DKTA. MPANGO : TANZANIA YAPIGA HATUA MATIBABU YA MOYO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akipokea zawadi kutoka kwa kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Asha Izina wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo katika ukumbi wa Golden Tulip uliopo mjini Zanzibar.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na wataalamu wa afya nchini walioshiriki katika Mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo leo wakati wa ufunguzi wa mkutano huo katika ukumbi wa Golden Tulip uliopo mjini Zanzibar.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo leo katika Ukumbi wa Golden Tulip uliopo mjini Zanzibar.

Baadhi ya washiriki wa mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa katika mkutano huo leo mjini Zanzibar.

Na: JKCI




Wagonjwa wa moyo zaidi ya 800 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo, na zaidi ya 2,000 kufanyiwa upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa cathlab kwa kipindi cha miaka miwili katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).


Aidha Wagonjwa wa moyo zaidi ya laki mbili wamepatiwa matibabu katika taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili ambapo kati yao wagonjwa 2400 walitoka nchi za jirani za Comoro, Congo DRC, Kenya, Malawi, Mozambique, Rwanda, Uganda na Zambia.


Akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo leo mjini Zanzibar Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango alisema kutokana na huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo, zimeweza kuifanya JKCI kuwa taasisi ya umma inayoongoza katika kutoa huduma za matibabu ya moyo Afrika Mashariki na kati hivyo kuwavutia wanataaluma kutoka nchi za jirani zikiwemo nchi za Malawi, Zambia na Rwanda kujenga mashirikiano.


Mhe. Dkt. Mpango alisema kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Serikali imeweza kuokoa fedha nyingi takribani bilioni 63 fedha za kitanzania zilizokuwa zinatumika kwaajili ya matibabu ya moyo nje ya nchi.


Mhe. Dkt. Mpango alisema kati ya mafanikio yaliyofanywa na Taasisi hiyo ni pamoja na uanzishwaji wa kambi maalumu ya matibabu ya moyo ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan services ambayo imekuwa ikitoa huduma ya kuwajengea uwezo wataalamu wa afya waliopo katika hospitali za mikoa na kuwafikishia karibu huduma za matibabu ya moyo wananchi wanaohitaji matibabu hayo.


Aidha Dkt. Mpango alisema Serikali itaendelea kuwekeza katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kupanua huduma za matibabu na kumtaka Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kufuatilia gharama za ujenzi utakaofanyika Hospitali ya JKCI Dar Group na kuziwasilisha serikalini mapema ili serikali iweze kuwekeza katika ujenzi huo.


Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alisema serikali itaendelea kuwekeza kuboresha matibabu ya moyo nchini upande wa majengo, kuwa na vifaa tiba vya kisasa vinavyofanana na vilivyopo nchi zilizoendelea pamoja na kuwaendeleza wataalamu wa moyo kuwa mabingwa wabobezi.


“Serikali imetupa fedha shilingi za kitanzania bilioni 9 kwaajili ya kuajiri na kusomesha madaktari kuwa mabingwa wabobezi katika masuala ya moyo na hii itahusisha wataalamu wa afya ambao ni madaktari wa upasuaji, wauguzi, wafamasia, na madaktari wa usingizi”, alisema Mhe. Ummy


Mhe. Ummy alisema Tanzania kama zilivyo nchi nyingine za Afrika inakabiliwia na changamoto kubwa ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo, kisukari, shinikizo la damu na saratani.


“Wakati serikali inawekeza kwenye matibabu tunao wajibu wa kuwekeza kwenye huduma za kinga kwani kinga ni bora kuliko tiba, hivyo tusifanye mzaha kwenye mafunzo yanayotolewa na wataalamu wa afya kuhusu kubadili mtindo wa maisha na kushiriki katika mazoezi ya mara kwa mara kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza”,


“Hata tukijenga Jakaya Kikwete 200 kama watanzania hatutabadili mtindo wa maisha hazitatosha hivyo tunapaswa kuwekeza kwenye huduma za kinga kuwaokoa wale ambao hawajapata magonjwa ya moyo wasipate”, alisema Mhe. Ummy


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI imeanzisha mkutano huo wa kisayansi kwa wataalamu wa afya nchini ukiwa na lengo la kuwapa ujuzi wataalamu wa afya nchini kuhusu magonjwa ya moyo.


“Mkutano wetu unahusisha huduma za awali kabisa ambazo mgonjwa wa moyo anatakiwa kupata lengo likiwa kuokoa maisha ya wagonjwa wa moyo kwani wengi wao hufika JKCI kwa kuchelewa”, alisema Dkt. Kisenge


Dkt. Kisenge alisema kupitia mkutano huo ulioanza na kongamano la siku moja kwa vitendo kwa wataalamu wa afya wameweza kupatiwa ujuzi wa kuokoa maisha, kufanya kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography-ECHO) pamoja na mafunzo ya jinsi ya kuunganisha mishipa ya damu ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge


Aidha Dkt. Kisenge alisema ili kuendelea kusogeza huduma za matibabu karibu na wananchi JKCI inaenda kusimamia kitengo cha moyo kilichowekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato, kuhimarisha huduma za matibabu ya moyo Hospitali ya Benjamini Mkapa, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugano, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Kaskazini (KCMC) na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya.

0 comments: