DC BULEMBO APIGA MARUFUKU UTOAJI RISITI ISIYO NA NAMBA YA GARI NA MUDA MUHEZA

 Na Mwandishi Wetu


MKUUkuu wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga Halima Bulembo amepiga marufuku utoaji wa risiti za ushuru wa stendi ambazo hazioneshi namba za basi wala muda
wa kuondoka katika stendi ya Muheza.

Bulembo amepiga marufuku hiyo jana alipotembelea stendi hiyo
 kuona shughuli zao za kila siku ambapo aligundua uwepo wa changamoto kwenye  utoaji risiti katika stendi hiyo.

Baadhi ya changamoto alizogundua ni  suala la utoaji wa risiti za mashine kwa magari  yanayopita katika stendi hiyo ambapo Mkuu wa Wilaya hiyo alibaini risiti za EFD zinazotolewa hazionyeshi muda au namba za
mabasi yaliyopewa risiti hizo.

Kutokana na changamoto hiyo Bulembo amesema pia atakutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Muheza pamoja na Wasimamizi wa ushuru katika stendi hiyo ili kuliangalia kwa undani jambo hilo aliloliita kuwa ni uhujumu wa wa mapato ya
Halmashauri.

Amesema inashangaza kuona kuwa watu waliopewa jukumu la kusimamia
taratibu na sheria  hawafanyi hivyo. “Kwa mfano mtu anapita hapa saa nne na nusu halafu anapewa risiti inayoonyesha amepita saa nne na ambayo haina namba za gari ?” Alihoji.

Aliyekuwa Msimamizi wa ushuru katika stendi hiyo aliyejitambulisha kwa jina la
Abbas  (al maarifu kama ‘Kidevu)’ amesema wakati walipokuwa wanaatumia risiti za kawaida walikuwa wanaandika namba za gari,
muda na namba ya mlipa kodi lakini baada ya kuingia risiti za mashine walianza kukata risiti kwa wingi anayetoa ushuru anapewa risiti yoyote ile ambayo haina jina, namba wala muda.

Kwa upande wake Msimamzi  wa sasa  katika Stendi hiyo  Omari Hatibu Semboza amethibitisha kuwepo wa changamoto hiyo kwenye utoaji risiti. Hata hivyo Msimamizi huyo amesema wanakabiliwa na changamoto ya kuwa na mashine moja,tatizo la umeme, stendi na watumishi wachache (watatu ambao wanatakiwa kuhudumia stendi tatu).



0 comments: