QASSEMI: KUJIUZULU HARIRI NA MATAMSHI ALIYOTOA NI HILA NYINGINE YA KUZUSHA FITNA NA MIVUTANO KATIKA ENEO

Qassemi: Kujiuzulu Hariri na matamshi aliyotoa ni hila nyengine ya kuzusha fitna na mivutano katika eneo
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kujiuzulu Saad Hariri wadhifa wa uwaziri mkuu wa Lebanon ni ishara ya hila mpya inayofanywa ili kuzusha mivutano ndani ya Lebanon na eneo la Mashariki ya Kati.
Bahram Qassemi ameyasema hayo sambamba na kupinga matamshi aliyotoa Hariri dhidi ya mchango na nafasi ya Iran katika eneo na kubainisha kwamba: kukariri tuhuma hewa na zisizo na msingi za Wazayuni, Wasaudi na Wamarekani dhidi ya Iran kulikofanywa na Waziri Mkuu wa Lebanon aliyejiuzulu ni ithbati kwamba kujiuzulu huko ni hila na mchezo mpya wa kuanzisha fitna na mivutano mipya ndani ya Lebanon na katika eneo, lakini wananchi wanamuqawama wa Lebanon watakivuka kipindi hiki pia bila ya tabu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa: Iran imekuwa siku zote ikitaka kuwepo amani na uthabiti katika nchi za eneo huku ikiamini kwamba maslahi yake yanakidhiwa kwa kuwepo amani, uthabiti na ustawi wa uchumi katika nchi zote jirani na za eneo; na ni kwa sababu hiyo ndio maana kukabiliana na machafuko na uvurugaji uthabiti na kupambana na makundi ya kigaidi kwa ajili ya kurejesha uthabiti katika nchi zote kumepewa kipaumbele katika sera zake za kieneo.
Saad Hariri, akitangaza kujiuzulu wadhifa wa uwaziri mkuu wa Lebanon
Huku akiashiria pia kwamba kujiuzulu Saad Hariri na kutolewa tamko hilo katika nchi nyengine sio tu ni jambo la kushangaza na kusikitisha lakini pia kunadhihirisha kuwa anacheza mchezo katika uwanja uliotayarishwa na wanaolitakia mabaya eneo hili, Qassemi ameongeza kuwa: atakayeibuka mshindi kwenye uwanja huo ni utawala wa Kizayuni ambao uhai na uwepo wake unadumu kwa kuwepo mizozo na mivutano kati ya nchi za Kiislamu za eneo la Mashariki ya Kati.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran ameashiria uhusiano mzuri sana uliopo baina ya Tehran na Beirut na kubainisha kwamba: kama alivyosisitiza hivi karibuni Rais Michel Aoun wa Lebanon juu ya kuwepo uhusiano mzuri wa kisiasa baina ya nchi mbili na kukanusha tuhuma za kuwepo uingiliaji wowote wa Iran katika masuala ya Lebanon, Jamhuri ya Kiislamu daima imekuwa ikiheshimu uhuru, kujitawala na kulindwa uthabiti na utulivu ndani ya nchi hiyo na kutangaza utayari wake wa kushirikiana na serikali ya Beirut katika nyanja zinazokidhi maslahi ya nchi mbili.../

0 comments: