WAFANYAKAZI WA UMOJA WA MATAIFA WASHAMBULIWA SUDAN

Watu wenye silaha wamewalenga wafanyakazi wanne ambao ni wajumbe wa kamati ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika katika mji wa Nyala katikati mwa mkoa wa Darfur Kusini nchini Sudan.
Katika hujuma hiyo wafanyakazi hao wa UN wametekwa nyara na mwingine mmoja kuuawa. Habari zaidi zinaarifu kuwa, watu watano waliokuwa wamejifunga niqabu nyusoni mwao na wakitumia gari lisilokuwa na namba za usajili, waliwazuia wafanyakazi hao akiwemo mwanamke mmoja na kisha kuwateka nyara na kumuua mmoja wao.
Chanzo kimoja cha kamati hiyo ya Umoja wa Mataifa kimenukuliwa kikisema kuwa, tukio hilo limejiri karibu na chuo kidogo cha elimu na viwanda mjini hapo Nyala wakati wafanyakazi hao walipokuwa njiani kuelekea ofisi moja ya Umoja wa Mataifa katika eneo la Saqra, kaskazini mashariki mwa mji huo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo baada ya uvamizi huo, washambuliaji walimmiminia risasi mwanamke miongoni mwa wafanyakazi hao na kuondoka na wengine. Mkuu wa polisi mkoa wa Darfur Kusini amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa, polisi wamejiweka katika hali ya tahadhari ambapo wamefunga njia zote za kuingia na kutoka mkoani hapo. Hadi sasa hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo.

0 comments: