SERIKALI IMETENGA SHILINGI BILIONI 11.4 KUBORESHA WAKALA WA NDEGE ZAKE

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akiongea na wajumbe wa Menejimenti ya Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) (hawapo pichani) wakati wa ziara yake kwenye taasisi hiyo jijini Dar es Salaam. Anayemsikiliza ni Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo Bwana Tito Kasambala
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bwana Richard Mayongela (kushoto) akimkaribisha Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (kulia) kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua Wakala wa Ndege za Serikali
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akipanda kukagua mojawapo ya ndege za Wakala wa Ndege za Serikali inayosafirisha viongozi wa ngazi ya juu wa Serikali wakati wa ziara yake kwa Wakala hiyo kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam
Mkaguzi Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali Mhandisi Bernard Mayila akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye wakati akifanya ukaguzi ndani ya ndege mojawapo inayosafirisha viongozi wa ngazi za juu wa Serikali wakati wa ziara yake alipotembelea Wakala hiyo kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akiteremka baada ya kukagua mojawapo ya ndege za Wakala wa Ndege za Serikali wakati wa ziara yake kwenye Wakala hiyo kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam

……………….

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kuboresha Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) ambayo inasimamia na kuendesha ndege ambazo zinasafirisha viongozi wa kitaifa wa Serikali

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye wakati wa ziara yake ya kikazi alipotembelea na kukagua utekelezaji wa majukumu ya Wakala wa Ndege za Serikali ambayo inasimamia na kuendesha ndege ambazo zinasafirisha viongozi wa kitaifa wa Serikali ambapo alizungumza na Menejimenti na wafanyakazi na kuwaeleza kuwa Serikali imejipanga kuboresha Wakala hiyo

Mhandisi Nditiye alisema kuwa azma ya Serikali ya Awamo ya Tano inayosimamiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ni kuhakikisha kuwa Taasisi za Serikali zinafanya kazi zake kwa weledi na uadilifu ili kufanikisha malengo ya Serikali ya kuwatumikia wananchi. “Serikali inatambua umuhimu wa Wakala hii na ina imani kubwa nanyi katika kuhakikisha kuwa mnafanya kazi zenu za kusafirisha viongozi kwa usalama na kwa uhakika ili waweze kutimiza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi na tayari ina nia ya kuboresha taasisi hii”, amesema Mhandisi Nditiye.

Naye Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TGFA Bwana Tito Kasambala amemueleza Mhandisi Nditiye kuwa taasisi yake ina ndege nne ambazo zinatumika kusafirisha viongozi wa kitaifa wa Serikali katika kutimiza majukumu yao ya kuwatumikia watanzania na tayari Serikali imetenga shilingi bilioni 11.4 kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/18 kwa ajili ya shughuli mbali mbali za Wakala ikiwemo matengenezo ya ndege, mafunzo kwa wanahewa na ukarabati wa karakana.

Mhandisi Nditiye amewaeleza wajumbe wa Menejimenti na wafanyakazi wa Wakala hiyo kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wao na umuhimu wa wahandisi wa ndege na marubani wa kupata nafasi ya kuendesha ndege na kozi za mafunzo mbali mbali kuendana na taaluma zao ambapo tayari makubaliano yamefanyika baina ya Wizara na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ya kuwapatia nafasi marubani wa ndege za Wakala wa Ndege za Serikali nafasi ya kurusha ndege mara kwa mara ili kuendana na matakwa ya taaluma zao.

Ameongeza kuwa Serikali inashughulikia suala la miundo ya watumishi wa umma ambapo Wakala wa Ndege za Serikali ni mojawapo ya taasisi ambayo muundo wake unafanyiwa kazi ili kuweza kuzingatia taaluma, kada za watumishi na maslahi yao. “Natumaini wote mnatambua na kuelewa kuwa kipindi cha hapo nyuma kidogo utumishi wa umma uliingiwa na baadhi ya watu wachache ambao walikuwa wanafanya ujanja ujanja na kuharibu utumishi wa umma ambapo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu, imelifanyia kazi jambo hili na ameunda bodi maalumu ambayo inafanyia kazi suala la muundo, kada na maslahi ya watumishi wa umma,” amesema Mhandisi Nditiye.

Aidha, wafanyakazi wa Wakala wa Ndege za Serikali wamemuomba Mhandisi Nditiye kuwasilisha ombi lao kwa Serikali la kuwaongezea mishahara yao kuendana na hali ya soko la ajira ya marubani ilivyo nchini kwa sasa.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

0 comments: