SERIKALI YAKIRI DOSARI KATIBA YA TFF


WIZARA ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo imekiri kwamba mchakato wa marekebisho ya Katiba ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF) yaliyofanywa na Mkutano Mkuu wa Dharura Julai 13, una dosari na ndio maana imekwama kwa Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo.  
Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku moja tu tangu Gazeti hili liandike habari ya katiba hiyo kukwama kwa msajili kutokana na marekebisho kupitishwa pasipo kupigiwa kura kama ibara ya 30 (iii) inavyotaka pamoja.
Dosari nyingine ambayo ilielezwa awali iliyomfanya Msajili Mercy Rwezaura kusita kupisha marekebisho hayo, ni kitendo cha TFF kuunfa Kamati za Maadili kabla ya katiba hiyo kupata baraka rasmi za ofisi yake.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu kutokea Jimboni kwake Mvomero, Morogoro, Naibu Waziri Amos Makala, alikiri kuarifiwa jambo hilo na Msajili kuwa  mchakato wa upitishaji marekebisho hayo una dosari kwa mujibu wa katiba.
“Ni kweli nimejulisha na ofisi ya Msajili kuwa kuna dosari, tena tunataka TFF wenyewe wawaeleze ukweli Watanzania  kwa sababu wakati mwingi serikali imekjuwa ikitupiwa lawama kwamba inataka kuharibu mambo,” alisema Makala.
Akifafanua zaidi, Makala alihoji inawezekana vipi marekebisho ya uundwaji wa Kamati za Maaadili kabla ya kupata baraka za Ofisi ya Msajili, wao TFF tayari wameshaunda Kamati husika na kutangaza wajumbe wake.
“Hivi inaingia akilini kweli, ninyi mmefanya mabadiliko ya katiba ili itambue uwezpo wa Kamati za Maadili na mmepeleka kwa Msajili ipate baraka, lakini kabla haijapita, ninyi mnaziunda kamati,” alihoji Makala.
Alipoulizwa juu ya hatma ya uchaguzi mkuu wa Shirikisho hilo ambao umetakiwa uwe umefanyika hadi kufikia Oktoba 30 mwaka huu, Waziri Makala alisema lolote litakalotokea mbelke ya safari, Serikali haipaswi kulaumiwa.
“Kuhusu ukomo wa muda ambao Fifa (Shirikisho la soka la Kimataifa) limetaka kwa kipindi fulani uchaguzi mkuu uwe umefanyika, sisi hilo tunawaachia TFF wenyewe waamue nini cha kufanya, sisi tunaangalia sheria na taratibu za nchi zinasema nini,” alisema.
Utata huo katika marekebisho ya Katiba yaliyofanywa kwa maelekezo ya Fifa, ni mwendelezo wa mchakato wa uchaguzi wa shirikisho hilo kuwa na dosari kwani
awali ulipangwa kufanyika Februari 24, lakini ukasimamishwa.

Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya soka, wanasema pamoja na mapungufu hayo,  katiba hiyo inaweza kupitishwa na Msajili, lakini kabla haijatumika kwenye uchaguzi, itapaswa kupata baraka za Mkutano Mkuu kisha kugongwa mhuri siku hiyo.

0 comments: