DK. KAMALA AWA MWENYEKITI MABALOZI WA AFRIKA UBELIGIJI
Posted by khamisimussa77@gmail.com at 6:53 AM
Balozi Joel M Nheleko wa Swaziland
nchini Ubeligiji, ambaye alikuwa Rais wa Mabalozi wa Afrika nchini
Ubeligiji aliyemaliza muda wake, akimkabidhi Balozi wa Tanzania Dk.
Diodorus Kamala mfuko wenye vitendea kazi kama ishara ya kumkabidhi
Urais wa Mabalozi wa Afrika Ubeligiji jijini Brussels juzi.
**** ****
Balozi wa Tanzania nchini Ubeligiji,
Dk. Diodorus Kamala ameteuliwa na mabalozi wa nchi za Africa
wanaoziwakilisha nchi zao nchini humo kuwa Mwenyekiti wao.
Balozi Kamala amepokea uenyekiti huo
kutoka kwa Balozi wa Swaziland nchini Ubeligiji, Joel Nheleko
aliyemaliza muda wake. Tanzania itashikilia kiti hicho kwa muda wa miezi
sita hadi Julai 1, 2013.
“Nimefurahi kupewa heshima hii, na
naamini nitaitumia fursa hii kufahamiana vizuri na mabalozi wenzangu na
kuvutia fursa za kiuchumi kwa nchi yetu,” alisema Balozi Kamala.
Wakati huo huo, juzi mabalozi wa nchi
tano zinazozunguka Bonde la Ziwa Tanganyika, walimchagua Balozi Kamala
kuwa mwenyekiti wao.
Nchi wanachama wa Bonde la Ziwa Tanganyika ni Burundi, Rwanda, Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Zambia.
Nchi hizi zimeunganisha nguvu
kutafuta wafadhili kwa ajili ya maendeleo ya Bonde la Ziwa Tanganyika,
ambapo eneo la bonde hili lenye wakazi wastani wa milioni 40 wanalenga
kuliendeleza kwa ajili ya kujenga miundombinu, kurahisisha usafiri na
usafirishaji, kujenga reli mpya na kuendeleza utalii.
Chini ya mpango huu wanalenga pia
kuboresha viwanja vya ndege vya nchi wanachama vya Mbala, Kalemie,
Bujumbura, Kigoma na Kasanga kwa nia ya kurahisisha usafiri wa anga
katika ukanda huu.
Dk. Kamala amekabidhiwa jukumu la kuratibu mpango huu na kwa pamoja watatafuta fedha kutoka kwa wafadhili kwa ajili ya mradi huu
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: