KUENEA MAGONJWA YA KUAMBUKIZA YEMEN SAMBAMBA NA JINAI ZA WASAUDIA

Katika hali ambayo kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza kama vile kipindupindu nchini Yemen kumepelekea makumi ya watu kupoteza maisha, makumi ya raia wengine wa nchi hiyo wanaendelea kupoteza maisha kutokana na hujuma za ndege za kivita za Saudia.
Ikitangaza habari hiyo hapo jana Alkhamisi Disemba 8, Wizara ya Afya ya Yemen imesema kuwa magonjwa ya kuambukiza yameenea katika mikoa 15 ya nchi hiyo na kusababisha vifo vya watu 89. Wakati huo huo jana ndege za kivita za Saudia na washirika wake ziliendeleza hujuma za kichokozi katika mji wa Sanhan na eneo la Bahlul katika mkoa wa San'aa na vilevile katika mkoa wa Saada na kusababisha maafa, majeraha na hasara kubwa katika maeneo hayo. Mbali na maafa ambayo yamesababishwa na hujuma hiyo ya kinyama ya Saudia ambayo imeingia katika mwezi wa 21 tokea ianzishwe, wananchi wa Yemen pia wamekuwa wahanga wa  magonjwa ya kuambukiza ambayo yameenea nchini humo kutokana na huduma duni za afya kutokana na kuharibiwa miundombinu muhimu ya nchi hiyo, ikiwemo ya afya katika uchokozi huo wa Saudia na washirika wake.
Hali mbaya ya afya Yemen kutokana na hujuma ya Saudia na washirika wake
Hujuma hiyo ya kijeshi imepelekea kuharibiwa asilimia 80 ya miundombinu hiyo muhimu katika maeneo ya mijini na hasa vituo vya afya na tiba. Mwezi Agosti mwaka huu, Shirika la Afya Duniani WHO lilitangaza kuwa ni asilimia 45 tu ya vituo vya afya vya Yemen ndivyo vinavyofanya kazi ikiwemo asilimia 37 pekee ya hospitali za nchi hiyo. Uhaba wa maji na chakula ni sababu nyingine ya kuenea magonjwa hayo ya kuambukiza, tatizo ambalo limekuwa kubwa zaidi kufuatia hujuma ya ndege za Saudia. Hali hiyo bila shaka imezidisha vifo vinavyotokana na magonjwa ya kuambukiza. Kuhusiana na suala hilo, katika ripoti yake ya hivi karibuni, Abdul Hakim al-Kahlani, mkuu wa kitengo cha kupambana na magonjwa ya kuambukiza katika Wizara ya Afya ya Yemen ametangaza kuwa watu 11 wamepoteza maisha yao kutokana na kipindupindu na wengine 78 kutokana na magonjwa ya utumbo au mfumo wa mmeng'enyo wa chakula.
Mauaji na uharibifu mkubwa wa miundombinu unaofanywa na Saudia nchini Yemen
Abdul Hakim al-Kahlani anaendelea kusema kuwa hivi sasa amepokea kesi za watu 138 wengine ambao wameathirika na kipindupindu katika mikoa 15 ya Yemen. Siku kadhaa zilizopita Shirika la Afya Duniani WHO lilitahadharisha kuhusiana na hatari ya kuenea kipindupindu nchini Yemen na kutangaza kuwa ugonjwa huo tayari umeathiri nusu ya mikoa ya nchi hiyo. Kwa kuzingatia hali hiyo ya kutisha, ndege za kivita za Saudia bado zinashambulia maeneo tofauti ya nchi hiyo. Kufikia sasa zaidi ya Wayemen 10,000 wamepoteza maisha yao moja kwa moja kutokana na mashambulio hayo ya kinyama. Jambo la kushangaza ni kuwa nchi za Magharibi ambazo zinapiga makelele na kusisitiza juu ya kusitishwa vita huko Halab nchini Syria ili kuwapa mwanya wa kupumua magaidi wanaotenda jinai na ukatili dhidi ya raia wa nchi hiyo, wamekaa kimya na kutofanya juhudi zozote za kusitisha hujuma ya Saudia nchini Yemen ili kuokoa maisha ya raia wasio na hatia wa nchi hiyo.

0 comments: