Norway, Mhe. Monica aliipongeza Tanzania kwa
kupiga hatua kubwa katika maendeleo na ukuaji wa uchumi ambao umefikia
asilimia 7. Alieleza kuwa Tanzania itafikia azma yake ya kuwa nchi ya
uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kwa vile inayo dhamira ya dhati na
imejipanga kupitia uvumbuzi wa gesi na mafuta, nguvukazi ya vijana na
mageuzi yaliyopo katika sekta ya uchumi.
Alieleza kuwa Norway ipo tayari
kuendelea kuisadia Tanzania katika sekta ya gesi na mafuta kwa vile
nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika eneo hilo hususan katika masuala ya
teknolojia. Aidha, aliongeza kuwa Tanzania ni mshirika wa kweli wa
Norway katika maendeleo hivyo nchi yake itashirikiana kikamilifu na
Tanzania.
“Kuna msemo maarufu unasema
kama unataka kwenda mbio nenda peke yako, lakini kama utanaka kufika
mbali nenda pamoja na mwenzako. Hivyo Norway inataka kwenda pamoja na
Tanzania ili kuziwezesha nchi hizi kufika mbali kimaendeleo” alisisitiza
Mhe. Monica.
Awali akizungumza wakati wa
ufunguzi wa semina hiyo, Balozi wa Norway hapa nchini Mhe. Hanne-Marie
Kaarstad alisema kuwa upo umuhimu mkubwa kwa nchi hizi mbili kukuza
biashara kwa kuishirikisha sekta binafsi kikamilifu kwani ni nyenzo
muhimu kwa maendeleo endelevu.
Semina hiyo ambayo imeandaliwa
kwa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Norway, Kituo cha Uwekezaji Tanzania
(TIC) na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) ilihudhuriwa na
Makampuni 34 kutoka Norway na Tanzania na pia wadau mbalimbali wa
biashara na uwekezaji
0 comments: