Kundi la kigaii la al Shabab limezidisha mashambulizi yake katika maeneo ya umma na yenye idadi kubwa ya watu nchini Somalia.
Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita pekee kundi hilo
limeshambulia bandari kubwa ya Mogadishu na kuua watu karibu mia moja.
Mashambulizi hayo yamezusha wasiwasi mkubwa kwa wakazi wa vitongoji vya
mji wa Mogadishu.
Kundi la al Shabab ambalo ni tawi la kundi la kigaidi la al Qaida
katika eneo la mashariki mwa Afrika, liliundwa na wanachama waliojitenga
na Muungano wa Mahakama za Kiislamu hapo mwaka 2006 na kuanzisha vita
dhidi ya serikali ya wakati huo ya Somalia kwa kisingizio cha kuanzisha
utawala wa Kiislamu.Takwimu zinaonyesha kuwa, katika kipindi cha muongo
mmoja wa kuanzia 2006 hadi 2016 kundi la al Shabab limefanya
mashambulizi 364 ya kigaidi. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini
kuwa, kundi la kigaidi la al Shabab linasaidiwa kifedha na kijeshi na
Eritrea, japokuwa serikali ya Asmara inakanusha madai hayo.
Wapiganaji wa kundi la kigaidi la al Shabab
Baada ya kuasisiwa, kundi hilo liliteka maeneo mengi ya katikati na
kusini mwa Somalia. Hata hivyo Disemba 2012 jeshi la Somalia
likishirikiana na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika
lilifanikiwa kuwafukuza wapiganaji wa al Shabab katika bandari muhimu ya
Kismayo na mjini Mogadishu. Kufurishwa katika maeneo hayo muhimu
kulipunguza kwa kiwango fulani uwezo na ushawishi wa kundi hilo la
kigaidi. Vilevile kutimuliwa Mogadishu na katika maeneo mengine muhimu
ya kistratijia kulilifanya kundi la al Shabab lianzishe mashambulizi ya
kulipiza kisasi hususan katika nchi za Kiafrika zilizotuma askari wa
kulinda amani nchini Somalia. Miongoni mwa mashambulizi hayo ni
yale yaliyolenga kituo cha kibiashara cha Westgate jijini Nairobi na
Chuo Kikuu cha Garisa ambayo yameua mamia ya watu na shambulizi la
kigaidi la Kampala wakati wa mechi za soka za Kombe Dunia mwaka 2010
zilizofanyika nchini Afrika Kusini. Vilevile kufurushwa kundi la al
Shabab katika maeneo na ngome zake muhimu kulikata vyanzo la pato vya
kundi hilo.
Mashambulizi ya al Shabab dhidi ya raia katika maeneo ya umma
Kundi la al Shabab ambalo wakati wa kuasisiwa kwake lilifanikiwa
kusajili vijana wengi wa Kisomali kwa ahadi za kurejesha amani na
utulivu nchini humo, katika miaka ya hivi karibuni limeshindwa na kupata
pigo katika jitihada za kusajili wapiganaji wapya. Pamoja na hayo bado
linadhibiti baadhi ya maeneo ya vijijini na limekuwa likifanya
mashambulizi ya kuvizia na kujilipua kwa mabomu katika maeneo ya mijini.
Kwa sasa kundi la al Shabab limezidisha mashambulizi ya kigaidi
katika maeneo ya umma na yenye idadi kubwa ya watu mijini katika kipindi
hiki ambapo serikali ya Somalia inajitayarisha kwa ajili ya uchaguzi
mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 28 Disemba. Mashambulizi hayo
yanafanyika kwa shabaha ya kukwamisha zoezi hilo muhimu la kidemokrasia.
Inatarajiwa kuwa uchaguzi wa 28 mwezi huu nchini Somalia utasaidia
kutayarisha mazingira ya kuundwa serikali kuu imara katika nchi hiyo
ambayo imekuwa ikisumbuliwa na machafuko ya ndani na migogoro ya kisiasa
tangu miongo miwili iliyopita.
0 comments: