RAIS ROUHANI ATUMA SALAMU ZA PONGEZI KWA VIONGOZI WA NCHI ZA KIISLAMU KWA MNASABA WA MAULIDI YA MTUME (S.A.W)

Rais Hassan Rouhani ametuma salamu za mkono wa pongezi, heri na baraka kwa viongozi wa nchi za Kiislamu kwa mnasaba wa maadhimisho ya kukumbuka kuzaliwa Mtume Mtukufu, Nabii Muhammad Al-Mustafa SAW.
Katika ujumbe wa salamu hizo alizowatumia viongozi wa nchi za Kiislamu, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema ana matumaini kwamba kwa baraka za maulidi matukufu ya Bwana Mtume SAW ambaye ni mtoa bishara ya heri na rehma na dhihirisho la akhlaqi bora na ruwaza njema, mfungamano wa udugu na urafiki baina ya mataifa ya Waislamu utazidi kustawi zaidi.
Katika salamu zake hizo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa: Nchi za Kiislamu zinapaswa kuitumia na kufaidika nayo mirathi adhimu ya Bwana Mtume SAW kwa kufanya juhudi na bidii zaidi za kuwabainishia na kuwaonesha walimwengu sura ing'arayo ya rehma na amani ya Uislamu.
Aidha amebainisha kwamba kwa kushikamana na umoja na kupata funzo kutoka kwenye chemchemi safi ya elimu ya Utume, Umma wa Kiislamu utaweza kurejesha kikamilifu amani, utulivu na uthabiti katika nchi za Kiislamu.
Kwa mtazamo wa madhehebu ya Suni, tarehe 12 Mfunguo Sita, Rabiul Awwal, na kwa mtazamo wa madhehebu ya Shia, tarehe 17 ya mwezi huo ndio siku aliyozaliwa Bwana Mtume Muhammad SAW. Imam Khomeini (RA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza kipindi cha baina ya tarehe mbili hizo kuwa ni Wiki ya Umoja ili kuimarisha umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu.../

0 comments: