Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe.
John Henjewele akifungua mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kudumu la
wapiga kura yaliyofanyika Juni 5, 2015 Katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Morogoro. Kulia, ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Kilombero Bi Azimina Mbilinyi.
Bi.
Sajira Mbaga ambaye ni Afisa kutoka tume ya Taifa ya Uchaguzi,
akihojiwa nawaandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo.
Baadhi
ya wajumbe wa mafunzo hayo wakila kiapo cha uaminifu katika utekelezaji
wa zoezi ambalo liko mbele yao. Kushoto ni Hakimu Mkazi Bi. Agnes
Ringo.
Baadhi ya vifaa vilivyowasili Mkoani Morogoro kwa ajili ya zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
…………………………………………………………
Na Andrew Chimisela Afisa Habari
Mkoa wa Morogoro umeanza maandalizi ya uboreshaji wa daftari
la kudumu la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi Mkuu wa Wabunge na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika Mwezi Oktoba
mwaka huu.
Maandalizi hayo yameanza jana kwa semina ya siku mbili
inayotolewa kwa waratibu wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga
kura katika ngazi ya Mkoa na Wilaya za Mkoa wa Morogoro.
Semina hiyo inalenga kutoa Elimu itakayowawezesha kutekeleza
jukumu hilo katika kufanikisha zoezi hilo muhimu. Mafunzo hayo
yatahusisha ujazaji wa fomu zitakazotumika kwenye zoezi zima la
uboreshaji la wapiga kura.
Aidha, yatatolewa mafunzo kwa vitendo yatakayohusu jinsi ya
kutumia kifaa cha kisasa yaani Biometric Voters Registration (BVR)
kinachochukua alama mbalimbali za mpiga kura kwa lengo la kuondoa
uwezekano wa mtu kujiandikisha zaidi ya mara mbili.
Akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rajabu
Rutengwe kupitia hotuba iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. John
Henjewele, aliwataka wanasemina kujifunza kwa bidii na kuhakikisha
wanajua utaratibu unaotakiwa kutumika katika kuboresha daftari hilo la
kudumu la wapiga kura.
Dkt. Rutengwe alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wa Mkoa wa
Morogoro kujiandikisha katika vituo vyao mara muda utakapowadia wa
kufanya hivyo. “Naomba kutoa wito kwa wananchi walio na sifa ya kuwa
wapiga kura Mkoani hapa waweze kujitokeza ili wajiandikishe”. Alisema.
“Aidha, napenda kuwahakikishia kwamba Serikali Mkoani hapa
imedhamiria kuhakikisha zoezi hili linafanyika kwa ufanisi mkubwa na
kufanikiwa” Dkt. Rutengwe aliongeza.
Naye Bi. Sajira Mbaga, Afisa kutoka Tume ya Uchaguzi alisema,
zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa Mkoa
wa Morogoro, linatarajiwa kuanza kufanyika Juni 14 mwaka huu na kuongeza
kuwa Tume hiyo inaendelea na jitihada za kuondoa changamoto
zilizojitokeza kwenye zoezi hili katika Mikoa mingine ambapo zoezi hili
limekwisha fanyikaA.
0 comments: