MAREKANI YAAZIMIA KUZUIA USHINDI MKUBWA WA JESHI LA SYRIA, ALEPPO

Wakati habari na ripoti mbalimbali zinaeleza kuwa makundi ya kigaidi yanakaribia kushindwa kikamilifu katika eneo la mashariki mwa mji wa Aleppo nchini Syria, Marekani inafanya jitihada kubwa za kuhakikisha inazuia ushindi wa jeshi la Syria dhidi ya magaidi hao.
Jeshi la Syria likisaidiwa na ndege za kijeshi za Russia na washauri wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran linakaribia kupata ushindi mkubwa huko Aleppo ambayo imekuwa miongoni mwa ngome kuu za makundi ya kigaidi nchini Syria kwa kipindi cha zaidi miaka 5 sasa. Kukombolewa eneo la mashariki mwa Aleppo hautakuwa mwisho wa uhai wa makundi ya kigaidi nchini Syria lakini ni hatua kubwa katika uwanja huo. Kwa msingi huo wasaidizi na waungaji mkono wa makundi hayo ya kigaidi, hususan Marekani na Saudi Arabia, katika siku za hivi karibuni wanafanya jitihada kubwa za kuishawishi Russia ikubaliane na usitishaji vita nchini Syia. Kama ilivyokuwa huko nyuma ambapo Marekani ilikuwa ikitumia kisingizio cha kutokea maafa ya kibinadamu na kutoa wito wa kusitishwa vita wakati inapoona magaidi wanakaribia kuangamizwa, mara hii pia Washington inataka kutumia kisingizio na mbinu hiyo hiyo.
Jeshi la Syria linaendelea kupata ushindi Aleppo
Pamoja na hayo na licha ya serikali ya Russia kukubali wazo la kufanyika mazungumzo mapya ya kusimamisha vita huko Aleppo, lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov amesisitiza kuwa, Washington imechukua misimamo ya kustaajabisha na inayogongana kuhusu suala la kuwaruhusu raia kuondoka kwenye medani ya mapigano katika eneo hilo.
Misimamo hiyo ya kustaajabisha na ya kukinzana ya Marekani ni kielelezo kwamba, Washington umekiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba eneo la mashariki mwa Aleppo limekombolewa kutoka kwenye makucha ya makundi ya kigaidi. Kwa utaratibu huo, Marekani inatoa wito wa kusitishwa mashambulizi ya jeshi la Syria na waitifaki wake huko Aleppo kwa shabaha ya kuokoa si maisha ya raia wa kawaida wa Syria bali magaidi wanaohaha wakikimbia huku na kule na hatimaye kuzuia kushindwa kikamilifu makundi hayo katika siku za mwishoni mwa uongozi wa Rais Barack Obama.
Rais Barack Obama wa Marekani
Kufeli kwa mazungumzo ya awali kati ya Marekani na Russia juu ya vita nchini Syria ambako ni matokeo ya siasa zinazogongana na serikali ya Washington, kumelifanya jeshi la Syria lizidishe juhudi za kulikomboa eneo la mashariki mwa Aleppo na sasa ni robo tu ya mashariki mwa eneo hilo ndiyo iliyobakia katika makucha ya magaidi hao wanaoungwa mkono na Marekani, Israel, Saudi Arabia na washirika wao.  
Licha ya kukabiliana na changamoto mbili kubwa katika vita vya Aleppo, yaani changamoto ya hali ya raia wa kawaida kutokana na idadi yao kubwa na msongamano wa nyumba na vilevile hatua ya makundi ya upinzani na kigaidi ya kukataa kusalimu amri, lakini jeshi la Syria linaendeleza operesheni hiyo kwa tadbiri ya hali ya juu na umakini mkubwa.
Idadi kubwa ya raia na msongamano wa nyumba, tatizo kuu katika vita vya Aleppo
Hapana shaka kuwa katika siku zijazo pia Marekani itaendelezajuhudi za kutaka kuzuia ushindi kamili na mkubwa wa jeshi la Syria huko Aleppo. Katika uwanja huo ripoti zinasema kuwa, Rais Barack Obama wa Marekani ameondoa baadhi ya vizuizi vya kuwatumia silaha za kisasa waasi na magaidi katika vita vya kukomboa mji wa Raqqah. Kwa hatua hiyo ya Obama, sasa Marekani inaweza kutoa silaha zaidi kwa makundi ya waasi ambayo yako tayari kushiriki katika vita dhidi ya serikali ya Syria katika mji wa Raqqah

0 comments: