Kwa wakati huo, bandari ya Zanzibar ndiyo iliyokuwa kubwa Afrika
mashariki. Pia Zanzibar, ilikuwa ndiyo kituo kikuu cha biashara katika
eneo zima la Afrika mashariki na Maziwa Makuu.
Meli za mataifa ya nje hasa Marekani, Uingereza, Ufaransa na Italia
zilitia nanga bandarini Zanzibar kupakia na kupakua bidhaaa mbalimbali.
Pia meli nyingi zilifika Zanzibar kuchukua maji safi ya kunywa yatokayo
katika chemchem ya Mwanyanya. Meli hizo zilitoa ajira ya muda ya
kusafisha mashine na kupangusa moshi. Mara nyingi mabaharia wa meli hizo
waliajiri watoto kuwachukulia vikapu vya kununulia vyakula sokoni na
kuwalipa ujira mdogo.
Kwa vile alipendelea kazi ya ubaharia, Abeid Amani Karume alifuatana na
bwana mmoja aitwae Juma hadi bandarini. Alijumuika na watoto kadhaa
waliofuata ajira ya muda huko bandarini. Ajira ya muda aliyoipata Karume
huko bandarini ilimfanya akutane na mabaharia wa nchi mbalimbali na
hivyo kuvutiwa na uzuri wa maisha ya ubaharia ya kusafiri na kuona nchi
na watu mbalimbali. Hali hiyo ilimfanya Karume azidi hamu na ari ya
kutafuta kazi ya ubaharia na kumuomba mama yake ruhusa ya kufanya kazi
melini. Mwanzoni mama yake mzazi alikataa shauri hilo. Lakini baadaye
alikubali ombi hilo baada ya kufahamishwa kuwa meli atakayofanyakazi
mwanawe haitosafiri mbali na itatia nanga bandarini Zanzibar mara kwa
mara.
Katika mwaka 1919 Abeid Amani Karume alipeleka barua ya kuomba kazi
melini lakini alikataliwa kwa vile alikuwa na umri mdogo wa miaka 14.
Hata hivyo hakuvunjika moyo na hakurudi Mwera kwa mama yake bali
alimtembelea mara kwa mara. Alijiunga na timu za masumbwi na mpira wa
miguu na kujuana na watu mbalimbali.
Kwa wakati huo timu za mpira wa miguu zilizojulikana Unguja zilikuwa ni
timu ya skuli ya Kiungani iliyoanzishwa na Mwalimu Augostino Ramadhani
na John Majaliwa. Mara nyingi timu hiyo ilishindana na timu ya watumishi
serikalini. Baadaye kuliundwa timu nyengine za mpira wa miguu ambazo ni
Vuga Boys, New Generation, United Service na New Kings. Karume
alijiunga na timu ya New Generation na kucheza nafasi ya mstari wa mbele
kushoto Inside left. Baadhi ya waanzilishi wa timu hiyo ni Bwana
Malingumu, Shaaban Feruzi, Saad Shoka, Masoud Thani na Mzee wa Shangani.
Mara tu baada ya kujiunga na timu hiyo, Karume alichaguliwa kuwa
msaidizi nahodha. Katika mwaka 1920 Abeid Amani Karume alikubaliwa kuwa
baharia katika meli iliyoitwa Golden Crown (Taji la Dhahabu). Meli hiyo
ilichukua abiria na mizigo kati ya bandari ya Zanzibar, Dar es Salaam,
Pemba, Tanga, Mombasa na Mikindani huko Kilwa.
Baadaye alishuka katika meli hiyo na kufanya kazi katika meli nyengine
iliyoitwa Cheko. Kwa bahati mbaya, meli hiyo iligonga mwamba na
kuvunjika huko Kimbiji, nje kidogo ya Dar es Salaam lakini watu wote
walinusurika.
Kazi ya ubaharia ilimpa tija Abeid Amani Karume kwani alinunua nyumba na
viwanja kila alipopata nafasi ya kwenda nyumbani. Kwa muda wote huo
Abeid Amani Karume alifanyakazi katika meli zilizopata leseni ya
kufanyakazi katika mwambao wa Afrika Mashariki.
Katika mwaka 1922, akiwa na umri wa miaka kumi na saba, Abeid Amani
Karume alipata kazi katika meli ya kampuni ya British Indian Steam
Navigation Company ya Uingereza. Akiwa na kampuni hiyo Karume, alikaa
nje miaka mitatu hadi 1925, aliporejea nyumbani kwa mapumziko.Tayari
wakati huo, Karume alikwishatembelea nchi za
Japan,Comoro,Madagascar,China,Singapore,New Zealand,Uingereza,Marekani,Canada,Ufaransa, Ubelgiji, India,Ureno,Hispania,Arabuni,Italia na Ugiriki.
Baada ya kupumzika kwa muda, Abeid Amani Karume alijiunga na kampuni ya
Eastern Telegraph Company na kufanya kazi katika meli ya kampuni hiyo
iitwayo Caranja. Meli hiyo ilikuwa ikitandika waya za simu baharini kati
ya Zanzibar na Aden. Aliendelea na kazi ya ubaharia hadi mwaka 1938
alipoacha kazi hiyo kutokana na sababu mbalimbali. Karume alishauriwa na
mama yake mzazi kuacha kazi hiyo. Vilevile aliacha kazi hiyo kutokana
na kuzorota kwa hali ya usalama duniani. Wakati huo, tayari vita vikuu
vya pili vya dunia vilikaribia. Baadhi ya kazi alizofanya katika meli
hizo ni Greaser, Fireman, Sailor na Headsailor.
Katika kipindi fulani cha kazi yake ya ubaharia, Abeid Amani Karume
alifanyakazi chombo kimoja na Khamis Heri Ayemba kutoka Tanga. Wote
wawili walirudi nyumbani wakati vita vya pili vya dunia vinakaribia.
Baada ya kuacha kazi hiyo,Khamis Heri Ayemba alijihusisha na biashara
huko kwao Tanga na kuwa tajiri mkubwa. Wakati wa kudai uhuru, Ayemba
alishirikiana na Peter Muhando na Mwalimu Kihere kuunda tawi la TANU
huko Tanga. Tarehe 23 Oktoba, 1955 wanachama wa mwanzo wa TANU huko
Tanga walikutana kuchagua uongozi wa chama hicho. Katika uchaguzi huo,
Khamis Heri Ayemba alichaguliwa kuwa Mwenyekiti na Peter Muhando
alichaguliwa kuwa katibu.
Kutokana na kusafiri sehemu mbalimbali duniani, Abeid Amani Karume
alijifunza mengi ya kimaisha na kuona jinsi gani mataifa ya ulaya na
mabepari walivyotumia hila na ujanja kuzinyonya nchi za Afrika. Katika
safari zake za ubaharia alikumbana na matatizo kadhaa. Tatizo kubwa
zaidi alokumbana nalo ni dhoruba kali sana iliyoikumba meli yao wakati
wakitokea Australia kwenda Lorence Marques (Msumbiji).
Katika miaka ya 1930, timu za mpira wa miguu Zanzibar zilikabiliwa na
mgawanyiko. Kutokana na mgawanyiko huo, ndipo hapo mwaka 1931 timu zote
za New Kings, Vuga Boys, United Service na New Generation zilipoungana
na kuunda umoja wa michezo wa waafrika uloitwa "African Sports Club".
Timu hiyo ilikuwa na "A" na "B", ambapo Karume alikuwa timu "A"
iliyokuwa ya kwanza mwaka huo kwenda Tanganyika kucheza mechi ya
kirafiki.
Umoja huo haukwishia hapo kwani katika mwaka 1934 uliundwa umoja wa
Waafrika (African Association). Umoja huo wa Waafrika ndiyo ulogeuka
kutoka kwenye michezo na kuwa umoja wa kisiasa.
Katika mwaka 1938 bandarini Zanzibar palikuwa na vijana wa Kiafrika
walounda umoja uliyoitwa “Motorboats Association”. Vijana hao walikuwa
wakivusha abiria kutoka bandarini hadi melini kwa kutumia mashua, kazi
ambayo iliwasaidia kupata pesa chache za kuendeshea maisha. Lakini
baadaye walijitokeza wafanyabiashara wajanja wenye asili ya Asia wenye
uwezo na kununua boti za mashine na kuvusha abiria. Wafanyabiashara hao,
walitumia mbinu ya kuungana na waafrika katika biashara hiyo.
Baada ya muda mfupi wafanyabiashara hao wenye asili ya Asia waliunda
chama chao kilichoitwa Syndicate. Taratibu wafanyabiashara hao
waliwaingiza ndugu zao na wale waafrika waanzilishi waligeuzwa vibarua
na kulipwa ujira mdogo sana. Abeid Karume aliwakusanya waafrika hao
kudai haki zao na kufanikiwa kufanya mapatano na waasia hao. Wamiliki wa
maboti hao, walikubali kuwalipa waafrika asimilia 40% ya mapato yote na
wao walichukua asilimia 60% na kugharamia uendeshaji na matengenezo ya
boti hizo.
Baada ya mafanikio hayo Abeid Amani Karume alipata sifa nyingi na mwaka
1939 alianzisha harakati za kuunda chama cha mabaharia Zanzibar ili
kupigania haki za wafanyakazi hao. Kwa wakati huo ilikuwa vigumu sana
kuwashawishi watu wasojua mipango ya vyama vya wafanyakazi. Hivyo basi
mwishoni mwa mwaka huo wa 1939 baadhi ya wafanyakazi waloshauriwa
kuanzisha umoja huo walikataa kushiriki katika umoja huo. Karume
hakusita na juhudi zake za kuanzisha umoja huo. Mwaka huohuo wa 1939,
alionana na mzungu aitwae Bwana Douglas Basil Berber aliyekuwa Inspekta
wa polisi kuomba kibali cha kuanzisha chama cha mabaharia wa Unguja na
Pemba.
Mzungu huyo alimshauri Abeid Karume awakusanye wale wote wanaotaka
kuanzisha chama hicho na wajiunge kwa mujibu wa sheria za India.
Zanzibar kwa wakati huo haikuwa na sheria kuhusu vyama vya wafanyakazi
Waafrika.
Baada ya kuwashauri wenzake, Abeid Karume alipata watu sita walokubali
kujiunga na jumuiya hiyo. Watu hao ni Bakari Jabu, Miraji Mselem, Juma
Maalim, Ismail Mbarouk, Mbarouk Salim na Kitwana Suwedi. Chama cha
Mabaharia wa Unguja na Pemba kilipata usajili tarehe 30 Ogosti, 1949 na
Makao Makuu yake yalikuwa Kisima majongoo.
Sheria ya vyama vya wafanyakazi vya Zanzibar ilipitishwa mwaka 1931.
Baadaye katika mwaka 1941, sheria hiyo ilifanyiwa mabadiliko na kuwa
Sheria Nambari 3 ya vyama vya wafanyakazi.
Jumuiya za mwanzo za wafanyakazi kuanzishwa Zanzibar ni pamoja na
Jumuiya ya Mabaharia, Jumuiya ya Wachukuzi na Umoja wa Watumishi wa
Majumba ya Wazungu. Hadi kufika mwaka 1951 tayari chama cha mabaharia
kilikuwa na wanachama 83. Tarehe 26 Oktoba 1959, Abeid Karume ambaye ni
muasisi wa jumuiya ya mabaharia aliacha uongozi wa jumuiya hiyo na
kujihusisha zaidi na siasa katika chama cha ASP ,lakini aliendelea kuwa
mdhamini wa jumuiya hiyo. Kabla ya hapo katika mwaka 1942, Karume
alikuwa katibu wa African Association na Rais wa Jumuiya hiyo hapo mwaka
1953. Baadaye nafasi hiyo ilishikiliwa na Bwana Herbert Barnabas.
Kwa mara ya kwanza Sheikh Abeid Karume alifunga ndoa na Bibi Pili binti
Ahmed Ambari mwanzoni mwa miaka ya Arubaini. Mke wake wa pili ni Bibi
Ashura binti Maisara. Baada ya kutengana na wake hao wawili, Sheikh
Karume alifunga ndoa na Bibi Fatma binti Gulamhussein Ismail (Fatma
Karume) katika mwaka 1944 mwishoni mwa mwezi wa Novemba, harusi ambayo
ilifanyika huko Bumbwini Misufini.
Bibi Fatma Gulamhussein Ismail alizaliwa Bumbwini mwaka 1929 akiwa ni
mtoto wa Bwana Gulamhussein Ismail na Bibi Mwanasha Mbwana Ramadhani.
Wazazi wa Bibi Fatma Karume ni wazaliwa wa Bumbwini. Bi Fatma Karume
alipata elimu ya msingi katika skuli ya Bumbwini na kuolewa mwaka mmoja
baada ya kumaliza masomo hayo. Mara tu baada ya kufunga ndoa, Bibi Fatma
Karume na Bwana Abeid Amani Karume walihamia mtaa wa Kisimamajongoo
nyumba Nambari 18/22 mjini Unguja kwa Sheikh Karume. Nyumba nyengine
mbili za Bwana Karume zilikuwa Gongoni na Michenzani.
Bi.Fatuma Karume alijifungua mtoto wa kwanza wa kike aliyeitwa Asha
katika mwaka 1946, lakini mtoto huyo alifariki siku ya pili yake. Mtoto
wa pili wa hayati Karume ni Amani Abeid Karume aliyezaliwa tarehe 1
Novemba, 1948. Mtoto wake wa tatu ni Ali Abeid Karume aliyezaliwa tarehe
24 Mei, 1950.
Mama yake mzazi Abeid Amani Karume, Bibi Amina binti Kadudu alifariki
dunia 1963 na kuzikwa katika makaburi ya Michenzani. Wake wengine ambao
waliolewa na Bwana Karume ni Bibi Nasra, Bibi Helemu na Bibi Fadya ambao
kila mmoja alizaa nae mtoto mmoja wa kike.
Mbali ya kuanzisha chama cha mabaharia pia Abeid Amani Karume alikuwa
muasisi wa Jumuiya ya Waafrika iliyoitwa African Dancing Club katika
mwaka 1940. Jumuiya hiyo ilikuwa na lengo la kuwaunganisha pamoja vijana
wa African Association.
Rais wa Jumuiya hiyo ya "African Dancing Club" alikuwa ni Bwana Pearcy
Baraka, Abeid Karume alikuwa Katibu Mkuu na Mweka hazina ni Mtumwa
Zaidi. Mbali ya kumiliki bendi ya muziki vilevile African Dancing Club
ilinunua banda la zamani ambalo lilibomolewa na kujengwa makao makuu.
Baadaye hapo tarehe 31 Januari, 1949 “African Dancing Club”
ilibadilishwa jina na kuitwa “African Youth Union”.
Kuundwa kwa chama cha Zanzibar Nationalist Party (Hizbu) mapema katika
miaka ya 50 na kutolewa kwa mapendekezo ya kufanyika uchaguzi mkuu wa
kwanza wa Zanzibar katika mwaka 1957 yaliwafanya viongozi wa Jumuiya ya
Waafrika African Association, na wale wa Shirazi Association waone
umuhimu wa kushirikiana. Viongozi hao waliona ulazima wa kuungana kuwa
kitu kimoja kupigania uhuru. Hivyo basi Jumuiya ya Shirazi Association
ilimtuma Bwana Haji Khatibu aliyekuwa rafiki mkubwa wa Abeid Amani
Karume apeleke shauri la kuunganishwa Jumuiya ya Waafrika na Jumuiya ya
Washirazi.
Kabla ya kukutana, kila jumuiya ilifanya kikao cha faragha kujadili
agenda ya mkutano. Shirazi Association walikubaliana kupendekeza jina la
Abeid Karume kutoka African Association kuwa Rais wa chama kipya
kitakachoundwa.
Nao African Association, walipanga kupendekeza jina la Sheikh Ameir Tajo
kutoka Shirazi Association kuwa Rais wa chama kipya kitakachoundwa.
Viongozi wa Jumuiya hizo walikubaliana kukutana kuanzia tarehe 1 hadi 5
Februari,1957. Mkutano ulifanyika kama ulivyopangwa hapo Mwembe Kisonge
nyumbani kwa Abeid Amani Karume chini ya Mwenyekiti wake Muhidini Ali
Omar. Kwa wakati huo, nyumba hiyo ya Abeid Karume alikuwa aliishi Hija
Saleh na Haji Ali Mnoga.
Mkutano huo ulimalizika jioni ya tarehe 5 Februari, 1957 kwa viongozi
hao kukubaliana kuunganisha Shirazi Association na African Association
na kuunda chama kilichoitwa Afro - Shirazi Union.
Baadaye chama hicho kiliitwa Afro - Shirazi Party, jina ambalo
lilitolewa na Ali Khamis kutoka Shirazi Association. Viongozi 18 wa
African Association na Shirazi Association walikutana na kuunda Afro
-Shirazi Party. Kumi ni kutoka African Association na Wanane kutoka
Shirazi Association. Viongozi wa African Association walikuwa ni Abeid
Amani Karume, Ibrahim Saadala, Abdalla Kassim Hanga, Bakari Jabu, Mtoro
Rehani Kingo, Rajabu Swedi, Ali Juma Seif, Mtumwa Borafia, Saleh Juma na
Saleh Mapete. Viongozi wa Shirazi Association ni Thabit Kombo Jecha,
Muhidini Ali Omar, Ameir Tajo, Ali Khamis, Haji Khatibu, Mdungi Ussi,
Ali Ameir na Othman Sharifu.
Katika mkutano huo pia alikuwepo mgeni mwalikwa Rais wa TANU, Mwalimu
J.K. Nyerere na Katibu Mkuu wa chama cha TANU, Bwana Zubeir Mtemvu. Pia
alihudhuria Bibi Maida Springer Kemp ambaye ni Mmarekani mweusi wa
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi wa Viwanda wa Marekani American
Federation of Labour Congress of Industrial Organization AFL - C 10.
Bibi Springer alikuwa ziarani barani Afrika kuangalia harakati za
ukombozi na alifuatana na Mwalimu Nyerere aliyepitia Zanzibar akielekea
Tanga kuitangaza TANU.
Chama cha Afro - Shirazi Party kilimteuwa Abeid Amani Karume kuwa Rais,
Mtoro Rehani Kingo kuwa Makamo na Thabit Kombo Jecha ni Katibu Mkuu.
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ni Ibrahim Saadala, Ali Khamis, Ameir Tajo,
Mtumwa Borafia na Muhidini Ali Omar. Baadaye wajumbe wa Shirazi
Association kutoka Pemba ambao ni Muhamed Shamte, Ali Sharif Mussa, Issa
Sharif, Suleiman Ameir na Hassan Ali waliitwa na kufahamishwa juu ya
kuunganishwa vyama hivyo.
Katika mwaka 1947 kuliundwa serikali za mitaa (Local Government) na
Baraza la Manispaa (Township Council) lilianzishwa 1954. Abeid Karume
alichaguliwa kuwa diwani (Councillor). Katika mwezi wa Juni 1957, Bwana
Karume alikwenda nchini Ghana kuhudhuria sherehe za uhuru wa taifa hilo.
Safari hiyo ilikuwa ni mwaliko wa kiongozi wa nchi hiyo, Bwana Kwameh
Nkrumah kwa vyama vyote vya kupigania uhuru barani Afrika.
Abeid Amani Karume alipendekezwa na chama cha ASP kuwa mgombea wa kiti
cha baraza la kutunga sheria wa jimbo la Ng'ambo, katika uchaguzi mkuu
wa kwanza wa Zanzibar wa 1957. Katika uchaguzi huo, Abeid Amani Karume
alijiandikisha katika jimbo la Ng'ambo kituo Nambari 84 ambacho ni Old
Shimoni School (Mao tse Tung) akiwa ni mfanyabiashara, mkaazi wa Kisima
Majongoo nyumba Nambari 18/22. Kadi yake ya kupigia kura ilikuwa Nambari
5818. Karume alishinda kiti hicho kwa kura 3,328 dhidi ya wapinzani
wake Ali bin Muhsin Barwan wa ZNP aliyepata kura 918 na Ibuni Saleh
mgombea binafsi aliyepata kura 55.
Hapo tarehe 15 Januari, 1960 Abeid Karume alishtakiwa na mfanyabiashara
aitwae Punja Kara Haji mkaazi wa Darajani mjini Unguja. Karume
alishtakiwa kwa madai ya kuvunja mkataba wa kukodi bekari ya
mfanyabiashara huyo.
Kesi hiyo Nambari 4 ya 1960 (Civil Case Number 4 of 1960) ilitayarishwa
na wakili Dinshaw Karai kwa niaba ya Punja Kara Haji. Ilidaiwa mbele ya
Jaji G.J. Horsfall wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kuwa hapo tarehe 17
Aprili,1958, Abeid Karume na Thabit Kombo waliingia mkataba na Punja
Kara Haji wa kukodi bekari ya Mchangani, nyumba nambari 2759 mali ya
Punja Kara Haji.
Mkataba huo ulieleza kuwa kodi hiyo itakuwa ni ya miaka mitatu kuanzia
tarehe 1 Mei 1958 kwa malipo ya Shilingi 7,395/20. Abeid Karume
alitakiwa alipe Shilingi 550/- kila mwezi. Waraka wa makubaliano hayo
ulotayarishwa na Wakili Dinshaw Karai ulitiwa saini hapo tarehe 18
Novemba, 1959 na Punja Kara Haji kwa niaba yake na Abeid Karume kwa
niaba yake na kwa niaba ya Thabit Kombo. Mkataba huo ulishuhudiwa na
mawakili Dinshaw Karai na Hemed Said.
Akiwasilisha madai dhidi ya Karume hapo tarehe 27 Januari, 1960 Punja
Kara Haji alidai kuwa tarehe 16 Novemba, 1959 Abeid Karume alifika
nyumbani kwake na kumueleza kuwa yeye na Thabit Kombo wanataka kuiacha
bekari hiyo kwa vile ilikuwa inawatia hasara.
Punja Kara Haji alieleza mahakama hiyo kuwa, baada ya kupata kauli hiyo
ya Abeid Karume walifikia makubaliano na mlalamikiwa. Abeid Karume
alitakiwa alipe Shilingi 7,395/20 kama ilivyo katika mkataba wao wa
tarehe 17 Aprili, 1958. Pia Karume alitakiwa akabidhi jengo la bekari
hiyo kwa mwenyewe hapo tarehe 31 Disemba, 1959. Akiendelea kutoa
ushahidi wake Punja Kara Haji alidai mahakamani kuwa yeye na Karume
walikubaliana fedha hizo Shilingi 7,395/20 zilipwe kwa awamu kwa
udhibitisho wa maandishi.
Awamu ya kwanza ya Shilingi 2,000/- ziwe zimelipwa ifikapo Disemba,
1959. Fedha zilizobaki Shilingi 5,395/20 zilipwe kidogo kidogo kwa
wastani wa Shilingi 500/- kila mwezi kuanzia tarehe 1 Januari, 1960.
Fedha hizo zilitakiwa ziendelee kulipwa kwa utaratibu huo kila siku ya
mwanzo ya kila mwezi. Punja Kara alidai kuwa Abeid Karume alishindwa
kulipa Shilingi 2,000/- hapo tarehe 1 Disemba,1959 na hakulipa Shilingi
500/-ilipofika tarehe 1 Januari,1960 kama walivyokubaliana. Kutokana na
madai yake hayo, Punja Kara Haji alidai mahakamani alipwe na Abeid
Karume Shilingi 7,395/20, asilimia 9% ya riba ya mwaka kuanzia tarehe ya
hukumu na alipwe gharama za kesi hiyo.
0 comments: