Picha na: khamisi Mussa
21/06/2023 Wadau wa afya nchini wameitaka jamii kuona
umuhimu wa kuchangia damu ili kuwezesha huduma za matibabu ikiwemo upasuaji wa moyo
kufanyika kwani changamoto ya upatikanaji wa damu imekuwa ikipelekea wagonjwa
kukosa huduma za matibabu kwa wakati.
Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa chama cha wachangia
damu kwa hiyari Tanzania Dominick Mkane alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kuona huduma zinazotolewa pamoja na kupata taarifa ya uhitaji wa
damu uliopo katika Taasisi hiyo
Mkane alisema kila mtu anaweza kuumwa na kuhitaji damu
wakati wowote hivyo ni muhimu jamii ikaelewa kuwa zoezi la kuchangia damu ni la
mzunguko kwani ipo siku mchangia damu naye atahitaji damu kutoka kwa mtu
mwingine.
“Sisi kama wachangia damu wa hiyari tunapenda kuungana
na wataalam wa afya wa JKCI kuifikia
jamii na kuielezea umuhimu wa kuchangia damu mara kwa mara kuwezesha matibabu ya wagonjwa wakiwemo wa
moyo wanaopatiwa matibabu hapa JKCI”, alisema Mkane.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya upasuaji wa
JKCI Dkt. Angela Muhozya alisema damu nyingi uhitajika katika upasuaji mkubwa
wa moyo, mgonjwa mmoja ili afanyiwe upasuaji anahitaji chupa tatu za damu na
endapo itatokea dharula mgonjwa anaweza kutumia hadi chupa kumi za damu
kufanikisha upasuaji huo.
“Ili upasuaji mkubwa wa moyo ufanyike damu ya kutosha
inatakiwa kuwepo kwani katika upasuaji mkubwa wa moyo tunasimamisha moyo na kuipeleka
damu katika mashine ya kuusaidia moyo na mapafu kufanya kazi (Heart Lung
Machine)”,
“Mashine hii ni ya mipira hivyo damu inapoingia kwenye
mashine inapoteza uhalisia wake na kuna kiwango cha damu kitakuwa hakifai tena
baada ya upasuaji kufanyika ndio maana hata baada ya upasuaji mgonjwa atahitaji
kuongezewa damu tena”, alisema Dkt. Angela
Naye mgonjwa aliyelazwa katika Taasisi hiyo Mariam Selemani
alisema alimchukua mwezi mmoja kukaa wodini kusubiria damu ili aweza kufanyiwa
upasuaji mkubwa wa moyo na baada ya kufanyiwa upasuaji huo kutokana na damu yake
kuwa ndogo kidonda chake kimechelewa kupona kwa haraka.
“Damu yangu ni ya kundi “O+” na upatikanaji wake
umekuwa wa shida lakini nashukuru ilipatikana kidogo na kuniwezesha kufanyiwa
upasuaji lakini hadi sasa sijaruhusiwa kwenda nyumbani kutokana na damu yangu
kuwa ndogo nahitaji kuongezewa damu nyingine ili kidonda kipone kabisa”, alisema
Mariam.
0 comments: