![]() |
| Mwakilishi wa Tazania Kudumu UN Tuvaco Manongi akizungumza katika kikao hicho |
TANZANIA YAITAKA DUNIA IWEKEZE KATIKA MAENDELEO BADALA YA ULIMBIKIZAJI WA SILAHA
Posted by khamisimussa77@gmail.com at 10:15 AM
Na Mwandishi Maalum, New York
Tanzania
imeitaka Jumuiya ya Kimataifa kupunguza matumizi makubwa katika
kujilimbikizia silaha zikiwamo za maangamizi na badala yake fedha hizo
zielekezwe katika kusaidia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu
( agenda 2030).
Wito
huo umetolewa siku ya jumanne na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania
katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, wakati Kamati ya Kwanza
ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inayohusika pamoja na mambo
mengine, usalama wa kimataifa likiwamo suala ya upokonyaji wa silaha
ilipokuwa ikijadilia ajenda ya upokonyaji silaha.
“
Kila Septemba 26 ya kila mwaka, tunaadhimisha siku ya kimataifa ya
kumaliza kabisa silaha za nyukilia. Lakini wakati Kamati hii ikianza
mijadala yake hakuna hatua yoyote ya maana iliyochukuliwa ya
kulimaliza tatizo hili” akasema Balozi Manongi na kuongeza, badala
yake dunia inashuhudia nchi ambazo zinazomiliki silaha za nyukilia
zikiendelea na kasi ya kuziongeza ikiwa ni pamoja na kuwekeza
mabilioni ya dola katika kuzifanyia marekebisho na kuziimarisha.
“Kwa
Tanzania, upokonyaiji wa silaha na maendeleo ni mambo yanayohusiana.
Kiasi cha fedha ambacho kinaelekezwa katika matumizi ya kijeshi
yangeweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa malengo ya
maendeleo endelevu. Ni kwa sababu hiyo tunaona umuhimu wa kazi za
Kamati hii”.Amesisitiza Balozi.
Akizungumzia
nafasi ya Umoja wa Mataifa katika kusimamia suala na upokonyaji wa
silaha kupitia Taasisi zake, Balozi amesema licha ya ugumu na
changamoto katika eneo hilo. Tanzania bado inamatumaini ya Umoja wa
Mataifa kama chombo muhimu kinachoweza kudhibiti usambaaji wa silaha
za maangamizi zikiwamo silaha ndogo ndogo, za kati na nyepesi.
Pamoja
na kuelezea namna Nchi zenye silaha za maangamizi zinavyoendelea
kujilibikizia silaha hizo ikiwani ni pamoja na kuziimarisha ili ziwe
za kisasa. Balozi pia ametumia fursa hiyo kutahadharisha dhidi ya
hasara za kibinadamu zinazoweza kutokea dhidi ya matumzi ya silaha
hizo.
Na
kwa sababu hiyo, Tanzania imezisihi nchi zinazomiliki silaha za
nyukilia kutumiza wajibu wao kisheria ikiwa ni pamoja na kuchukua
hatua za kuangamiza silaha hizo kwa uwazi na bila kuchelewa na kwa
kuzingatia makubaliano ya Mkataba wa Kimataifa wa upokonyaji wa
silaha.
Tanzania
pia imekumbushia haja na umuhimu wa nchi ambazo hazina silaha za
nyukilia kutonyimwa fursa ya kutumia teknolojia ya nyukilia kwa
shughuli salama zikiwamo za utafiti na shughuli nyingine za
maendeleo na ustawi wa nchi zao.
Kuhusu
Ukanda Huru zisizokuwa na silaha za nyukilia, Tanzania ambayo ni
nchi mwanachama wa Mkataba wa Palendaba (Africa Nuclear Free Zone)
inaunga mkono uwepo wa Kanda huru ambazo hazina silaha za nyukilia.
Katika
hatua nyingine , Tanzania imekaribisha kuanzishwa kwa Benki ya
Teknolojia kwa nchi zilizonyuma kimaendeleo ( Technology Bank for
Least Developing Countries).
Kuanzishwa
kwa bank hiyo kunalenga pamoja na mambo mengine kuzisaidia nchi za
LDC’s kuwa na fursa na uwezo wa kutumia teknolojia sahihi kutoka kwa
mataifa yaliyoendelea.
Hayo
yameelezwa na Bw. Songalieli Shilla, Afisa Mkuu Mambo ya Nje katika
Uwakilishi wa kudumu wa Tanzania wakati alipochangia kwa niaba ya
Tanzania majadiliano ya Kamati ya Pili ya Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa ilipokuwa ikijadili masuala mtambuka yakiwamo ya ukuaji wa
uchumi na maendeleo.
Tanzania
ikasisitiza kwamba kuanzishwa kwa Banki hiyo kutazisaidia nchi
za LDC’s kuingia katika ushindani na mataifa yalioendelea. Na kwamba
Tanzania inafarijika pia kwamba Benki hiyo itaendelea kuzisaidia
hata zile nchi ambazo zitakuwa zimefunzu kutoka nchi zenye uchumi wa
chini na kwenda kwenye uchumi wa kati.
Benki
hiyo ambayo chimbuko lake ni mkutano uliofanyika mwaka 2011 nchini
Uturuki na ambayo tayari maandalizi ya awali yamekwisha kufanyika
inatarajiwa kuzinduliwa mwakani.
Kamati
ya Pili ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inahusima na masuala ya
Uchumi na Fedha, na katika mkutano huo, pamoja na kukaribisha
uanzishwaji wa Benki hiyo, pia Tanzania imezungumzia changamoto
mbalimbali ambazo zinakweza kukwamisha utekelezaji wa ajenda ya
maendeleo endelevu hususani kwa nchi zinazoendelea.
Amezitaja
baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na mabadiliko ya tabia
nchi, upatikanaji wa raslimali fedha kutoka vyanzo vya ndani na
kutoka kwa wadau na washirika wa maendeleo.
Baada
ya kukamilika kwa Mkutano na Majadiliano ya jumla ya Baraza Kuu la
71 la Umoja wa Mataifa, mkutano uliowakutanisha viongozi wakuu wa
Nchi na Serikali kutoka mataifa mbalimbali duniani. Nchi wanachama
wa Umoja wa Mataifa, kupitia Kamati Sita zinazounda Baraza Kuu la
Umoja wa Mataifa, zimeingia katika ngwe nyingine muhimu ambapo sasa
wajumbe wanakutana kupitia Kamati hizo kujadiliana agenda na
maazimio mbalimbali kuanzia yale yanayohusu uchumi, fedha na
maendeleo, haki za binadamu, ustawi wa jamii, Amani na usalama,
umalizwaji wa ukoloni, utawala wa sheria , sheria za kimataifa na
bajeti na utawala.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

0 comments: