UZAZI PASIPO MIPANGO UNAVYOWATESA WANAWAKE KISHAPU.



 Bi. Rejina Moshwa (37) mkazi wa Kijiji cha Isoso akizungumza na mwandishi wa habari kutoka Clouds FM, Aziz Kindamba
Paschal Kulwa Manyinzi (42) mkazi wa Kijiji cha Isoso akiwa katika picha na baadhi ya watoto wake baada ya mazungumzo na Thehabari.com

Na Thehabari.com, Kishapu

WASUKUMA ni moja ya makabila nchini Tanzania ambayo awali yalishikilia desturi ya familia kuwa na idadi kubwa ya watoto. Familia moja yaani baba na mama waliendelea kuzaa kadri walivyo jaaliwa kupata watoto bila kujali ukubwa wa familia. Mume pia hakuwa na kizuizi katika familia cha kuongeza mke mwingine endapo atakuwa na ardhi (mashamba) na mifugo (hasa ng'ombe) ya kutosha kuweza kuihudumia familia aliyonayo.

Wapo walioamini kwamba kuwa na ukubwa wa familia ni kuongeza nguvu kazi katika uzalishaji kwa kutumia ukubwa wa familia. Hata hivyo pia wapo walioamini uzazi ni mpangilio wa Mungu hivyo haupaswi kupangiliwa na wazazi bali mola mwenyewe. Hivyo basi familia za imani hii ziliendelea kuza hadi pale uwezo wa kupata watoto ulipopotea wenyewe au vizuizi vingine.

Hata hivyo sasa hivi mambo yamebadilika kiuchumi, hali ni ngumu hivyo familia nyingi zinapangia idadi ya watoto. Waliojisahau na kuendelea kuzaa idadi kubwa ya watoto pasipo na uwezo kuwamudu wanajuta na kutamani wangelipata uelewa wa elimu hiyo awali.

Hali hii ya majuto ndiyo inayozikuta baadhi ya familia katika vijiji anuai Kata ya Kishapu, mkoani Shinyanga, baada ya kuzungumza na mwandishi wa makala haya. Familia hizi zimejikuta na idadi kubwa ya watoto kiasi cha baba na mama kushindwa kuwapatia mahitaji ya msingi watoto wao hivyo familia kuendelea kuwa na maisha duni kiuchumi.

Bi. Rejina Moshwa (37) mkazi wa Kijiji cha Isoso ni miongoni mwa familia zinazojutia uamuzi wa kuwa na idadi kubwa ya watoto. Anasema familia yao ilikuwa na jumla ya watoto 10, lakini bahati mbaya wawili walifariki dunia hivyo kubakia na watoto nane ambao ni mzigo mkubwa hivi sasa.

"...Hatukuwa na elimu ya kupangilia watoto tulizaa mfululizo kadri ya tulivyo jaaliwa, lakini watoto hawa sasa ni mzigo kwetu, tunajuta. Tumeshindwa kuwasomesha na wamekosa muelekeo...na hata upatikanaji wa chakula cha familia nzima ni tatizo...hasa ukichangia na hivi karibuni ukame uliibuka eneo hili mambo yamezidi kuwa mabaya," anasema Bi. Moshwa.

Paschal Kulwa Manyinzi (42) ni mume wa Bi. Rejina Moshwa, anasema licha ya kuwa na mifugo kidogo yeye ni mkulima wa mazao mchanganyiko yaani Pamba, mtama, karanga na viazi. Anakiri watoto wake mwenyewe kuwa mzigo mkubwa kimalezi kwa sasa. "Wakati tunaanza kuzaa nilifuata mila na desturi za zamani, unajua zamani suala la kuzaa halikuwa la kupangilia, mtu ulikuwa unazaa tuu...suala la kupangilia limeanza juzi.

"Zamani (enzi za wazazi wetu) idadi kubwa ya watoto katika familia ilikuwa ni nguvu kazi...lilikuwa likizaidia katika kilimo...kama mtu ulikuwa hauna familia kubwa ulitapata shida kwenye kilimo. Lakini dunia ya sasa huwezi kuzaa kama mimi ni mzigo," anasema Manyinzi.

Hata hivyo licha ya ukubwa wa familia hii haina ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo kwani heka tano ambazo inadai ilipewa kwa urithi toka kwa wazazi wa Manyinzi imetwaliwa na Serikali kwa ajili ya shughuli za maendeleo na kubaki heka moja. Familia hii inalazimika kukodi ardhi kwa ajili ya kilimo kila msimu wa kilimo.

Modesta Machia (43) ni Mkazi wa Kijiji cha Kishapu, Kata ya Kishapu Wilaya ya Kishapu. Anasema yeye na mumewe wana jumla ya watoto nane walio hai kati ya 10 ambao walibahatika kuwazaa. Anasema watoto wawili walitangulia mbele za haki. Anasema watoto walionao kwa sasa ni mzigo katika malezi.

"...Mwanzoni tulikuwa tunazaa haraka haraka kwa kuwa hatukuwa na uelewa juu ya uzazi wa mpango...lakini laiti ningejua nisingelikubali kupata idadi kubwa ya watoto kama ilivyo sasa...lakini nimepata uelewa nikiwa nimechelewa na nimefunga kizazi kabisa," anasema Bi. Machia. Anasema mume wake kwa sasa ni muhudumu wa usafi katika zahanati ya kijiji chao.

Mwanamama huyu anashauri familia nyingine kuzaa kwa mpangilio na kuzingatia kipato cha familia ili kupunguza umaskini wa kiuchumi katika familia. Anasema mwanamke kuzaa mfululizo hushindwa kuchangia shughuli za kujiongezea kipato katika familia na hata kuchoka mapema kwenye shughuli za uzalishaji mali.

Hata hivyo changamoto nyingine kwa uzazi wa idadi kubwa ya watoto ipo kwa akinamama pekee, kwani inapotokea mke na mume wakatofautiana na kufikia kuachana, idadi kubwa ya kinababa humuachia mke watoto waliozaa na yeye kwenda kuoa sehemu nyingine. 

Bi. Paskazia John mama mwenye watoto nane amekubwa na hali kama hiyo, kwani baada ya kuzaa na mumewe watoto nane walikorofishana na kutengana hivyo mwanaume kumuachia watoto wote nane ambao kwake ni mzigo mara dufu. Anasema unapoolewa katika familia ya kisukuma hasa maeneo ya vijijini kuzaa idadi kubwa ya watoto ni kitu cha kawaida. Anaongeza kuwa na endapo utaonekana mvivu wa kuzaa mwanaume anaweza kukuongezea mke mwenzako ili akusaidie.

Anabainisha kuwa baadhi ya wanaume wa kisukuma wanaamini kwamba kuwa na idadi kubwa ya watoto ni sawa na kuwa na uwezo kiuzalishaji, yaani watoto watatumika kama nguvu kazi shambani. Lakini kwa kuwa kaya nyingi za maeneo ya wasukuma mama (mke) pamoja na watoto huwa ndiyo watendakazi wakubwa mashambani huku baba akibaki kuwa msimamizi na kiongozi wa familia wanawake ndiyo wenyemzigo mkubwa katika familia nyingi za kuangaika na watoto.

Hata hivyo si familia zote zenye mzigo mkubwa wa watoto wanashindwa kuzimudu. Ally Sosoma (60) ni mkulima na mkazi wa Kijiji cha Isoso, katika familia yake ana jumla ya watoto 20 ambao wamepatikana ndani ya wake watatu. Anasema familia yake imeanza kuwa mzigo mkubwa kwake baada ya kuanza ukame mfululizo yaani mwaka 2011 hadi sasa. Anaongeza kuwa hapo nyuma haikuwa mzigo kwa kuwa alikuwa anajituma na ardhi ya kutosha hivyo alizalisha chakula na ziada ya kutosha jambo ambalo haikuwa tabu kuendesha familia yake.

Anasema mila na desturi ya kuwa na idadi kubwa ya watoto ameirithi kutoka kwa baba yake ambaye alikuwa na wake watatu. "...Pamoja kwamba baba alikuwa na wake watatu lakini baba yangu mkubwa alikuwa na wake saba hivyo alikuwa na watoto wengi sana, hivi ndio chanzo cha kuwa na idadi kubwa ya watoto...mimi nilipenda na ndiyo maana nimezaa wengi. Lakini si kweli kwamba watu wanasema ukioa mwanamke wa kisukuma na kutozwa ng'ombe nyingi lazima akuzalie watoto wengi," anasema Sosoma.

Kwa upande wake, Yamesa Sheka mkulima mkazi wa Kishapu; anasema mila na desturi za kuwa na idadi kubwa ya watoto kwa sasa zimepitwa na wakati kutokana na kupanda kwa gharama za maisha. Idadi kubwa ya watoto inachangia umaskini katika familia nyingi kwa kile wazazi kushindwa kuwahudumia watoto. Kijana huyu anawatoto saba kwa sasa lakini anajuta kuwapata kwani ni mzigo kuwalea. "...Ningelipata elimu ya uzazi mapema ningelikomea watoto wanne tu, lakini haikuwa hivyo," anasema Sheka.

Maxmilian Lugembe ni Ofisa Mtendaji Kata ya Kishapu, akizungumzia utaratibu wa familia kuzaa idadi kubwa ya watoto anasema inachangiwa na mfumo dume ambao wameuendekeza familia nyingi za kisukuma. Anasema katika mfumo huo baba ndiye mwenye maamuzi ya kuongeza watoto bila kushauriana na mwenza wake. 

"...Maeneo haya familia kuwa na watoto 10 au 8 ni kitu cha kawaida. Elimu inatolewa ya uzazi wa mpango ambayo anaipata mama pekee lakini kutokana na mfumo dume mama hana uamuzi katika familia hivyo unakuta aisaidii...kwanza wanaume hawataki wake zao kujiusisha na uzazi wa mpango (kutumia dawa kupanga uzazi) na wengine wakifanya kwa siri na kugundulika unakuwa ugomvi mkubwa," anasema Lugembe. 

"Inafikia wakati hata wanawake wanaoonekana kupanga uzazi katika ndoa zao wanaaminika kuwa ni wahunu, yaani wanataka kupumzika kuzaa ili wapate nafasi ya kufanya maovu (uhuni) nje ya ndoa. Wapo wanaoamini kuwa ishara ya kumpenda mwanaume ni kumzalia watoto...unazaa uwezavyo hadi uchoke," anasema.

0 comments: