Uchaguzi uliofutwa mwaka jana katika visiwa vya Zanzibar ambayo
ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unatarajiwa kufanyika
Jumapili ya kesho huku Tume ya Uchaguzi (ZEC) ikitangaza kuwa,
maandalizi yote kwa ajili ya uchaguzi huo yamekamilika.
Licha ya Chama cha Wananchi CUF kutangaza kuwa, hakitasimamisha
mgombea wake katika uchaguzi wa kesho, lakini karatasi za kupigia kura
zilizowasili hivi karibuni zikitokea nchini Afrika Kusini zina picha za
wagombea wote 14 wa kiti cha Urais wa Zanzibar.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kurudiwa uchaguzi huo
ndio utakaokuwa ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa Zanzibar ulioibuka mwaka
jana baada ya matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25 kufutwa, lakini weledi
wengine wa mambo wanasema, kutoshiriki chama cha CUF katika uchaguzi wa
kesho kutapelekea mgogoro huo uendelee kushuhudiwa hasa kwa kutilia
maanani nguvu kubwa ya chama hicho katika siasa za Zanzibar.
Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliingia
katika mgogoro wa kisiasa mwezi Oktoba mwaka jana baada ya Mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi visiwani humo, Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya
uchaguzi kwa kile alichokiita ukiukwaji wa sheria na utaratibu wakati wa
zoezi la upigaji kura. Hatua hiyo ilichukuliwa katika hali ambayo
matokeo yote ya uchaguzi wa majimbo 54 ya Baraza la Wawakilishi yalikuwa
yameshatangazwa pamoja na karibu theluthi mbili ya kura za Urais.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: