RAIS MAGUFULI AFUTA SAFARI ZOTE ZA WATUMISHI KWENDA NG'AMBO
Posted by khamisimussa77@gmail.com at 8:16 PM
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli leo asubuhi
katika Ikulu ya Dar es Salaam amefanya kikao na Makatibu wakuu, Manaibu
Makatibu wakuu, Gavana wa Benki Kuu Prof. Benno Ndulu na Kamishna Mkuu
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kutoa uelekeo wa Serikali
anayoitaka mara baada ya kuapishwa.
“Nataka
Serikali iendelee kwa nguvu zote na katika kutekeleza dhana ya ‘HAPA
KAZI TU’ na viongozi kuzingatia na kukumbuka ahadi nilizotoa ili zianze
kuonekana na kufanyiwa kazi mara moja” Rais Magufuli amesema.
Katika Kikao chake,
Rais ametoa mwongozo na kusisitizia kuwa ni lazima kila mtendaji
Serikalini kuuzingatia, kufuata sheria na taratibu ili taifa lisonge
mbele kwa ufanisi zaidi.
Katika kikao hicho
Rais ameelekeza mambo kadhaa ambayo watendaji hao wanapaswa kuyasimamia,
kuyawekea mikakati na kuyapanga vizuri ili atakapo teua Baraza lake la
Mawaziri mambo hayo yawe tayari ili Mawaziri watakaoteuliwa waweze
kuyasimamia bila kukosa.
Mambo hayo muhimu ni kama ifuatavyo:
Kuanzia mwezi Januari
mwaka 2016, wanafunzi wote wanaoanza shule watasoma bure bila kulipa
ada, Katika jambo hili, Rais amewataka watendaji kuanza kuliwekea
mikakati tayari kwa utekelezaji
Suala la mikopo ya wanafunzi nalo lifanyiwe kazi na mipango yake ikamilike kwa ajili ya utekelezaji mzuri zaidi.
Amefuta safari zote za
nje ya nchi kuanzia leo hadi hapo atakapolitolea suala hilo maamuzi
mengine na kueleza kuwa shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi
zifanywe na kusimamiwa na mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha nchi huko
nje.
Pengine patokee
jambo la dharura sana na hata hilo lazima kibali kitolewe na Rais au
Katibu Mkuu Kiongozi. Badala yake Rais amewataka watendaji hao kufanya
zaidi ziara za kwenda vijijini ili kuzijua na kutatua kero za wananchi
wa Tanzania.
Katika Kikao hicho,
Rais amemtaka Kamishna wa TRA, Ndugu Rished Bade kusimamia kwa makini
zoezi la ukusanyaji wa mapato nchini na kuhakikisha kero ndogo ndogo kwa
wananchi lianze kutekelezwa kama alivyo ahidi kwa kufanyiwa kazi mapema
zaidi.
Rais ameitaka TRA
kukusanya mapato hayo kutoka kwa wafanya biashara wakubwa zaidi na wale
wanaokwepa kodi bila kuogopa mtu wala taasisi yoyote hapa Tanzania na
kusisitiza kuwa katika Serikali hii wa kutoa maamuzi vinginevyo zaidi ya
haya ni yeye Rais ama Makamu wake.
Rais Magufuli pia
ameagiza usimamizi katika suala la manunuzi ambalo limekuwa likitumika
vibaya na kuwa mwanya wa kuibia Serikali kwa watu kuongeza bei ya vitu
hata kama ni vya bei ndogo kabisa katika jamii.
“Ikitokea suala hilo
likagundulika kwa watu kuongeza bei ya vitu, watendaji watawajibishwa
mara moja”. Rais amesema, na kuwataka watendaji hao kufanya kazi zao kwa
kuzingatia Sheria na taratibu zilizopo na kuzingatia maadili mema ya
kazi.
………………………MWISHO……………………
Imetolewa na Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
7 Novemba, 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: