Zaidi ya wahamiaji 700 wanahofiwa kufa maji katika Bahari ya Mediterenia
kutokana na kuzama kwa mashua zao wiki iliopita licha ya kwamba meli za
uokozi zimewaokoa maelfu ya wengine katika operesheni ngumu kabisa.
"Nataka kuiambia dunia kwamba njia hii hatari sana kwetu kwa sababu kaka
yangu, dada yangu watakuja kupoteza maisha yao katika mkondo huu wa
bahari.Tafadhali tusaidieni tuwe na uhuru katika nchi yetu . Sitaki
kubakia hapa au mahala pengine popote pale.Nataka nchi yangu iwe na
uhuru."
Hiyo ni kauli ya Habtom Tekle raia wa Eritrea mwenye umri wa miaka 27
akiwa ni miongoni mwa wahamiaji walionusurika katika janga la kuzama kwa
mashua za wahamiaji wiki iliopita katika bahari ya Mediterenia na
kusababisha maafa ya mamia ya wahamiaji.
Kuzama kwa mashua zao hizo kumesababisha idadi kubwa ya vifo kutokea
katika Bahari ya Mediterenia tokea maafa ya mwezi wa Aprili mwaka 2015
ambapo mashua moja ilizama ikiwa na wahamiaji 800.
Mashua zinazama bila kujulikana
Mashirika ya misaada ya kibinaadamu yanasema mashua nyingi za
wahamiaji zinazama bila ya kugundulikana na watu waliokufa kutopatikana
kabisa isipokuwa majaaliwa yao kuja kujulikana baada ya familia zao
kuripoti kwamba hawakuwasili Ulaya walikokuwa wakiwatarajia.
Bahari iliyo shwari pamoja na utulivu wa hali ya hewa hivi karibuni
kumesababisha kuongezeka kwa idadi ya wahamiaji wanaojaribu kukimbilia
Ulaya.
Idadi kubwa ya wahamiaji wasiojulikana walipo na wanaodhaniwa kuwa
wamekufa walikuwa kwenye mashua ya uvuvi iliokuwa ikiburuzwa na mashua
nyengine ya kusafirisha watu kwa magendo kutoka bandari ya Sabratha
nchini Libya iliyozama Alhamisi.
Makadirio ya maafa
Makadirio ya polisi na mashirika mengine ya misaada ya
kibinaadamu kwa kuzingatia maelezo ya wahamiaji walionusurika, ni kuwa
watu kati ya 400 hadi 500 hawajulikani walipo kutoka katika mashua hiyo
iliyozama.
Kwa mujibu wa polisi ya Italia, watu 300 waliokuwa katika eneo la chini
katika mashua ya pili walizama na mashua yao hiyo, wakati wengine kama
200 waliokuwa sehemu ya juu ya mashua hiyo walichupa baharini, lakini ni
90 tu walioweza kuokolewa pamoja na wengine 500 waliokuwemo katika
mashua ya kwanza.
Kwa mujibu wa shirika la kutetea watoto la Save the Children wengi wa
wahamiaji walikuwa ni raia wa Eritrea, wakiwemo wanawake na watoto.
Uturuki yatishia kutelekeza makubaliano
Hayo yanajiri wakati serikali ya Uturuki ikitishia kuyatelekeza
makubaliano na Umoja wa Ulaya ya kudhibiti wimbi la wakimbizi barani
Ulaya, iwapo raia wake hawatoruhusiwa kusafiri barani Ulaya bila ya
visa.
Wakati pande hizo mbili zikiwa katika mvutano mkubwa, Waziri wa Mambo ya
Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, amesema haiwezekani kwa serikali ya
Uturuki kubadili sheria zake za kupambana na ugaidi ambazo Umoja wa
Ulaya unataka zirekebishwe kama moja ya masharti ya kuondosha viza kwa
Waturuki wanaoingia Ulaya.
Akitilia mkazo kauli ya Rais Recep Tayyip Erdogan wiki iliyopita, waziri
huyo amesema ikibidi Uturuki itachukuwa hatua za kiutawala kukwamisha
makubaliano hayo.
Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/AP
Mhariri: Mohammed Khelef
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: