UMOJA NA MSHIKAMANO BAINA YA WAISLAMU, MAJIBU BORA KWA WATENDAJI JINAI

Habari kutoka katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni zinaonesha kushtadi jinai dhidi ya Wapalestina na jambo hilo limelifanya kuwa la wajibu suala la kuleta umoja na mshikamano haraka iwezekanavyo katika safu za Waislamu na wapenda haki duniani, kwa ajili ya kupambana na Israel na kuilazimisha ikomeshe jinai zake dhidi ya wananchi madhlumu wa Palestina.
Udharura huo umejitokeza katika hali ambayo Waislamu hivi sasa wamo katika Wiki ya Umoja inayoadhimishwa kwa mnasaba wa Maulid ya Bwana Mtume Muhammad SAW. 
Matukio ya eneo la Mashariki ya Kati katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita yanaonesha kuwa, msamiati mpya wa kisiasa ambao mhimili wake ni kupinga uvamizi na kuwaunga mkono wanyonge duniani mbele ya ubeberu wa waistikbari; na ambao pia msingi wake ni mafundisho matukufu ya dini ya Kiislamu; umeingia katika kamusi ya misamiati ya kimataifa, kwa baraka za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Ni jambo lililo wazi kwamba, iwapo kadhia ya Palestina na kukaliwa kwa mabavu maeneo mbalimbali ya Palestina hususan mji mtakatifu wa Baytul Muqaddas itafanywa kuwa maudhui kuu ya kuunganisha nguvu za kupambana na mabeberu, bila ya shaka yoyote jambo hilo litavunja kivitendo njama zote za waistikbari wanaofanya kila wawezalo kujaribu kuififiliza kadhia ya Palestina. Wazayuni na waungaji mkono wao wanatumia njama mbalimbali kuwasahaulisha walimwengu suala la Palestina na kuficha jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya taifa hilo madhlumu. Njama yao kuu ni kujaribu kulifanya suala la Palestina kuwa linahusiana na Wapalestina wenyewe tu au kwa zaidi linahusiana na Waarabu na halihusiani kivyovyote vile na ulimwengu wa Kiislamu, ili kwa njia hiyo wawapokonye Waislamu haki yao ya kupigania ukombozi wa maeneo yao matakatifu ya Palestina.
Mkutano wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu mjini Tehran
Aidha Wazayuni wanafanya mashambulizi ya mtawalia dhidi ya Wapalestina ili kuwadhoofisha na kuendeleza siasa zao za kupora ardhi za Wapalestina hao. Lakini njama zote hizo zimeshindwa kutokana na kuwa macho wananchi wa Palestina kiasi kwamba siku ya Jumatano, wakati idadi kubwa ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni walipoingia kwenye kambi ya wakimbizi ya Shuafat (Sha'fat) kwa madai ya kufanya mazoezi ya kijeshi, Wapalestina walisimama kidete na kupambana vikali na wanajeshi hao vamizi wa Israel. 
Hii ni katika hali ambayo, tangu ilipoanza Intifadha ya Quds mwezi Oktoba 2015 hadi hivi sasa, Wapalestina 268 wameshauawa shahidi. Bila ya shaka ni kwa kuzingatia hatari kama hizo ndio maana Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akawa anasisitizia mara kwa mara udharura wa kushikamana Waislamu na kulindwa malengo matukufu ya taifa la Palestina. Ayatullah Khamenei amekuwa akisisitiza kuwa, iwapo Wapalestina wataungana na iwapo Waislamu wengine watashirikiana na Wapalestina hao walioungana katika kukabiliana na Wazayuni, basi utawala wa Kizayuni wa Israel hauwezi kudumu kwa zaidi ya miaka 25 ijayo.
Nukta ya kutaamali hapa ni kwamba, njia pekee ya kukomboa haki za taifa la Palestina na kuikoa Quds Tukufu ni muqawama na mapambano kwani njia nyingine zote zilizobakia ni tasa na hazina mwisho mwema. Hivyo uungaji mkono wa pande zote kwa wanapambano wa Palestina inabidi iwe ndio ajenda kuu ya Waislamu wote na kila mpenda haki duniani.
Quds, Kibla cha Kwanza cha Waislamu

Jambo jengine ambalo halipaswi kusahauliwa ni kwamba mabeberu wanafanya njama za kuwashughulisha Waislamu na migogoro ya ndani ili kuwasahaulisha kadhia ya Palestina. Hivyo kukabiliana kwa pamoja na makundi ya wakufurishaji kama vile Daesh na magenge mengine ya kigaidi ni wajibu wa kila mtu kwani kinyume na hivyo, kuna hatari kadhia ya Palestina ikawekwa pembeni kutokana na migogoro inayozushwa kila uchao na magenge hayo ya kitakfiri.
Hivi sasa Waislamu wamo katika Wiki ya Umoja, wiki ambayo ni fursa bora ya kuwaunganisha na kuwafanya wawe kitu kimoja. Ni jambo lisilo na shaka hata kidogo kwamba, fursa hiyo inabidi itumiwe vyema kuwakumbusha Waislamu kuwa kadhia yao kuu ni suala la Palestina na kwamba magenge ya kigaidi na kitakfiri ni katika njama za maadui wa Uislamu za kuwavunja nguvu Waislamu na kuwasahaulisha kadhia yao kuu, yaani kupambana na Israel ambayo inayakaliwa kwa mabavu maeneo yao matakatifu huko Palestina, ikiwemo Quds, ambacho ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu.

0 comments: