RAIS MSTAAFU DK. JAKAYA KIKWETE AWASILI TUNIS, TUNISIA

J1Rais Mstaafu wa awamu ya nne na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika katika Mgogoro wa Libya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akimkaribisha Waziri wa Manghreb, nchi za Kiarabu na Afrika wa Aljeria Mheshimiwa Abdelkader Messaleh, aliyemtembelea hotelini kwake katika Jiji la Tunis, Nchini Tunisia.
J2Rais Mstaafu wa awamu ya nne na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika katika Mgogoro wa Libya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akizungumza na Waziri wa Manghreb, nchi za Kiarabu na Afrika wa Aljeria Mheshimiwa Abdelkader Messaleh, aliyemtembelea hotelini kwake katika Jiji la Tunis, Nchini Tunisia.
J3Rais Mstaafu wa awamu ya nne na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika katika Mgogoro wa Libya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akiagana na Waziri wa Manghreb, nchi za Kiarabu na Afrika wa Aljeria Mheshimiwa Abdelkader Messaleh, aliyemtembelea hotelini kwake katika Jiji la Tunis, Nchini Tunisia.
…………………………………………………………………………………….
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika wa Usuluhishi wa Mgogoro wa Libya, amewasili jana Jijini Tunis nchini Tunisia  kushiriki Mkutano wa 8 wa Nchi majirani wa Libya.
Mkutano huo umeitishwa na Serikali ya Tunisia, na ni muendelezo wa jitihada za nchi majirani kusaidia kuleta hali ya amani na usalama nchini Libya.
Rais Mstaafu Kikwete amewasili Tunis akitokea Salalah nchini Oman alikoshiriki Mkutano wa Kamati ya Bunge la Kuandika Katiba ya Libya.
Akiwa Jijini Tunis, Jana tarehe 22 Machi, 2016 Dkt. Kikwete amefanya mazungumzo na Waziri wa Masuala ya Maghreb, nchi za Kiarabu na Afrika, wa Algeria Mheshimiwa Abdelkader Messaleh, aliyemtembelea hotelini kwake.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Messaleh amempongeza  Rais Mstaafu Kikwete kwa kuteuliwa na Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika kusuluhisha mgogoro wa Libya. Amemueleza hali ya usalama na kisiasa ya  Libya na mtizamo wa nchi yake juu ya namna bora ya utatuzi wa mgogoro huo, na akamhakikishia ushirikiano wa Serikali ya Algeria katika jukumu lake alilokabidhiwa na Umoja wa Afrika.
Kwa upande wake, Rais Mstaafu Kikwete amemshukuru Waziri Abdelkader Messaleh kwa maelezo yake na ushirikiano aliomuahidi na akamueleza matumaini yake ya kupatikana kwa suluhu ya mgogoro huo hasa ikizingatiwa kuwa nchi jirani na Libya na Umoja wa Afrika zitashirikiana na wadau wote kuhakikisha mgogoro huo unatatuliwa.
Rais Mstaafu Kikwete amesisitiza kuwa suluhisho la kudumu la mgogoro wa Libya liko mikononi mwa wananchi wa Libya wenyewe.
Katika ziara yake nchini Tunisia, mbali na kuhudhuria Mkutano wa 8 wa nchi jirani na Libya,  Rais Mstaafu Kikwete anatarajiwa pia kukutana na Waziri Mkuu Mteule na Mwenyekiti wa Baraza la Utawala la Libya,  (Presidency Council) Mheshimiwa Fayez Al-Sarraj,  wadau wengine wa Libya  pamoja na kutembelea Ofisi ya Ujumbe wa Umoja wa Afrika kwa Libya iliyoko jijini Tunis.
Rais Mstaafu Jakaya Kikwete anatarajiwa kurejea nchini tarehe 25 Machi, 2016.
Imetolewa; Ofisi ya Rais Mstaafu.
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Tunis
22 Machi, 2016

0 comments: