PUTO LA KUPUNGUZA UZITO LINAVYOPUNGUZA MAJONJWA YASIYOAMBUKIZA

MAGONJWA yasiyoambukiza (NCDs) ni yasiyoenea kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.

Hivi sasa NCDs imekuwa mzigo kwa taifa kutokana na kutumia gharama kubwa ya matibabu kwa muda mrefu na kupoteza nguvu kazi.

Wizara ya Afya imesema unene uliokithiri na uzito kupita kiasi ni kisababishi cha magonjwa yasiyoambukiza kwa asilimia 73 ya magonjwa hayo.

Imetaja vichocheo vingine ni changamoto za lishe zinazosababisha magonjwa hayo kwa asilimia 32 na matumizi ya tumbaku kwa asilimia 14.8.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2016, zinaonesha kuwa vifo milioni 42 sawa na asilimia 71 vilivyotokea duniani vilitokana na magonjwa hayo na asilimia 25 ya vifo hivyo viliwahusu wenye umri wa miaka 30 hadi 70.

Mkurugenzi wa Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Dk James Kiologwe, anasema mzigo wa magonjwa umeongezeka nchini na vihatarishi vimeongezeka kwa kasi hivyo wanatakiwa kuangalia nini cha kufanya kudhibiti.

“Sasa watu wanaofanya ngono isiyo salama ni wachache kuliko wenye uzito kupindukia, mzigo unaongezeka, theluthi mbili hawajifahamu, wengine wanafika hospitali wakiwa na madhara zaidi,” anasema Dk Kiologwe.

Anasema tafiti zinaonesha kuwa kwa miaka 10 visababishi vimeongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza kuliko yanayoambukiza.

Dk Kiologwe anasema vihatarishi vinavyosababishwa na lishe isiyo sahihi ni asilimia 18 na vya matumizi ya pombe ni asilimia 15.9.

“Tumeona kuna haja ya kupata elimu kwa magonjwa yasiyoambukiza, tumeamua kutumia mhimili wa habari ili kutoa elimu sahihi na katika mapambano haya tunakinzana na changamoto za kibiashara na viwanda ambazo nao ni muhimu kupata elimu sahihi,” anasema Dk Kiologwe.

Anasema wanatengeneza timu kwa kila mkoa ili kutoa elimu ya magonjwa yasiyoambukiza na wanatarajia kuandaa tuzo kwa wanaoandika habari zinazohusu magonjwa hayo.

Anasema tabia bwete, ulaji usiofaa na kutokufanya mazoezi ni vyanzo vikubwa vya magonjwa hayo.

HUDUMA YA KUPUNGUZA UZITO YATOLEWA

Katika kudhibiti magonjwa hayo, kwa mara ya kwanza nchini, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila jijini Dar es Salaam imeanza kutoa huduma ya kupunguza uzito uliokithiri kwa kuweka puto tumboni.

Hadi sasa watu 26 wenye uzito zaidi ya kilogramu 100 wamepata huduma hiyo inayogharimu Sh milioni 3.5 hadi milioni nne.

Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Mohammed Janabi anasema hawatoi huduma hiyo kwa sababu ya urembo bali wanalenga kusaidia watu.

“Hii ni operesheni yetu ya tatu leo na leo (Desemba 21, 2022) tumewafanyia watu wawili wote ni kilogramu 100 kwenda juu wa kwanza kilo 160 na wengine kilo 105, hawajafanya kwa sababu ya urembo. Wiki moja iliyopita tulifungua kliniki ya mafuta tunawakaribisha hospitali zingine zilete wagonjwa kupata huduma,” anasisitiza Profesa Janabi.

JINSI UNAVYOFANYIKA

Profesa Janabi anasema utoaji huduma hiyo utahusisha uingizaji wa mrija wa puto kupitia mdomo hali itakayopunguza kiwango cha chakula kwa mhusika.

“Tutaweka kwa miezi nane, tutaingiza kupitia mdomo hadi kwenye tumbo, hakuna upasuaji tunatumia mitambo ifike mahali pake tunajaza dawa, linapunguza ukubwa wa tumbo ukila kidogo utashiba hivyo tunategemea uzito utapungua.”

HUKINGA NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA

Profesa Janabi anaeleza kuwa faida kubwa ni kusaidia kinga dhidi ya magonjwa ya kisukari, kiharusi, moyo na kushindwa kupumua.

Anabainisha kuwa matibabu yatakayotolewa ni siri ya mgonjwa ambapo pia matibabu hayo huchukua siku mbili tu.

“Siku ya kwanza unaweza kusikia kama una vidonda vya tumbo lakini baada ya muda utaendelea kawaida, hospitali hatukaribishi watu lakini tunawaomba wale wenye uzito mkubwa wafike kliniki tuna kliniki ya siku mbili hapa Mloganzila na siku mbili Muhimbili-Upanga,” anasisitiza.

Pamoja na hayo anasema pindi mgonjwa anapopatiwa huduma hiyo na kupungua atapata usaidizi wa mtaalamu wa lishe ili asiongeze tena kiwango cha kula na uzito kuongezeka tena.

“Kabla ya kumhudumia tutapima vitu vingine vyote ndio upate huduma, faida kubwa ni kitu ambacho baada ya miezi nane tutatoa na hali ya kula kidogo itaendelea na akirudi tabia ya mwanzo anaweza kuwekewa mara nyingine hivyo ni vyema kuweka kiasi.

“Na matatizo mengine ni ya kurithi ukiwa na mtoto ana uzito mkubwa mlete wakati mwingine unaweza kukuta mtoto amezaliwa na kilo nne watu wakaona ni kitu sahihi kumbe si kweli,” anasema Profesa Janabi.

Anasema gharama ya huduma hiyo nje ya nchi inategemea na nchi; India ni Sh milioni 15 hadi 20 na Ulaya ni Sh milioni 30 kwenda juu lakini nchini ni Sh milioni 3.5 hadi Sh milioni nne.

“Hii ni sehemu ya utalii tiba hivyo nchi za jirani tunatoa huduma hizi waje kupata huduma, ni tiba salama kama tunavyopandikiza figo, uloto na zingine wakitaka kupata huduma hapa ni rahisi,” anaeleza Profesa Janabi.

UZITO HUPUNGUA HARAKA

 Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji, Erick Kimaro anasema wanatarajia mtu kupungua kilogramu 30 na kuendelea kwa muda wa miezi nane.

Dk Kimaro anasema kama baluni ikipasuka katika baluni wameweka maji dawa hivyo maji yataonekana kwenye haja na itatolewa na kuwekwa nyingine.

“Tutapima magonjwa mengine mfano wenye shinikizo la damu tukipunguza uzito itawasaidia hivyo ni sehemu ya tiba.

WAJIPANGA KUTOA HUDUMA

Naibu Mkurugenzi wa Mloganzila, Dk Julieth Magandi anasema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa wakati.

“Huduma hii inahusika na kuweka puto tumboni bila upasuaji kwa wagonjwa ambao wana uzito uliopitiliza kiwango kinachotakiwa na tumejipanga kuanzisha huduma hii katika mifumo miwili; wa kwanza tumeanzisha kliniki maalumu wagonjwa wote lazima wapime kiwango cha mafuta katika damu na kwa wale ambao wanataka kupunguza uzito wataonana na timu ya wataalamu kuhudumiwa,” anaeleza Dk Magandi.

Anasema mgonjwa anapofika moja kwa moja anapelekwa chumba maalumu na wataalamu wote wanaotakiwa watamwona na huduma atapewa akiwa sehemu moja.

Aidha, anabainisha kuwa tangu wameanza mwitikio umekuwa mkubwa na kusababisha kuanzisha kambi maalumu.

“Tukumbuke watu walikuwa wanasafiri kwenda nje lakini sasa huduma ipo ndani, wataalamu wapo wakutosha na vifaa vipo mgonjwa akija asubuhi jioni anatoka,” anasema.

UTALII WA MATIBABU

Mjumbe wa Medical Tourism Taifa, Abdulmalick Mollel, anaeleza kuwa wamekuwa wakirekodi vipande vya video na kutafsiri kwa lugha mbalimbali ili kutangaza huduma hiyo.

“Kwanza madaktari bingwa tayari tulishakaa nao na kuangalia maswali yanayohitaji katika jamii, wanapokuwa wamehojiwa tunakata vipande na kutafsiri kwa lugha mbalimbali na kutangaza huduma zinazopatikana na tumeshafanya hivyo na madaktari wapo wanajibu maswali kuhusu huduma hiyo.

“Na watu wanapigiwa simu kuelimishwa na pia hata baada ya kupata huduma wanatafutwa kujua hali zao zinaendeleaje,” anasema Mollel.

Daktari Bingwa wa Upasuaji, Kimaro alisema watu kutoka nchi mbalimbali wamekuwa wakitafuta huduma hiyo huku wengine tayari wameshafika kuipata.

“Nimepokea simu kutoka nchi mbalimbali kupata huduma za baluni kutoka Congo (DRC) wanataka huduma na Kenya na mwingine wa Syria amewekewa, tumepata simu nyingi na watu wanatafuta huduma na leo (Januari 20, mwaka huu) tunawafanyia watu sita,” anaeleza Dk Kimaro.

0 comments:

DKT. MWINYI AONGOZA MATEMBEZI YA UHAMASIOSHAJI UPIMAJI WA MOYO NA KUFANYA MAZOEZI


 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwasalimia na wananchi wa mitaa ya Muembemimba akiwa katika Matembezi ya Kuhamasisha Ufanyaji wa Mazoezi  “Tembea na JKCI Linda Afya ya Moyo Wako” na Kufunga Kambi ya Upimaji wa Moyo iliyofanyika katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Unguja Jijini Zanzibar kuazia 23 - 27, Januari 2023. Matembezi hayo yalianzia  katika viwanja vya Maisra Suleiman na kumalizikia katika Uwanja wa Amaan Unguja leo 28-1-2023. Kushoto kwa  Rais ni  Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akishiriki katika Matembezi ya Kuhamasisha Ufanyaji wa Mazoezi  “Tembea na JKCI Linda Afya ya Moyo Wako” na Kufunga Kambi ya Upimaji wa Moyo iliyofanyika katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Unguja kuazia 23-27, Januari 2023, matembezi hayo yaliyoanzia katika viwanja vya Maisara Suleiman na kumalizikia katika Uwanja wa Amaan Unguja leo 28-1-2023  (kushoto kwa Rais) ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Peter Kisenge, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hassan K.Hafidh na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said na (kulia kwa Rais) Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Idrissa Mustafa Kitwana.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Hussein Ali Mwinyi, akishiriki katika mazoezi ya viungo yakiongozwa na Kocha Mkuu wa Mazoezi ya Viungo Zoni D. Ndg. Ahmad Rajab, baada ya kumalizika kwa Matembezi ya Kuhamasisha Upimaji wa Moyo na kufanya mazoezi  “Tembea na JKCI Linda Afya ya Moyo Wako” yaliyoanzia katika viwanja vya Maisara Suleiman na kumalizikia katika Uwanja wa Amaan Unguja na(kulia kwa Rais) ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla na Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui na (kushoto kwa Rais) Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  Dkt.Peter Kisenge.

Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakishiriki katika mazoezi ya viungo baada ya kumalizika kwa Matembezi ya Kuhamasisha Upimaji wa Moyo na kufanya mazoezi  “Tembea na JKCI Linda Afya ya Moyo Wako” yaliyoanzia katika viwanja vya Maisara Suleiman na kumalizikia katika Uwanja wa Amaan Unguja. Matembezi hayo yaliongozwa na RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Hussein Ali Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia baada ya kumalizika kwa Matembezi ya Kuhamasisha Upimaji wa Moyo na ufanyaji wa Mazoezi “Tembea na JKCI Linda Afya ya Moyo Wako” na kufunga Kambi ya Upimaji wa Moyo, iliyofanyika katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Unguja Jijini Zanzibar 23-27,Januri 2023, matembezi hayo yalimalizika katika Uwanja wa Amaan Unguja.

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza baada ya kumalizika kwa Matembembezi ya Kuhamasisha Upimaji wa Moyo na kufanya mazoezi  “Tembea na JKCI Linda Afya ya Moyo Wako” na ufungaji wa Kambi ya Upimaji wa Moyo iliyofanyika katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja iliyoaza 23-27,Januari 2023, ufungaji huo uliyofanyika katika uwanja wa Amaan Unguja Jijini Zanzibar. 

WAZIRI wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmin Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Hussein Ali Mwinyi, kuzungumza na Wananchi, baada ya kumalizika kwa Matembezi ya Kuhamasisha Upimaji wa Moyo na kufanya mazoezi “Tembea na JKCI Linda Afya ya Moyo Wako” na ufungaji wa Kambi ya Upimaji wa Moyo iliyofanyika katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Unguja Jijini Zanzibar, iliyoaza 23-27,Januari 2023, matembezi hayo yaliyomalizikia katika uwanja wa Amaan Unguja.

**********************************************************************************************************************************************************************************

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi kubadili mfumo wa maisha kwa kufanya mazoezi ili kujikinga na magonjwa mbalimbali yasioambukiza ukiwemo ugonjwa wa moyo.

Alisema hatua hiyo imethibitishwa na wataalamu wa afya kupitia utafiti walioufanya unaoonesha moja ya hatua muhimu ya kukabiliana na magonjwa hayo ni kufanya mazoezi.

“Nawasihi nyote muendelee kushiriki kwenye kambi mbalimbali za upimaji wa magonjwa na matembezi kama haya, kwani ni muhimu kwa afya zenu, kila mtu huko anakoishi atambue kufanya mazoezi ni kinga muhimu katika kuepuka magonjwa mengi hasa yasio ambukiza, kwa hiyo sote tuhimizane tujenge utamaduni wa kufanya mazoezi na kupima afya zetu mara kwa mara ili kubaini mapema kama tuna matatizo ya kiafya, kuchukue hatua za matibabu” Alishauri Dk. Mwinyi.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo viwanja vya Amani, Zanzibar alipofunga kambi ya upimaji na matibabu ya moyo na kampeni ya kufanya mazoezi yenye kauli mbiu “Tembea JKCI, Linda Afya ya Moyo Wako”.

Alisema taifa linatumia pesa nyingi za kigeni kugharamia matibabu ya moyo na magonjwa mengine nje ya nchi. Hivyo aliipongeza taasisi ya JKCI kwa kubunifu mikakati mbali mbali ya kinga na tiba ya maradhi ya moyo nchini.

Aidha, aliishukuru taasisi hiyo kwa kuwajengea uwezo watumishi wa afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuwasihi kuendeleza utamaduni huko kwa watumishi wa Pemba.

“Nawasihi JKCI mfike na Pemba kwa ajili ya uchunguzi na kuhamasisha ufanyaji wa mazoezi kama njia bora ya kuimarisha afya, bila ya shaka wananchi wa Pemba nao wanahitaji huduma zenu na elimu hii kama mlivyofanya hapa Unguja” Alishauri Dk. Mwinyi.

Katika hatua nyengine Rais Dk. Mwinyi aliitaka  taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kuongeza huduma zao kwenye maeneo mbalimbali ya nchi na kueleza kuwa kuwepo kwao kutasaidia kupambana na matatizo mbali mbali ya afya ambayo jamii wanakabiliana nayo.

Alieleza hatua hiyo itasaidia kuongeza uwezo na wataalamu watakao wahudumia vizuri wananchi na kupunguza madhara ya magonjwa haya ambayo yanaongezeka kila siku.

Alisema tokea kuanzishwa kwa taasisi hiyo, mwaka 2015 tayari imesaidia wagonjwa wengi wakiwemo waliotibiwa kwa dawa na waliofanyiwa upasuaji na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa, hivyo aliitaka taasisi hiyo kuimarisha utendaji wao na kuongeza tija kwa watu wengi kunufaika na huduma zao.

“Nafahamu kuwa taasisi hii imekuwa na utendaji mzuri sana tokea ilipoanzishwa. Hata hivyo, bado kuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi ili kuyafikia malengo ambayo Tanzania tumejiwekea, katika kuimarisha afya za wananchi kwa kutoa huduma bora na zenye kiwango cha kimataifa”. Alieleza.

Akizungumza kwenya hafla hiyo, Waziri wa Afya, Nassor Mazurui alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar watashirikiana na taasisi ya JKCI, kuongeza wataalam wa matatizo ya moyo Zanzibar kutokana na uhaba wa wataalamu hao ambapo alieleza kwasasa wapo wawili tuu.

Alisema alisema Zanzibar kwa sasa ina madaktari bingwa wawili tuu wanaoshughulikia matatizo ya moyo.

0 comments:

CRISTIANO RONALDO: FOWADI WA URENO AANZA KWA USHINDI

  Cristiano Ronaldo alicheza mechi yake ya kwanza ya katika klabu mpya ya Al Nassr katika ushindi wao wa 1-0 dhidi ya Ettifaq kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Saudia siku ya Jumapili.


Mshambulizi huyo wa Ureno mwenye umri wa miaka 37 alijiunga na klabu hiyo mwezi uliopita kwa mkataba utakaodumu hadi 2025, akiripotiwa kulipwa zaidi ya £177m kwa mwaka.


Aliongoza safu ya mashambulizi na kucheza mchezo mzima ambao kiungo wa Brazil Talisca alifunga bao la ushindi.


Al Nassr wako kileleni mwa ligi ya Saudia, pointi moja juu ya Al Hilal iliyo nafasi ya pili.


Ronaldo - ambaye aliwahi kuzichezea Manchester United, Juventus na Real Madrid - alilakiwa na mabango na shangwe kutoka kwa mashabiki wake wapenzi kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha King Saud mjini Riyadh.


Haya yanajiri baada ya kufunga mabao mawili akiichezea Riyadh All Star XI katika mechi walioshindwa kwa idadi ya magoli 5-4 dhidi ya timu ya Lionel Messi ya Paris St-Germain kwenye mechi ya kirafiki manmo Alhamisi.

0 comments:

MWANAMKE WA KWANZA PALESTINA ATAWAZWA KUWA MCHUNGAJI

    Katika maeneo mengi ya kikristo duniani, kuwa na viongozi wa kike wa kanisani si jambo geni tena. Lakini mpaka sasa, Nchi Takatifu - ambapo matukio mengi katika Biblia yamewekwa - ilikuwa haijawahi kutokea mwanamke kutoka ndani ya nchi hiyo kuwa kiongozi wa dini.


Siku ya Jumapili, ilikuwa sherehe ya raia wa Palestina kutoka Jerusalem, Sally Azar, kuwa mchungaji mwanamke wa kwanza katika kanisa la Kilutheri katikati ya Mji Mkongwe, iliyohudhuriwa na mamia ya watu kutoka mataifa mbalimbali.


"Nilifurahishwa zaidi kuona msisimko wa watu wengine," Mchungaji Azar alisema. "Ni hisia isiyoelezeka kuchukua hatua hii kwa kuungwa mkono na kanisa."


"Nina matumaini kwamba wasichana na wanawake wengi watajua kuwa jambo hili linawezekana na hata wanawake wengine kutoka kwenye makanisa mengine watajiunga nasi. Najua itachukua muda mrefu, lakini nadhani itafurahisha zaidi ikiwa hii hali itabadilika nchini Palestina.


" Wakristo ni wachache katika maeneo ya Palestina, Israel na Jordan. Wakristo wengi hapa ni wa Kanisa la Orthodox la Ugiriki na kuna Makanisa ya kikatoliki ya Latini, ambayo hayaruhusu mapadre wanawake.


Hata hivyo, idadi ya wanawake wanaowekwa wakfu katika Makanisa ya Kiprotestanti inaongezeka katika miongo michache iliyopita. Na hii inawapa fursa ya kuwa viongozi wa shule na hospitali katika ardhi takatifu.

0 comments:

MAMIA WAJITOKEZA KUMZIKA MWANDISHI WA HABARI RWANDA

    Mamia ya watu walishiriki katika mazishi ya mwandishi wa habari John William aliyefariki katika ajali ya gari, huku mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yakitaka uchunguzi huru kuhusu kifo chake.


Wanahabari wengi nchini humo, marafiki, na wanafamilia walishiriki katika mazishi haya siku ya Jumapili, huku kukiwa hakuna mengi yaliyosemwa kuhusu kazi ya marehemu au jinsi kifo chake kilivyotokea.


Frank Habineza kutoka chama cha upinzani cha Democratic Green Party of Rwanda, Victoire Ingabire na Bernard Ntaganda ni miongoni mwa wanasiasa waliohudhuria mazishi hayo.


"Hatutasahau mchango wako wa thamani katika kukuza uhuru wa vyombo vya habari katika mazingira yenye changamoto", Bi Ingabire alisema kuhusu kifo cha Bw Ntwali.


Polisi walisema Bw Ntwali alifariki papo hapo kwenye ajali ya barabarani siku ya Jumanne usiku wakati bodaboda aliyokuwa amepanda ilipogongwa na gari, dereva akakamatwa, polisi waliongeza.


Lakini Human Rights Watch ilisema kwamba "kuna sababu nyingi za kutilia shaka" maelezo ya polisi na kutaka "utaalamu wa kimataifa kubaini kama aliuawa au la."

0 comments:

TUNDURU KUANZA MSAKO WA WANAFUNZI NA WAZAZI WENYE WATOTO WASIORIPOTI SHULE

 Na Mwandishi wetu, Tunduru


SERIKALI Wilayani Tunduru,imetangaza msako mkali kwa wazazi na walezi wenye watoto ambao wamechaguliwa kuanza kidato cha kwanza kwa muhula wa masomo 2023 lakini hadi sasa bado hawajaripoti kwenye shule walizopangiwa.

Pia msako huo,utawahusu wazazi na watoto wenye umri na sifa ya kuanza elimu ya awali na msingi na waliokatisha masomo bila sababu za msingi na hivyo kusababisha kuongezeka kwa watoto wanaodhurura ovyo mitaani.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius,amesema hayo jana wakati akizungumza na Gazeti hili kuhusiana na hali ya mahudhurio kwa wanafunzi waliochaguliwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza na elimu ya msingi mwaka 2023 katika shule mbalimbali wilayani humo.

“tutatumia week end hii(mwisho wa juma)kuwatafuta wazazi ambao bado hawajapeleka watoto wao shule ili watueleze kwanini watoto wao wako nyumbani,tutatumia sheria kuwafikisha mahakamani wazazi wasiopeleka watoto wao shule,hii nchi inaendeshwa kwa mujibu wa sheria,hivyo ni lazima tutumie sheria zilizopo”alisema Mtatiro.

Alisema wilaya ya Tunduru ni wilaya yenye mwamko mdogo wa elimu,hata hivyo kama viongozi waliopewa dhamana wataendelea kuhamasisha wazazi na jamii umuhimu wa kupeleka watoto shule ili kupata haki yao ya msingi.

Mtatiro ametoa wiki moja kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanapeleka watoto shule na baada ya muda huo kupita serikali haitakuwa na huruma na mzazi au mlezi ambaye atabaki na mtoto wake nyumbani bila sababu za msingi na atafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Aidha,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na serikali yake ya awamu ya sita kwa kuipatia wilaya hiyo fedha za kutosha ambazo zimewezesha kujenga na kuboresha miundombinu ya elimu ambayo imesaidia sana wanafunzi kuwa na sehemu nzuri ya kujifunzia na walimu kufundishia.

Amewaagiza viongozi wa ngazi za vijiji,kata na Halmashauri kuwafuatilia watoto wote ambao hawajaanza kwenda shule na kuwataka wazazi kutoa ushirikiano kwa serikali iliyoonyesha dhamira ya dhati ya kuwajali wananchi kwa kujenga vyumba vingi vya madarasa.

Baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo wamesema,kusua sua kupeleka watoto shule linatokana na hali ya kiuchumi kwani licha y serikali kuruhusu walimu kupokea wanafunzi bila ya kuwa na sale, ni vyema watoto kuwa na mahitaji yote muhimu.

Ali Sadala alisema, siyo kwamba wazazi hawapendi kupeleka watoto wao shule,isipokuwa changamoto za maisha zinachangia sana watoto kutokwenda shule kwa wakati.
  MMkuu wa wilaya ya Tunduru Wakili Julius Mtatiro akizungumzia kuhusiana na mahudhurio ya wanafunzi waliochaguliwa kuanza elimu ya sekondari kwa mwaka wa masomo 2023.

0 comments:

KMC FC YAREJEA NYUMBANI KUWAVAA NAMUNGO

 Kikosi cha Timu ya KMC FC kesho kitashuka katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam kikiwakaribisha Namungo ya Ruangwa Mkoani Lindi katika mchezo utakaopigwa saa 16 00 jioni.


Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni chini ya kocha Mkuu Thierry Hitimana itakuwa nyumbani kwenye mchezo huo ikiwa ni mara baada ya kupita takribani mwezi mmoja KMC FC kucheza kwenye uwanja huo na kuibuka na ushindi wa magoli mawili kwa sifuri dhidi ya Polisi Tanzania uliochezwa Disemba 22 mwaka jana.

Kikosi hicho cha wana Kino Boys kimeshajiandaa kikamilifu kuwakabili Namungo licha ya kuwa ni mchezo wenye ushindani na kwamba kama Manispaa ya Kinondoni imejipanga kutumia vizuri uwanja wa nyumbani.

"Tunakwenda kwenye mchezo mgumu lakini tunakila sababu ya kuhakikisha kwamba Timu inapata matokeo mazuri kutokana na ushindani uliopo kwasasa huku ukizingatia Msimu wa Ligi Kuu ya NBC 2022/ 2023 unakwenda ukingoni.

"Tunapokwenda kwenye mchezo wa kesho pamoja na kwamba tupo nyumbani lakini tutaingia tukiwaheshimu wapinzani wetu kutokana na kwamba wanakikosi kizuri na benchi lao la ufundi pia ni zuri, lakini KMC FC inawachezaji bora zaidi ambao siku zote wamekuwa wakiipa thamani kwakuipambania Manispaa ya Kinondoni ili kupata matokeo chanya.

Kwa upande wa Afya za wachezaji, wote wako vizuri wana hari na morali huku tukiwa na ufahamu kuwa mashabiki zetu wamekuwa na shauku ya kuona burudani kwenye uwanja wa Uhuru na hivyo tumejiandaa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kwenye mchezo huo wanaondoka na furaha.

KMC FC itawakosa wachezaji wawili muhimu kutokana na kusumbuliwa na majeraha ambao ni Awesu Ally Awesu pamoja na Hance Masoud Msonga huku wachezaji wengine wakiwa tayari kwa mtanange huo.

KMC FC inawaomba mashabiki zake kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa kesho ili kuishuhudia Timu yao ikipambana kuwapa burudani na hivyo kusonga mbele kwa kuvuna alama tatu muhimu na kuendelea kujiweka vizuri katika msimamo wa Ligi ambapo ipo kwenye nafasi 10 huku ikiwa imecheza jumla ya michezo 20 na kukusanya alama 23.

0 comments:

WASHTAKIWA NANE WAKIWEMO ASKARI WAWILI JWTZ WANAODAIWA KUKUTWA NA KOBE 116 BILA VIBALI WASOMEWA MASHARTI YA DHAMANA

 MAHAKAMA  ya Hakimu Mkazi Kisutu imewasomea masharti ya dhamana washtakiwa nane wakiwemo mwanajeshi kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), wanaodaiwa kukutwa na nyara za serikali ambazo ni Kobe 116 bila ya kuwa na kibali.



Hata hivyo, washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi, wamesomewa masharti ya dhamana bila ya wao kuwepo mahakamani kutokana na changamoto za usafiri kutoka gerezani.

Akisoma masharti hayo Hakimu Mkazi Mkuu,  Rhoda Ngimilanga amewataka washtakiwa kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wanaoishi Dar es Salaam, wenye barua na vitambulisho vya Nida na watakaosaini bondi ya sh. Milioni tano. 


Washtakiwa katika kesi hiyo ni, mfanyabiashara Josephat Moyo (52) mkazi wa Tabata, Deogratius Lugeng'a (40),  MT 88046 Sajenti Cosmas Ndomba kutoka JWTZ na  Mfanyabiashara Hamza Abdalah ( (52).


Wengine ni MT 118102 Kassim Abdalah (35), Nkanamuli Ngaza (52)  mlinzi kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na wakukima wawili Kutoka mkoa wa Dodoma ambao ni  Stephano Chedego (51) na Mwaluko Mgomole.


 Wote kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya uhujumu Uchumi yenye mashitaka matatu likiwemo la kuongoza genge la uhalifu na kujihusisha na nyara za serikali ambazo ni kobe 116 bila kibali.


Inadaiwa, kati ya Januari mwaka hadi Julai 3 mwaka 2022 ,Dar es Salaam, washtakiwa hao waliendesha genge la uhalifu kwa kununua, kukusanya, kusafirisha, na kuuza nyara za Serikali ambazo ni Kobe 116  wenye thamani ya USD  8120 sawa na sh
 18,935,840.


Katika shitaka la pili imedaiwa, katika tarehe isiyojulikana mkoani  Dar es Salaam, washtakiwa  kwa pamoja walijihusisha na nyara hizo za serikali kwa kununua na kuziuza bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.


Pia,  Julai 3 mwaka 2022 katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, washitakiwa hao walikutwa na kobe hao bila kuwa na kibali.


Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 30, 2023 washtakiwa watakapoletwa mahakamani kwa ajali ya kuangalia kama upelelezi umekamilika na kudhaminiwa iwapo watakuwa wametimiza masharti ya dhamana.

0 comments:

NMB YATOA MSAADA WA VIFAA TIBA VYA SH. MIL 26 WILAYA YA ARUSHA

Sekta ya afya ni sekta muhimu kwa maendeleo ya jamii zetu na kwa kulitambua hilio, Benki ya NMB imeshirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya kusaidia kuboresha huduma za Afya kwa Wilaya ya Arusha kwa kutoa msaada wa vifaa tiba vyenye jumla ya thamani ya zaidi ya sh. 26,000,000 katika kituo vya Afya - Mkonoo ambavyo ni;


✅ Vitanda 10 vya kujifungulia kwa kina mama

✅ Vitanda 10 vya kulazia wagonjwa wa kawaida


Huku, kwa Kituo cha Afya Levolosi waliwakabidhi mabenchi 20 ya kusubiri huduma na kukalia kwa wasindikizaji.

Kabla ya kukabidhi vifaa hivyo, Afisa Mkuu wa Huduma Shirikishi wa NMB, Nenyuata Mejooli alisema kuwa vifaa hivyo ni moja ya ushiriki wetu katika maendeleo ya jamii na wao kama benki inayoongoza Tanzania, wanao wajibu wa kuhakikisha jamii inayowazunguka inafaidika kutokana na faida wanayoipata.

Lakini pia, aliongezea kuwa Benki ya NMB imekuwa ikipokea maombi mengi sana ya kuchangia katika miradi ya jamii, lakini benki imejikita zaidi katika maeneo ya elimu, afya, na misaada ya hali na mali katika nyakati ngumu kama za majanga na tumekuwa mstari wa mbele kuchangia huduma za kijamii kwa lengo la kurejesha sehemu ya faida yetu kwa jamii.

kwa zaidi ya miaka kumi mfululizo, Benki ya NMB imekuwa ikitenga asilimia 1℅ ya faida yake kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii inayoizunguka.



0 comments:

TANZANIA COMMERCIAL BANK YASHIRIKI UZINDUZI UJENZI WA RELI YA KISASA KUTOKA TABORA HADI ISAKA

   Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Phillip Mpango akisikiliza maelezo ya ushiriki wa benki ya Tanzania Commercial Bank TCB katika ujenzi wa Reli ya kisasa(SGR) kutoka kwa Mkurugenzi wa wateja Wakubwa wa Tanzania Commercial Bank (TCB),  Adolphina William wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa ujenzi wa reli ya SGR LOT 4 kati ya Tabora na Isaka, uliofanyika leo mjini Isaka, mkoani Shinyanga
  Mkurugenzi wa wateja Wakubwa wa Tanzania Commercial Bank (TCB),  Adolphina William wakati (kulia), akizungumza wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa ujenzi wa reli ya SGR LOT 4 kati ya Tabora na Isaka, uliofanyika leo mjini Isaka, mkoani Shinyanga ambapo katika hafla hiyo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Phillip Mpango.
  Tanzania Commercial Bank (TCB) Imeendelea kushiriki zoezi endelevu la ujenzi wa kipande cha nne cha ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Tabora hadi Isaka chenye urefu wa kilomita 165.
TCB imeshirikia kikamilifu katika hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha kutoka Tabora hadi Isaka chenye urefu wa kilomita 165..

TCB imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo katika sekta mbalimbali na kuhakikisha kuwa inatoa huduma stahiki kila kona ya Tanzania na kuhakikisha inaunga mkono kwa asilimia zote maendeleo ya nchi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa wateja wakubwa wa  Tanzania Commercial Bank Adolphina William  wakati wa uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa reli ya Kisasa (SGR) awamu ya nne leo Mkoani Shinyanga

Adolphina amesema, Tanzania Commercial Bank  ni Benki ya Wananchi na  wamejitoa na wameshiriki kwa hatua kubwa katika kuhakikisha shirika la Reli Tanzania (TRC) linafanikisha mradi wa SGR   kwa mafanikio makubwa.

“Tanzania commercial Bank ni wadau wakubwa wa maendeleo hapa nchini na kuchangia ujenzi wa Taifa, TRC wanafanya kazi nzuri sana kuhakikisha wanaunganisha wananchi kwa njia ya usafiri wa reli hivyo mradi huu wa SGR utaleta mafanikio makubwa hapa nchini.

Adolphina ameeleza kuwa kwa Sasa Tanzania Commercial Bank ina matawi kila pembe ya Tanzania hivyo imejipanga vyema kutoa huduma kwa watanzania pamoja na wageni kutoka nje hivyo amewasihi watanzania ambao bado hawajafungua akaunti na benki ya TCB wakafungue akaunti ili kunufaika na huduma zinazopatikana katika Benki hiyo.

0 comments:

MAKALA YA MAKUMBUSHO YA TAIFA YA MAJIMAJI INAVYOWEZA KUKUZA UTAMADUNI RUVUMA

 Makumbusho ya Taifa ya Majimaji kukuza utalii wa kiutamaduni Utalii wa kiutamaduni hapa nchini bado haujapewa kipaumbele ukilinganisha na nchi nyingine kama Afrika ya kusini ambayo utalii huo umepiga hatua kubwa.


Mkoa wa Ruvuma una utajiri mkubwa wa utalii wa utamaduni ukilinganisha utalii wa ikolojia,miongoni mwa vivutio vya utalii wa utamaduni ni Makumbusho ya Taifa ya Majimaji yaliopo katika eneo la Mahenge Manispaa ya Songea.

Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anabainisha kuwa,wadau wa utalii katika Mkoa wa Ruvuma wamekusudia kuanzisha na kukuza utalii wa kiutamaduni (cultural tourism) sanjari na kuboresha maeneo yote ya kihistoria ili kuendeleza utamaduni hatimaye maeneo hayo yaweze kuingiza mapato baada ya watalii kutembelea kama ilivyo katika visiwa vya Zanzibar.

Challe anasema,wadau wa utalii mkoani Ruvuma tayari wameshatembelea maeneo muhimu ya kihistoria kama vile Makumbusho ya Taifa ya Majimaji,Makumbusho ya Rashid Kawawa,Maposeni,Luhira,Peramiho na Chandamali katika Wilaya ya Songea ili kutambua maeneo ya kihistoria na umuhimu wake kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Huu ni mwanzo wa jukumu la kuziboresha kumbukumbu za kihistoria katika mkoa wa Ruvuma na kuimarisha utalii wa ndani na nje lengo likiwa ni kuutangaza mkoa wa Ruvuma’’,anasisitiza Challe.

Kwa upande wake Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Bartazar Nyamusya anasema serikali imedhamiria kuyafanya Makumbusho ya Taifa ya mashujaa wa vita ya Majimaji kuwa makumbusho ya mfano Tanzania kutokana na makumbusho hayo kuhifadhi vifaa halisi na silaha halisi ambazo walitumia
mashujaa hao kupambana na wakoloni wa kijerumani.

“Hii ni Makumbusho pekee nchini iliyoanzishwa mwaka 1980 ambayo imebahatika kuwa na vifaa vyote asilia na muhimu katika utamaduni na historia ya mtanzania hali ambayo inaitofautisha makumbusho hii na nyingine zilizopo hapa nchini ”,anasisitiza Mhifadhi huyo. Naye Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa Philipo Maligisu anabainisha zaidi kuwa Mji wa Songea ni miongoni mwa miji michache nchini ambayo ilitoa upinzani mkali katika vita ya Majimaji na kwamba katika makumbusho hayo kuna ushahidi ambao unaonesha moja kwa moja kuwa wazee wa Songea walishiriki kikamilifu katika vita hivyo.


Anabainisha zaidi kuwa katika eneo la mashujaa wa majimaji yamejengwa majengo mbalimbali ambayo yamehifadhiwa vifaa ambavyo ni mila na utamaduni wetu vilitumiwa na mashujaa hao ili kuwaletea watanzania uhuru.

Maligisu anasema ndani ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji kuna mnara wa kumbukumbu ya wanajeshi ambao walitoka Songea kwenda kupigana vita ya Idd Amini kati ya mwaka 1978 hadi 1979 ambapo wakati wanarudi baada ya kushinda vita hiyo walipata ajali mbaya na kufariki dunia askari wote 56 katika milima ya Lukumbulu wilayani Songea.


Amesema Ili kuwakumbuka mashujaa hao serikali ilijenga mnara katika eneo Makumbusho ya Taifa ya Majimaji ambako walizikwa mashujaa wa vita ya majimaji kama sehemu ya kuwakumbuka hivyo kurithisha mila,ushujaa na utamaduni wa mtanzania.

Kulingana na sera ya utamaduni ya mwaka 1997 pamoja na sheria ambayo inayatambua maeneo haya serikali imeamua mji wa Songea uingizwe katika vivutio vya utalii wa kiutamaduni kwa ajili ya kuendeleza historia ya Mji wa Songea ili uwe wa kihistoria, kishujaa na kiutamaduni.

Utafiti uliofanywa na Makumbusho ya Taifa umebaini kuwa mji wa Songea una vigezo vyote vya kuingizwa katika rasilimali za kiutamaduni za taifa,ili kuhakikisha kuwa watalii wengi wa ndani na nje ya nchi wanafika katika makumbusho hayo ili kujifunza utamaduni wa mtanzania.

Hali ya mila,utamaduni na desturi iliyopo kwa vijana wa sasa katika nchi yetu ni mbaya kwa kuwa vijana wengi wamesahau utamaduni mila na desturi za mtanzania na kuendekeza mila za kigeni ambazo zimeharibu kabisa maadili mema ya mtanzania.

Mbunge Jimbo la Nyasa Injinia Stella Manyanya anasema uhamasishaji wa kufufua utalii wa kiutamaduni kusini unaendelea ili kuhakikisha watu wa rika zote wanatembelea vivutio mbalimbali za utalii ikiwemo Makumbusho ya Taifa ya Majimaji. Injinia Manyanya ameipongeza Idara ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji kwa kuandika barua kwa wakuu wa shule katika mkoa wa Ruvuma ili kuhakikisha wanafunzi wanapata nafasi ya kutembelea vivutio vya utalii na kujifunza mambo mbalimbali ili kupenda utalii tangu wakiwa wadogo.
katikati mwenye suti ya bluu ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI Mheshimiwa David Silinde alipotembelea Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea
Ngoma halisi ya kabila la wangoni inayoitwa Ligihu ambayo ipo hatarini kutoweka kwa sababu wanaocheza ni wazeeSanamu ya askari iliyojengwa ndani ya makumbusho ya Taifa ya Majimaji,sanamu hii imejengwa kuwakumbuka askari wa JWTZ wapatao 56 waliofariki dunia  eneo la Lumbule Songea wakati wanarudi katika vita ya  Kagera mwaka 1979

0 comments: