MAWAZIRI WA KIGENI WA IRAN NA RUSSIA WAJADILI KADHIA YA SYRIA

Mawaziri wa kigeni wa Iran na Russia wajadili kadhia ya Syria
Mawaziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia wamefanya mazumgumzo ya simu kuhusu usitishwaji vita nchini Russia.
Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran siku ya Ijumaa alifanya mazungumzo na mwenzake wa Russia Sergei Lavrov. Wawili hao walijadili mchakato wa mazungumzo ya mahasimu nchini Syria pamoja na mapatano ya usitishwaji vita nchini humo. Aidha walizungumza kuhusu misaada ya kibinadamu kutuma Syria na udharura wa kupambana na makundi ya kigaidi.
Zarif na Lavrov aidha walibadilishana mawazo kuhusu udharura wa kuendelea kuwepo mazungumzo ya mara kwa mara baina ya maafisa wa ngazi za juu wa Tehran na Moscow.
Mazungumzo ya kusaka amani yalianza Jumatatu huko Geneva chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. Mazungumzo hayo yameungwa mkono kwa pande zote na Marekani na Russia; nchi ambazo kidhahiri zinaonyesha kufikia makubaliano kuhusu kuhitimisha vita huko Syria. Pamoja na hayo, Bashar al Jaafari, Mkuu wa Ujumbe wa serikali ya Syria katika mazungumzo ya Geneva amesisitiza kuwepo vikwazo viwili vikuu kwenye mazungumzo hayo, ambavyo ni kutokuwepo ajenda ya kazi inayoeleweka na vile vile kutofahamika muundo wa ujumbe wa washiriki wa mazungumzo kwa upande wa wapinzani wa serikali ya Syria katika mazungumzo hayo.

0 comments: