WANAFUNZI WASIOONA SHULE YA MSINGI SAME WAPOKEA MSAADA WA MAHITAJI MUHIMU

 Na Mwandishi Wetu, Same


SHULE ya Msingi Same mkoani Kilimanjaro imepokea msaada vitu mbalimbali muhimu kwa ajili ya wanafunzi wasioona  katika shule hiyo wenye jumla ya  thamani ya Sh.milioni moja kutoka Mgahawa wa Ustaadhi Food Restaurant.

Msaada huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya Mgahawa huo kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan katika program ya 'Tabasam na Mama'

Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo Mkurugenzi wa Mgahawa wa Ustadhi Food Restaurant Radhia Awadhi Daffa amesema ametoa msaada huo kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa anaguswa na matatizo ya watoto wenye uhitaji hapa nchini kwa  kuwachangia gharama za matibabu na kuwapatia misaada mbalimbali.

"Ustaadhi Food Restaurant tumeamua kuendeleza program ya Tabasam na Mama kwa kuchangia mahitaji muhimu kwa wenye uhitaji  na program hii kwetu itakuwa endelevu"amesema Radhia

Mbali na hayo pia ameishukuru Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Same na Mkurugezi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kwa kumpatia ushirikiano wa kutosha katika kuwafikia watu wenye uhitaji.

Aidha Mkurugenzi huyo ametoa mwito kwa wakina mama kuwa mstari wa mbele katika kumuunga mkono Mhe Rais Dk  Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya.

Awali Mkuu wa shule ya Msingi Same Elimu ya Awali Hurumar Mgonja  amemshukuru Radhia Awadhi kwa msaada aliotoa kwa watoto hao na kuzitaka taasisi nyingine kuiga mfano kwa kuwasaidia watoto wenye uhitaji.

0 comments: