VISA VIPYA VYA EBOLA VYATHIBITISHWA GUINEA CONAKRY

Visa vipya vya Ebola vyathibitishwa Guinea Conakry
Shirika la Afya Duniani WHO limepeleka timu ya wataalamu Kusini mwa mkoa wa Nzérékoré nchini Guinea Conakry baada ya visa vipya viwili vya Ebola kubainika na kuthibitishwa katika maeneo ya kijijini.
Maafisa wa afya wa Guinea walitoa taarifa kwa WHO na wadau wake Machi 16 kwamba kuna vifo vitatu vinavyotatanisha katika wiki za karibuni kwenye kijiji cha Koropara na watu wengine wa familia hizo hivi sasa wana dalili zinazofanana na Ebola.
Wizara ya afya ya Guinea, WHO, kitengo cha Marekani cha kudhibiti magonjwa CDC na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani UNICEF, wamepeleka wachunguzi Machi 17, na vipimo vikachukuliwa kutoka kwa watu wanne, na mama na mwanae wa miaka mitano ambao ni ndugu wa mmoja wa waliokufa wamethibitishwa kuwa na virusi vya Ebola na wamepelekwa kwenye kituo cha tiba.
Visa hivyo vipya vimethibitishwa Ijumaa, siku ambayo WHO imetangaza kumalizika kwa mlipuko wa ugonjwa huo katika nchi jirani ya Sierra Leone. Shirika hilo linaonya kwamba kulipuka upya kwa ugonjwa huo kutarajiwe, na nchi tatu zilizoathirika awali an kwamba ziwe makini na uwezo wa kuzuia, kubaini na kukabiliana na mlipuko.
Ebola imeua zaidi ya watu 11,300 tangu mwezi Desemba 2013 katika mripuko mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa wa ugonjwa huo uliozikumba zaidi nchi tatu za magharibi mwa Afrika za Guinea, Liberia na Sierra Leone. Inaelezwa kuwa, maradhi ya Ebola yamezorotesha pakubwa pia uchumi wa nchi hizo.

0 comments: