Mshukiwa
mkuu wa mashambulizi ya kigaidi ya Paris Salah Abdesalam amejeruhiwa na
kukamatwa na maafisa wa usalama katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels
hapo jana Ijumaa katika msako mkubwa
Abdeslam
mwenye umri wa miaka 26 na washukiwa wengine wanne walikamatwa katika
mtaa wa Molenbeek mjini Brussels. Waendesha mashitaka wamesema mshukiwa
huyo wa mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika mwezi Novemba mwaka jana
katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris alijeruhiwa mguuni wakati wa
operesheni hiyo ya polisi ya kumkamata.
Abdeslam
anaaminika ndiye aliyapanga mashambulizi ya kujitoa muhanga katika
maeneo mbali mbali mjini Paris ambayo yalisababisha vifo vya watu 130 na
kusababisha watu wengine 350 kupata majeraha. Rais wa Ufaransa Francois
Hollande amesema vita dhidi ya ugaidi havikomi baada ya operesheni hiyo
ya jana jioni licha ya kuwa ni ushindi.
Hollande
ambaye pamoja na Waziri mkuu wa Ubelgiji Charels Michel walifanya
mkutano wa pamoja kwa wanahabari, amesema anawafikiria waathiriwa wa
mashambulizi ya tarehe 13 Novemba kwasababu Salah Abdeslam alihusika
moja kwa moja katika maandalizi, uratibu na kutekeleza mashambulizi
hayo.
Rais huyo
wa Ufaransa amesema ataomba Abdeslam kupelekwa Ufaransa kutoka Ubelgiji
haraka iwezekanavyo ili kufunguliwa mashitaka. Hollande anatarajiwa
kufanya mkutano wa baraza la ulinzi na usalama Jumamosi kufuatia
kukamatwa kwa mshukiwa huyo ambaye alikuwa anasakwa kote barani Ulaya.
Michel
ambaye alilazimika kuondoka ghafla kutoka mkutano wa kilele wa viongozi
wa Umoja wa Ulaya na Uturuki wa kujadili suala la wahamiaji, amesema
kukamatwa kwa Abdeslam ni hatua muhimu sana kwa taifa lake katika vita
dhidi ya kuenea kwa itikadi kali.
Mshukiwa
mwinine aliyekamatwa katika operesheni hiyo ni mwanamume anayejulikana
kwa jina bandia Amine Choukri ambaye pia anatumia jina jingine la
kisyria la Monir Ahmed Alaaj.
Abdeslam
na Choukri walichukuliwa alama za vidole na polisi wa Ujerumani mnamo
tarehe 5 mwezi Oktoba, mwezi mmoja kabla ya mashambulizi ya
Paris.Choukri pia anashukiwa kuwa Soufiane Kayal ambaye alisimamishwa na
polisi katik mpaka kati ya Austria na Hungary mwezi Septemba wakiwa na
Abdeslam.
Mshukiwa
pekee wa mashambulizi hayo ya kigaidi ya Paris ambaye bado hajakamatwa
ni Mohammed Abrini ambaye alinakiliwa katika kamera za uchunguzi katika
kituo kimoja cha mafuta karibu na mji wa Paris siku mbili kabla ya
kufanyika mashambulizi hayo.
Abdeslam
ambaye ana rekodi ya uhalifu, anaaminika kuwa mshukiwa pekee aliye hai
miongoni mwa timu ya majihadi 10 waliofanya mashambulizi ya kigaidi
Paris wakiulenga ukumbi wa burudani wa Bataclan, mikahawa na uwanja wa
michezo wa Stade de France.
Inasemekana
mshukiwa huyo ambaye ni mzaliwa wa Ufaransa mwenye asili ya Kimorocco
alitorokea Brussels siku moja baada ya mashambulizi hayo, baada ya
kutojiripua na inaaminika tangu mashambulizi hayo, amekuwa katika mji
huo wa Brussels.
Waendesha
mashitika wamesema kikosi maalumu cha usalama kiliisaka nyumba moja
katika mtaa wa Molenbeek kufuatia ushahidi uliopatikana katika
operesheni nyingine iliyofanywa mjini Brussels siku ya Jumanne ambapo
mshukiwa mwingine anayeshusishwa na mashambulizi ya Paris aliuawa na
wengine wawili walitoroka.
Alama za
vidole za Abdelslam ziligundulika katika nyumba hiyo na kupelekea msako
mkubwa wa kumsaka. Vituo vya televisheni vya Ubelgiji vilimuonyesha
Abdeslam aliyekuwa amefunikwa uso kwa kitambaa cheupe akiburutwa na
maaskari kuelekea katika gari la polisi.
Rais wa
Ufaransa amesema kufuatia kukamatwa kwa washukiwa kadhaa nchini Ubelgiji
wanaohusishwa na mashambulizi ya Paris, kuna uwezekano mkubwa kuwa
waliohusika walikuwa wengi kuliko ilivyokuwa inadhaniwa awali. Ubelgiji,
hasa kitongoji cha Molenbeek kimetajwa kuwahifadhi wanajihadi
wanaohusishwa na makundi ya wanamgambo wenye itikadi kali.
Abdeslam,
Abdelhamis Abaaoud ambaye alikuwa mwanachama wa kundi la Dola la
Kiislamu IS na mmoja wa washukiwa wakuu wa mashambulizi ya Paris na
mshambulizi mwingine Bilal Hafdhi wote wanasemekana kuwahi kuishi katika
mtaa huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: